Walimu, Kikwete: Nani msaliti?


Yusuf Aboud's picture

Na Yusuf Aboud - Imechapwa 20 October 2010

Printer-friendly version
Uchambuzi

BAADA ya kupata mwaliko kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya Siku ya Walimu Duniani, Rais Jakaya Kikwete alifikiri kuwa amepata fursa adhimu, ambayo angetumia kurejesha uhusiano mzuri na wafanyakazi.

Alifunga safari hadi Songea, Mkoani Ruvuma yalikofanyika maadhimisho hayo, 5 Oktoba 2010.

Aliwakuta walimu watulivu lakini wasio na uchangamfu; alipowasabahi walimwitikia na walimpa ujumbe kupitia mabango ambao ni muhtasari wa matatizo waliyowahi kumbwagia katika maadhimisho kama hayo miaka minne iliyopita.

Angalia ujumbe kwa njia ya mabango: Hili linasema, “Hatuna makazi;” lile linaibua, “Tunaishi kwenye bora makazi si makazi bora.” Jingine linauliza, “Mbona hatupandishwi madaraja?” Lipo hata linalohoji, “Malipo yetu ya likizo vipi?”

Tofauti na mwaka huu, mwaka 2006, walimu wakiwa na hamasa waliadhimisha Siku ya Walimu Duniani mjini Mtwara kwa matumaini makubwa. Mgeni rasmi alikuwa Rais Kikwete.

Ni katika maadhimisho hayo, yaliyofanyika 11 Oktoba badala ya Oktoba 5, walimu walimweleza ukweli wa hali ngumu ya maisha.

Ni siku hiyo, Kikwete aliwapa matumaini ya kinadharia na ahadi kuhusu uboreshaji wa maslahi yao hasa mishahara yao.

Aliwasimulia hadithi tamu kwamba “…katika mwaka huu wa fedha 2006/07 serikali imeongeza mishahara yenu, kama ilivyokuwa kwa kada nyingine za utumishi wa umma.”

Aliahidi kuiboresha mishahara yao, pamoja na watumishi wengine wa umma kadri uchumi unavyokua. 

Aliwaambia tayari kuanzia 18 Mei 2006, serikali ilishaunda Tume ya Kuboresha Mishahara ya Watumishi wa Umma, wakiwamo walimu na kwamba tume hiyo tayari imeanza kazi tangu 1 Julai 2006.

Kwamba kazi kubwa ya tume ilikuwa kufanya uchunguzi kuhusu hali ya mishahara ya watumishi wa umma na kutoa mapendekezo ya namna ya kuiboresha zaidi.

Lakini aliwaacha hoi aliposema kwa upande wa walimu, tume ilikuwa inapitia maeneo kadhaa kujua:

  • Misingi gani itumike kupanga mishahara ya walimu;
  • Serikali ifanye nini kuboresha mishahara ya walimu;
  • Mwalimu wa shule ya msingi, sekondari na chuo ana majukumu gani anayoyafanya kuanzia asubuhi hadi jioni;
  • Kazi ya mwalimu inaweza kulinganishwa na ipi nyingine katika Utumishi wa Umma na kwa nini;
  • Mambo gani mengine yazingatiwe katika kuboresha mshahara wa mwalimu.

Tafsiri yake ni kwamba hadi mwaka 2006, Kikwete alikuwa haijui kazi, majukumu, wajibu, hadhi na stahiki za walimu.

Ndiyo maana serikali ilikuwa haijui imetumia vigezo gani katika kupanga mishahara yao.

Alikuwa hajui namna ya kushughulikia kero na malalamiko ya mishahara na posho zao. Wala hakuwa anajua mwalimu anafanya nini tangu asubuhi.

Je, nini kilifuata baada ya walimu kugundua kuwa “wameingizwa mjini,” tena na kiongozi wa nchi?

Mgomo wa 2008:

Mwaka 2008 kupitia chama chao – Chama cha Walimu Tanzania (CWT), walimu walikaa na kubaini kuwa ahadi za Kikwete zilikuwa “longolongo.” Kwa kauli moja, wakaanzisha mapambano.

Katika mapambano hayo, CWT iliamua kutumia lugha ambayo inaaminika kuwa serikali inaisikia haraka – mgomo – ili kushinikiza kulipwa stahiki zao.

Miongoni mwa madai ya walimu ni malimbikizo ya posho, nyongeza za mishahara, matibabu, fedha za kujikimu, nauli, fedha za uhamisho na upandishwaji madaraja.

Siku moja kabla ya kufanyika mgomo, serikali ambayo inadaiwa ni sikivu chini ya Rais Kikwete, ilikimbilia mahakamani, mgomo ukuzuiwa usiku.

