Walimu wakuu wajichongea Mbinga


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 30 November 2011

Printer-friendly version
Tuseme Ukweli

WALIMU wakuu wanatarajiwa kuwa mfano wa kuigwa kwa walimu wengine katika mambo mengi kama vile kuandaa maazimio, maandalio ya masomo, kufundisha na kusimamia uwajibikaji.

Hali ni tofauti katika shule za Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga mkoa wa Ruvuma. Tathmini iliyofanywa na Idara ya Elimu na kila shule kukabidhiwa ripoti kwa ajili ya kujitathmini inaonesha baadhi ya shule ni dhaifu na walimu wakuu ni ‘bomu’.

“Tathmini nyingine iliyofanywa ni kuhusu uwezo wa walimu kufundisha. Matokeo ya tathmini hii ni kwamba baadhi ya walimu wakiwemo walimu wakuu wa shule za msingi hawafundishi ipasavyo; baadhi yao hawaandai maazimio ya kazi, na wengine hawaandai na kuwapa mazoezi wanafunzi,” anaeleza David Mathias Mkali, Afisa Elimu wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, katika mahojiano na mwandishi wa makala haya ofisini kwake hivi karibuni.

Mkali ambaye alihamishiwa Mbinga Machi mwaka huu akitokea Tunduru, alifanya mambo mawili makubwa. Kwanza alikutana na waratibu wa elimu kata, walimu wakuu na wadau mbalimbali wa elimu.

Pili aliwapima wanafunzi kwa lengo la kubaini wasiojua kusoma na kuandika na uwajibikaji wa walimu na walimu wakuu wa shule 321 katika urithishaji maarifa kwa wanafunzi.

Idara ya Elimu sasa inatumia matokeo ya tathmini hiyo  kuhamasiaha uwajibikaji, kufanya mageuzi makubwa ya ufundishaji darasani kwa kuwapa wanafunzi wasiojua kusoma na kuandika masomo ya ziada.

“Hali ya sasa ya mashuleni ni mbaya hasa kwa sampuli ya shule zilizofanyiwa ukaguzi kwani hali ya ufundishaji ni chini ya asilimia 50 na zipo shule zenye asilimia 0. Hata baadhi ya walimu wakuu utendaji kazi wao ni mbovu. Katika mikakati ya kuinua elimu walimu wakuu zaidi ya 50 watashushwa vyeo,” anafafanua Mkali akisema wameshindwa kutekeleza majukumu yao.

Matokeo ya tathmini katika shule 54 yanaonesha Shule ya Msingi ya Huruma imepata wastani wa asilimia 70 katika maandalio, 96 katika mazoezi na 83 katika utendaji kazi ikifuatiwa na Kipika yenye 84 (maandalio), 70 (mazoezi) na 77 (utendaji kazi) wakati Mabuni imeshika mkia ikiwa na 2 (maandalio), 8 (mazoezi) na 5 (utendaji kazi). Shule 16 zimepata alama juu ya 50 huku 38 zikipata wastani chini ya 50.

Aidha, walimu 213 wakiwemo walimu wakuu kati 364 waliofanyiwa tathmini wamepata wastani chini ya asilimia 50.

Mwalimu aliyeshika nafasi ya kwanza alipata wastani wa asilimia 144 katika maandalio ya masomo, asilimia 113 katika mazoezi na asilimia 129 utendaji kazi na anatoka Shule ya Msingi ya Kipika. Aliyeshika nafasi ya mwisho alipata asilimia 0 katika maandalio, asilimia 23 katika mazoezi na asilimia 0 katika utendaji kazi na anatoka Shule ya Msingi ya Mabuni.

Baadhi ya walimu na walimu wakuu imeelezwa kwamba ni walevi, watoro, wazembe na kwamba uwepo wa walimu wengi wasiofuata taratibu au wasio na uwezo katika ufundishaji, umechangia matokeo yasiyoridhisha kwa wanafunzi wanaohitimu elimu ya msingi wilayani humo, mwaka hadi mwaka.

Mathalani, mwaka 2008 wanafunzi 14,415 walifanya mtihani wa kuhitimu eimu ya msingi na kati yao, 6,979 tu sawa na asilimia 48 ndio walifaulu.

Idadi ya wanafunzi waliofanya mtihani wa darasa la VII mwaka 2009 walipungua hadi 12,934 yaani pungufu kwa wanafunzi 1,481 na matokeo yao, wanafunzi 6,567 sawa na asilimia 50 walifaulu.

