WAKUU WA MIKOA:Tulitegemea waokoaji, tukapata wazamishaji


Kondo Tutindaga's picture

Na Kondo Tutindaga - Imechapwa 21 September 2011

Printer-friendly version
Jamvi la Weledi

RAIS Jakaya Kikwete ameteua wakuu wapya wa mikoa. Kubwa katika uteuzi huo, ni kuwapandisha vyeo wakuu wa wilaya 15 na kuwafanya wakuu wa mikoa.

Ni wazi sasa nafasi za wakuu wa mikoa na wilaya zinahojiwa juu ya umuhimu wake. Zimebaki kuwa ni alama ya uwakilishi wa rais katika maeneo yao. Unapokuwa na rais mtendaji wa kila siku, akiwa na waziri mkuu pamoja na wizara ya Tamisemi yenye wakurugenzi watendaji kila wilaya, hakuna umuhimu wa wakuu hawa.

Kuwepo kwao ni mzigo kiuchumi kwa taifa na kero kwa watendaji halisi wa shughuli za serikali na serikali za mitaa. Migogoro wilayani na mikoani haitaisha mpaka kazi za hawa wateule zifahamike waziwazi.

Kikubwa ni kwamba katika wakuu hawa wa mikoa walioteuliwa, hakuna mpya hata mmoja; ama walikuwa wakuu wa wilaya, mikoa, au wabunge walioshindwa.

Walihitajika wazamiaji wa kuokoa maisha na chombo kwa kuwa mabaharia wanaoendesha, ama wamechoka sana, wameshindwa kazi au wamekimbia kazi yao ya kuendesha chombo chetu.

Badala yake, walioteuliwa ni sehemu ya mabaharia waliozamisha chombo chetu. Si wazamiaji wa kuokoa maisha ya abiria wala chombo, bali ni wazamishaji zaidi wa chombo chetu.

Yeyote aliyehusika na mchakato wa kuwateua hawa kuwa wakuu wa mikoa alikuwa na kigezo kingine kisicho cha kubadilisha hali ya utendaji katika serikali yetu. Nitaeleza.

Kuteuliwa kuwa mkuu wa mkoa si suala la kupandishwa cheo kutoka cheo cha chini yake kama inavyoonekana katika sehemu kubwa ya walioteuliwa. Ukuu wa mkoa ni nafasi ya uteule wa kutenda kazi za serikali na kwa hiyo kigezo kikuu na kumridhidha mteuzi kuwa mteuliwa anayo rekodi ya kutenda kazi kwa viwango vya ngazi ya mkoa au zaidi.

Kinachoangaliwa hapa ni mkoa si wilaya anakotoka aliyeteuliwa. Hii ni kwa sababu aliyetenda vema katika ngazi ya wilaya amefanya hivyo kwa sababu tu ni wilaya na si mkoa. Ni makosa kudhani kuwa aliyefanya vema katika wilaya atafanya vema katika mkoa.

Dhana ya ukuu wa mkoa kuwa ni promosheni ya wakuu ya wilaya ni mpya katika historia ya utawala hapa nchini. Wakati wa Mwalimu Julius Nyerere, hata mawaziri wangeweza kuteuliwa kuwa wakuu wa mikoa, mawaziri wakuu wangeteuliwa kuwa mawaziri wa kawaida na hata mawaziri wangeteuliwa kuwa naibu mawaziri.

Tuliwahi hata kuwa na waziri aliyeteuliwa kuwa mkuu wa wilaya. Kwa Mwalimu cheo ilikuwa dhamana si fadhila, na zaidi ya utendaji, Mwalimu aliangalia uumini wa mteuliwa katika masuala ya msingi kama uzalendo, utaifa na uwezo wa kuwafundisha Watanzania.

Utamaduni huu mpya wa kuteua kwa misingi ya kupandishana vyeo, ni mzigo kwa taifa na unaongeza vinyongo visivyo na sababu miongoni mwa watawala.

Inavyoonekana kwa sasa ni kuwa, utendaji wa wakuu wa wilaya na mikoa hauna utaratibu wa tathmini inayoeleweka. Tathmini kama ipo, imejengwa katika vigezo vya kisiasa zaidi ambavyo havipimiki kirahisi (appraisal).

Utendaji wao umegeuka kuwa suala la kujiuza kwa vyombo vya habari ili waonekane wanafanya kazi sana, au wajipendekeze kwa wana usalama ili waandikwe vizuri; na wakati mwingine wahamasishe zawadi kubwa na nono ili wakubwa wanapotembelea maeneo yao waonekane wakarimu.

Ikiwa hivi ndivyo vigezo vya kupandishwa vyeo kuwa wakuu wa mikoa, hali ya utendaji katika serikali haitabadilika hata kama rais atafanya mabadiliko kila mwezi. Tufike mahali tukubali kuwa kuna watu ambao uwezo wao wa kutenda unaishia ngazi ya wilaya na hata kama wakifanya vizuri haina maana kuwa watafanya vizuri ngazi inayofuata.

Kama huu ndio uteuzi wa wakuu wa mikoa, tutegemee viroja zaidi kwa uteuzi wa wakuu wa wilaya. Kutokana na migawanyiko iliyosheheni ndani ya chama tawala, tayari kuna dalili kuwa kila mkubwa katika serikali ana msululu mrefu wa watu anaopigania wateuliwe.

Hali kadhalika, maafisa usalama walio karibu na ikulu, hao nao wana misururu mirefu ya watu wanaopambana wapitishwe kuwa wakuu wa wilaya. Misusuru hiyo mirefu nyuma ya watawala na wana usalama, haina kigezo kingine zaidi ya uswahiba, mapenzi, rushwa, makundi ya urais na itikadi za chama tawala.

Vigezo hivi vikiachwa viongoze uteuzi wa wakuu wa wilaya na mikoa, hakuna uwezekano wa kuinua hali ya utendaji katika serikali hii kwani kila Mkuu wa Wilaya atakuwa anafanya kazi kumpendezesha aliyewezesha kuteuliwa kwake.

Na kwa kuwa uteuzi wa wakuu wa mikoa na wilaya haufanywi na ofisi ya rais tu, kuna hatari kuwa rais anabebeshwa mizigo, ama bila kujua au kwa kujua lakini akawa dhaifu wa kujitetea. Kwa kuwa vita vya urais wa mwaka 2015 vimepamba moto, ni wazi ajenda hiyo ndiyo inayotawala vigezo vya uteuzi wa wakuu hao kwa sasa.

Matokeo ya udhaifu huu wa kimtizamo ndiyo yanayopelekea wakuu wa mikoa na wilaya kutumia muda mwingi kupiga siasa za vyama badala ya kufanya kazi za maendeleo.

Kimsingi, kwa kuwa wakuu wa wilaya na mikoa wanategemewa kuwa makada wa chama tawala, basi rais na waziri mkuu wangefanya utaratibu wa chama tawala kutoa mawazo yake katika uteuzi wa watu hawa na ikibidi, uteuzi huu uthibitishwe na kamati kuu ya chama tawala.

Hii inaweza kuondoa migawanyiko iliyomo na inayoweza kuendelezwa na uteuzi usiochujwa. Kutokufanya hivi ni kuwafanya wateule washiriki kikamilifu kuzamisha badala ya kuokoa chombo na abiria.

Hivi sasa kuna uvumi kuwa orodha ndefu ya watu walioahidiwa na rais kuwa watateuliwa, hawakutokea kwenye orodha. Uvumi unaeleza kuwa waliondolewa na watu wengine “wasio wa rais.” Tusubiri. Yatajitokeza.

tutikondo@yahoo.com
0
No votes yet