Walimu wabomoa chungu cha ujinga


Ndimara Tegambwage's picture

Na Ndimara Tegambwage - Imechapwa 30 May 2012

Printer-friendly version
Uchambuzi

SASA unaweza kusoma Sayansi kwa Kiswahili. Kikwazo cha lugha ya kigeni kimeanza kuondolewa. Chungu cha ujinga kimebomoka.

Walimu na wadau wengine, wamefanikisha uchapishaji wa kitabu cha somo la Kemia kwa Kidato cha I.

Kitabu kinaitwa: Furahia Kemia/Enjoy Chemistry – Kwa wanaoanza kujifunza/A textbook for beginners. Kimechapwa mwaka 2011.

Fungua kitabu. Kushoto ni Kiswahili, kulia ni Kiingereza. Kimesheheni maarifa, maelekezo na michoro ya vifaa vya kufanyia mazoezi. Ni sayansi.

Waandishi wanaelekeza: “Soma sentensi, kifungu cha maneno au mada nzima kwa Kiingereza. Pale tu unapoona kwamba huelewi kila kitu ndiyo usome sentensi, kifungu cha maneno au mada hiyo kwa Kiswahili.”

Hapa waandishi wamejikita katika maana na uelewa. Kama hukuelewa, au hukuelewa vizuri kile ulichosoma, basi unageukia lugha nyingine.

Inaelekezwa mwanafunzi asome kwanza Kiingereza. Akielewa, basi aendelee. Asipoelewa, apate msaada wa Kiswahili. Kwa msingi huo, kitabu kinafundisha Kiingereza kwa msaada wa Kiswahili.

Furahia Kemia hakiondoi umuhimu wa kuwa na vitabu vya kiada vya sayansi vilivyoandikwa kwa Kiswahili moja kwa moja – lugha ya mwalimu na mwanafunzi nchini – bali ni moja ya njia za kufikia huko.

Angalia mbele – miaka minne ya kuchapisha vitabu vingine kwa ajili ya vidato vingine na kwa masomo mengine ya sayansi. Kutakuwa na tofauti.

Iko wapi basi, sababu ya kutokuwa na msimamo katika matumizi ya lugha ambayo wote – walimu na wanafunzi – watakuwa wanaelewa vizuri; huku wakijifunza lugha nyingine zozote watakazo?

Ibrahim Kipepe wa MwanaHALISI amehoji wanafunzi jijini Dar es Salaam juu ya kitabu hiki. Rosemary Kelvin wa sekondari ya Zanaki anasema, “Kitatusaidia sana sisi ambao hatukutokea shule za Kiingereza.”

Janeth Julius (Zanaki) anasema, “Wanafunzi watapata msamiati muhimu unaotokea kwenye mitihani.”

Ramadhani Mohamed wa sekondari ya Makoza, Tabata anasema, “Tunaosoma shule za Kata, tutanufaika zaidi kutokana na mafundisho ya sasa kutokidhi uelewa wa masomo.”

Eric Bayona wa sekondari ya Migombani, Segerea, “Kitabu kinaweza kuchanganya wanafunzi ambao wataegemea kwenye Kiswahili na hatimaye mitihani ikaja kwa Kiingereza.”

Bakari Salum wa sekondari ya Tambaza anasema, kitabu hiki kilicho madukani sasa, “Kitaleta ongezeko la wanaofaulu kwa vile wengi watakuwa na uelewa mpana.”

Hussein Juma wa sekondari ya Ananasif anasema, “Unajua tumefundishwa kwa Kiswahili hadi darasa la saba. Hatujui kusoma wala kuandika Kiingereza. Hiki kitakuwa mkombozi.”

Naye Justina Kakuru aliyemaliza Kidato cha IV miaka mitatu iliyopita anasema, “Ningepata msingi kama huu, ningesoma sayansi.”

Furahia Kemia kimechapishwa na kampuni ya Mkuki na Nyota Publishers ya Dar es Salaam kwa udhamini wa HakiElimu – asasi ya kijamii nchini inayopigania uwazi, haki ya kupata elimu bora na demokrasi; na asasi nyingine ya Faire Welt Rastatt e. V.

Hata katika mazingira ya uchumi huria, kitabu hiki ni mkuki kwa mikonga ya kibeberu ya uchapishaji, ambamo kwa miaka mingi, watawala wamenaswa na kukataa kuamua juu la lugha ipi itumike kuvuna elimu na maarifa.

0713 614872
0
No votes yet