Mwaka 2010, kwa sababu ya vifo na utoro, wanafunzi walipungua zaidi hadi kufikia 11,431 waliofanya mtihani, ambapo wanafunzi 4,689 sawa na asilimia 41 ndio walifaulu.

“Vilevile takwimu zilizokusanywa hadi kufikia terehe 19 Mei 2011 zinaonesha kwamba, ukiacha wanafunzi wa darasa la I na la II, wilaya nzima ya Mbinga madarasa kuanzia la III hadi la VII wanafunzi 15,128 kati ya wanafunzi 116,966 hawajui kusoma na kuandika,” alisema Mkali.

“Kati ya wanafunzi hao waliopungukiwa KKK yaani wasiojua kusoma, kuandika na kuhesabu wanafunzi wa darasa la VII waliofanya mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi walikuwa 1,744,” alifafanua Mkali.

Sababu zilizozoeleka za matokeo mabaya kila mwaka kwa wanafunzi wa shule za msingi na hata sekondari nchini, hutajwa na wadau wa elimu kuwa ni ukosefu wa miundombinu ya madarasa, uhaba wa vitabu vya kufundishia na kujifunzia, upungufu wa walimu, ukosefu wa huduma ya maji na umeme, umbali mrefu kufika shuleni, umaskini na mwamko mdogo ya wazazi.

Pamoja na sababu hizo, katika mkutano wa tarehe 23 Septemba 2011 ambao uliwahusisha walimu wakuu wa shule za msingi, mbele ya mkurugenzi wa halmashauri ya Mbinga, walimu wakuu walijishitaki wenyewe.

Kuhusu suala la walimu kutoandaa maazimio, mandalio ya masomo, kutotoa mazoezi kwa wanafunzi na kutofundisha kikamilifu, walimu wakuu walidai kuwa hiyo inatokana na walimu kutohimizwa, walimu wakuu kutokagua mandalio ya kazi, walimu wakuu wenyewe kutoandaa na kufundisha ipasavyo, kamati za shule na uongozi wa kata kutofuatilia maendeleo ya elimu.

Kuhusu utoro, ulevi na uzembe kwa baadhi ya walimu, walimu wakuu hao walidai inatokana na walimu wakuu kutobainisha na kuchukua hatua, walimu wakuu pia kuwa watoro, wazembe na walevi wa kutupwa na pia hutoa ruhusa kiholela tena bila kufuatilia.

Vilevile suala la kutofundisha siku zote 194/195 zilizowekwa na wizara, walimu wakuu hao walijishtaki wakisema ni kutokana na wao kutosimamia kikamilifu na kutofanya ufuatiliaji wa karibu.

Matatizo mengine ambayo walimu wakuu wanadaiwa kuwa nayo ni kuwafanyisha kazi za vibarua wanafunzi kama vile kusomba matofali, kuchuma kahawa katika mashamba ya watu badala ya kusoma.

Hadi sasa wilaya ina jumla ya shule 321 zenye jumla ya wanafunzi 116,966 kuanzia madarasa ya awali hadi la VII.

Vilevile ina walimu 2,021 hivyo kufanya uwiano wa mwalimu na wanafunzi kuwa 1:58 badala ya ule wa 1:40 wa kitaifa. Mahitaji halisi ni walimu 2921 hivyo Mbinga ina upungufu wa walimu 903.

Upungufu wa walimu umechangiwa na sababu nyingi. Mosi wilaya inapangiwa walimu wapya wachache kuliko mahitaji; pili ni uwepo wa walimu wengi wanaostaafu na kufariki dunia.

Mathalani mwaka 2008 waliajiriwa walimu wapya 15 wakati 22 walistaafu na 18 walifariki dunia; mwaka 2009 waliajiriwa 19 ilhali walistaafu 24 na waliofariki dunia walikuwa 15; mwaka 2010 waliajiriwa 22, waliostaafu 23 na  waliofariki 20 na hadi Juni mwaka huu walistaafu walimu 39 na watano wamefariki.

Tatizo jingine lililochangia upungufu wa walimu katika shule za msingi ni walimu wenye stashahada na shahada kuhamishiwa kufundisha katika shule za sekondari.

0789 383 979, jmwangul@yahoo.com
0
No votes yet