Hata hivyo, tayari ulikuwa umefanikiwa kwa asilimia 80.

Baada ya serikali kufanikiwa kuhujumu mgomo, ilianza kuhaha kulipa baadhi ya madai na iliharakisha zaidi pale ilipoona kuwa CWT inaandaa mgomo mwingine. Mpaka sasa, bado walimu wanalilia maisha bora.

Atibua wafanyakazi

Kutokana na mlolongo wa kutoridhishwa na utekelezaji wa ahadi za serikali, Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) lilikataa kumwalika katika Siku ya Wafanyakazi Duniani na lilipanga kugoma nchi nzima kuanzia 5 Mei 2010.

Mgomo haukufanyika. Kikwete alitishia kuwapiga ngeu watakaoandamana.

Lakini katika mazingira ya kutatanisha CWT ilikaa kimya ikamwalika Kikwete akawa mgeni rasmi katika Siku ya Walimu Duniani, mapema mwezi huu.

Je, si walimu kupitia CWT waliungana na wafanyakazi wote, chini ya mwavuli wa TUCTA, kumkataa Kikwete kuwa mgeni rasmi Mei Mosi?

Kwa nini CWT chini ya TUCTA imkatae Kikwete, lakini yenyewe ione anastahili kuwa mgeni rasmi? Jibu ni moja tu: Kuna juhudi za kuwagawanya, kuwapondaponda ili watawalike kwa urahisi.

Kampeni

Idara zote za serikali zinahaha kuhakikisha Kikwete haadhiriki katika uchaguzi mkuu wa mwishoni mwa mwezu huu.

Maofisa elimu wanawaandikia barua walimu waende na wanafunzi wao kwenye mikutano ya kampeni ya mgombea urais wa CCM.

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) nayo inadaiwa kujitosa katika kampeni kwa ajili ya Rais. Kuna madai kuwa tarehe 15 mwezi huu, maofisa wa TAKUKURU walifanya kampeni katika chuo cha VETA, Arusha.

Katika baadhi ya idara nyeti, watumishi wanadaiwa kuruhusiwa saa 6.00 mchana, kwenda nyumbani kuvua nguo za kazi ili waweze kuhudhuria mikutano ya kampeni.

Kwa kawaida hutoka kazini saa 8.30.

Zote hizi ni juhudi za dakika za lala salama. Mgombea urais wa CCM anahaha kufanya maridhiano na wote aliowakosea.

Ndiyo maana, baada ya kugundua ‘alipotea’ kuwatumia wazee wa CCM Dar es Salaam, kama jukwaa la kushambulia wafanyakazi, hapo Mei mwaka huu, walimu wamejitosa kumpa uwanja ili ‘atubu’ kiutu uzima.

Nani kawapumbaza walimu hawa? Wanajua matatizo waliyomweleza mwaka 2006 ndiyo waliyomkabidhi hivi karibuni. Na yeye majibu aliyowapa mwaka 2006 ndiyo aliwapa tena safari hii.

Je, katika mchezo huu wa “nikune nikukune,” walimu hawaoni kwamba ndio wanachezewa akili na wanajiangamiza wao na taifa zima?

Walimu wanajua pia kwamba ahadi ya serikali mwaka 2006, 2007 na 2008 ya kujenga nyumba nchi nzima haijatekelezwa; na walimu 181,440 hawana nyumba. Hali ni mbaya zaidi vijijini.

Walimu waliopandishwa madaraja wanalipwa mishahara ya zamani, hawajalipwa fedha za malimbikizo ya posho za uhamisho, kufundishia na matibabu; wameomba serikali iwaharakishie.

Kikwete (akasimama akajiuliza, awambie nini), akasema amesikia matatizo yanayowakabili na atayafanyia kazi yote, ikiwa ni pamoja na na kuboresha zaidi maslahi yao na kuwataka wafanye kazi kwa bidii ili kuinua kiwango cha elimu nchini.

Kauli hiyo si alitoa mwaka 2006?

Kama ameshindwa kulipa madai halali ya walimu kwa miaka mitano sasa, atapata wapi pesa za kutimiza ahadi alizomwaga nchi nzima?

Kama Kikwete ameshindwa kutekeleza yaliyomo katika ripoti ya Tume aliyounda mwenyewe 2006, atatekeleza yaliyo katika ripoti aliyounda nani?

Kilio: Katika kipindi cha 2005 – 2010 chini ya Rais Kikwete; walimu, wafanyakazi wanalia; wazee wa Afrika Mashariki na wanafunzi vyuo vikuu, wanalia.

Kicheko: Walioishi roho kwatu kwa miaka mitano iliyopita ni wanasiasa, wazee wa CCM, mafisadi na walarushwa.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: