Walimu shule za msingi Kibondo ni mzigo


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 20 July 2011

Printer-friendly version
Tuseme Ukweli

USEMI kwamba mwalimu ni kioo, kiongozi na mlezi wa jamii bora ya kesho hauna mashiko katika wilaya ya Kibondo. Walimu wamekuwa kero kutokana na utoro kiasi kwamba wengine wamefunguliwa mashitaka katika Tume ya Utumishi wa Walimu (TSD) ili wafukuzwe.

Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa makala haya katika shule zaidi ya 16 kati ya Julai 11 na 15 mwaka huu katika wilaya hiyo, unaonyesha kuwa kuporomoka kwa nidhamu ya walimu, kumeporomosha utendaji kazi na kusababisha wanafunzi wengi kufeli na wao kuwa watoro pia.

Mathalani, mwaka 2008 wanafunzi 8654 walijiandikisha kufanya mtihani wa kuhitimu shule ya msingi wilaya ya Kibondo kutoka katika shule 140.

Ilipofika Septemba, walioingia kwenye chumba cha mtihani walikuwa 8362 yaani watoto 292 pungufu ya waliojiandikisha na wanafunzi 3226 tu walifaulu kuingia sekondari. Waliofaulu walikuwa asilimia 39 ya watoto waliofanya mtihani.

Idadi ya wanafunzi walioandikishwa kufanya mtihani ilipungua mwaka 2009 na kufikia 7776; waliofanya mtihani walikuwa 7619 yaani 159 walitoweka na vijana 2538 walifaulu sawa na asilimi 34.

Mwaka 2010 walijiandikisha wanafunzi 7863 lakini waliofanya mtihani walikuwa 7685 yaani 178 pungufu na waliofaulu walikuwa 2485 sawa na asilimia 33.

Matokeo haya yamemkera zaidi Afisa Elimu wa Shule za Msingi Wilaya ya Kibondo, Bilunghama Nyalinga. Tayari ameweka mikakati ya kukabiliana na tatizo hilo.

Nyalinga anasema; “Matokeo haya yanasikitisha sana, hayaridhishi hata kidogo. Ukiangalia tunashuka kila mwaka. Yapo mambo mengi yaliyochangia lakini kubwa ni utoro wa walimu kwenye vituo vya kazi na wanafunzi.”

Kwa mujibu wa Nyalinga, walimu wengi ni wa UPE, wapo zaidi ya 700 kati ya walimu 1340 waliyopo, japo wamejiendeleza. “Ni wazee, wamekaa kienyeji mno, hawana mawazo mapya wala mbinu mpya za kufundishia. Mwonekano wao hauna ushawishi kwa wanafunzi,” anasema.

Walimu wengi wamejiingiza kwenye mikopo ya riba kubwa kutoka kampuni zinazokopesha kama Bayport hivyo hawakai vituoni, huwakimbia wadai. “Mfano mwalimu mmoja (jina limehifadhiwa) alikopa Sh. 50,000 lakini sasa anadaiwa Sh. 3,500,000,” anaeleza.

Mwalimu huyo ni miongoni mwa walimu waliojiingiza kwenye matatizo kwani mishahara yao huishia kulipa madeni.

Uchunguzi unaonyesha kwamba kutokana na kukaa kienyeji, baadhi yao wakifika mjini hukaribishwa na kina dada na kukirimiwa ngono. Robo tatu ya walimu wa kiume wa vijijini wamejikuta wakiwa na mahawara au nyumba ndogo zinazowasumbua washindwe kukaa kwenye vituo vya kazi.

“Tumewafungulia mashitaka walimu 26 tangu mwaka 2006 lakini wenzetu TSD ambao ndio mamlaka ya nidhamu hawajatoa uamuzi. Walimu hawa hukosekana shuleni hadi miezi minne,” anafafanua.

Kadhalika walimu wakuu wamekuwa wakitoka kwenye vituo vya kazi kwa madai ya kufuatilia fedha za ruzuku (Capitation Grant) na kufanya ununuzi wa vifaa.

“Tumewazuia wasishiriki mchakato wa kununua bali washiriki vikao vya kupanga, walimu wa fedha ndio waende kufanya manunuzi wao wabaki kushughulikia usimamizi,” anaeleza.

Utoro mwingine unaoathiri maendeleo ya elimu katika wilaya hiyo ni wa wanafunzi.

Kwanza katika baadhi ya shule unachangiwa na utoro na uhaba wa walimu. Wanafunzi wakikaa muda mrefu bila walimu huamua kuondoka.

Pili unatokana na tabia ya wazazi kutojali umuhimu wa elimu; hawafuatilii watoto wao kama wamefika shuleni wala kujua kama wamejifunza au hapana. Wazazi wa aina hii hufurahia kuwatuma watoto wao sokoni kwa shughuli za kusaidia familia.

Wanaoishi karibu na barabara huishia kwenye vibanda vya sinema na wanaoishi karibu na mito hufurahia kuvua samaki na kuwinda.

Uchunguzi unaonyesha kuwa wafugaji wanaoishi katika kijiji cha Ilunde kilichopo pori tengefu la Muyowosi wanachangia wanafunzi kuacha shule. Huwachukua vijana kwa ahadi ya kuwapa ng’ombe mmoja baada ya mwaka. Wazazi hupewa Sh. 50,000 wawaachishe shule watoto wao ili waende kufanya kazi ya kuchunga ng’ombe.

Wanafunzi 300 wa darasa la III hadi la VII kutoka shule za msingi za kata za Busunzu, Busagara, Lugongwe na Itaba wamelowea huko tangu mwaka 2000.

Mbali ya wafugaji, wakulima wakubwa wa tumbaku wilayani Urambo, Tabora nao hutorosha wanafunzi ili wakafanye kazi za vibarua. Shule za kata za Kitahana, Busagara, Kasanda, Mugunzu na Gwanumpu ndizo zimeathirika zaidi. Wazazi hupewa Sh. 50,000 tu ili wawaruhusu watoto wao.

Wanaume wanaoishi kata za mpakani na Burundi wamegundulika kuwa na wake Tanzania na Burundi. Wazazi hao huandikisha watoto shule, lakini ukifika wakati wa michango, hutorokea Burundi pamoja na watoto. Wengi hawafanyi hata mitihani.

Kata za Mabamba, Mugunzu, Gwanumpu pamoja na Bukiriro zimeathirika zaidi na shule za Gwanumpu, Ntoyoyo, Mukarazi, Kiga, Kumkuyu huwa hazifaulishi kabisa. Wanafunzi huchora tu karatasi za mitihani na wengine huambiwa na wazazi wao wakifanya mtihani na wakafaulu watajigharimia wenyewe sekondari.

Mikakati Kwanza, serikali ya wilaya ya Kibondo, kwa msaada wa UNICEF inaendesha semina iliyopewa jina la Tuseme ili wananchi waelezane umuhimu wa elimu kwa watoto wao na wanafunzi kwa wanafunzi.

Pili wameanzisha shule sita za mfano zenye mazingira ya kumjali mtoto ambako wazazi huzungumza matatizo yanayowakabili na kupeana mbinu namna ya kutatua. Mradi huo uko katika shule za msingi za Nyaruyoba A na B, Kifura, Kasuga, Nyakayenzi na Katahokwa.

Wenyeviti wa vijiji, watendaji wa vijiji na kata pamoja na madiwani wameombwa kushiriki kazi ya uhamasishaji wazazi wajue urithi pekee wenye manufaa kwa watoto wao ni elimu.

Serikali za vijiji zimetakiwa kutumia askari wa mgambo kuzuia na kukamata watu wanaopita kwenye vijiji vyao wakiwa na nia ya kuwalaghai wazazi wawaachie watoto wao waende ama kuchunga ng’ombe au kwenye kilimo cha tumbaku.

Hata hivyo, tatizo la utoro si kubwa sana kwa shule za sekondari. “Utoro ni kidogo kwa shule za sekondari na naweza kusema hakuna kabisa kwa wanafunzi wa kidato cha V na VI kwa sababu wanaelewa walichofuata,” anasema Afisa Elimu Sekondari Wilaya ya Kibondo, Alex Rwabigene.

“Kuna upungufu wa walimu lakini waliopo wanajitahidi kadri ya uwezo wao. Tatizo jingine tunalopata ni wazazi kutoona kuwa elimu ni muhimu. Wanafunzi wengi wanapofeli, wengine wanakosa ari na wazazi hawaoni tofauti ya kusomesha na kutosomesha,” anafafanua.

0789 383 979, jmwangul@yahoo.com
0
No votes yet