Waliogundua dhahabu wamebaki mafukara


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 30 March 2011

Printer-friendly version
Gumzo la Wiki

WAMILIKI wa ardhi tajiri yenye dhahabu wameng’olewa kama gugu. Wakafagiwa kama takataka na kuwekwa kando. Baadhi wanaripotiwa kufukiwa machimboni wakiwa hai.

Hiyo ndiyo historia ya Wananchi na Dhahabu katika kijiji cha Kakola, wilayani Kahama, mkoa wa Shinyanga.

Nenda Kakola. Wasikilize wananchi: Kijiji ambacho hakikuwa na mpangilio mzuri kama kilivyo leo, lakini kikaendelea kukua hasa baada ya kugunduliwa dhahabu, kilifutwa ghafla na eneo lote kukabidhiwa kwa mwekezaji.

Kampuni ya Kahama Mining Corporation Limited (KMCL), ndiyo ilikabidhiwa eneo lote la kijiji ambako dhahabu iliota mithili ya uyoga.

Uamuzi wa serikali wa mwaka 1996 ulisababisha msuguano kati yake na wananchi ambao kijiji chao kilikuwa kinatambuliwa rasmi kiserikali tangu mwaka 1974.

Kilichofuata ni magreda ya KMCL kuranda eneo lote yakibomoa nyumba na mabanda na kufukia machimbo ya watu binafsi tayari kwa uchimbaji wa kisasa.

Taarifa za wananchi kijijini Kakola zinasema wachimbaji wadogo wapatao 52 walifukiwa wakiwa hai ndani ya machimbo yao.

Ilikuwa hivi: Katikati ya miaka ya 1970 zilipatikana habari njema za utajiri wa haraka kuliko mifugo na kilimo katika eneo lililokuwa na miti mingi la Kakola, wilayani Kahama.

Wafugaji wenyeji waliona “vitu vinavyong’aa” kwenye mashina ya miti iliyoanguka, lakini hawakujua kama vilikuwa na thamani. Wakawa wanavichezea.

Henry Kisambale (67), kupitia kwa mkalimani wangu, Enos Mabelele (41), anasimulia mwanzo wa uvamizi wa Bulyanhulu.

Anasema baadhi ya wananchi walipochukua “vitu vinavyong’aa” na kuwaonyesha wageni, ndipo eneo hilo lililokuja kuitwa Bulyanhulu lilipovamiwa na watu kutoka sehemu mbalimbali na kuanza kuchimba kile kilichokuja kuitwa “dhahabu.”

“Naifahamu vizuri sana historia ya eneo hili,” anasimulia Kisambale aliyeishi Kakola kwa zaidi ya miaka 57 sasa.

“Tulikuwa tunachunga ng’ombe katika msitu uliokuwa na miti mikubwa ya kivuli iitwayo nkola. Siku moja wakati tunachunga, tulikuta mti wa nkola umeanguka huku vikionekana vitu vinavyong’aa kwenye shina na mizizi,” anaeleza.

Kisambale anasema eneo hilo walikuwepo ndege wengi ambao muda mwingi walikuwa wanalia ‘bruubruubruu.’ Mlio huo wa ndege ndio ulizaa jina la Bulyang’hulu,  yaani kule wanakolia ndege.

Baada ya vitu vile vinavyong’aa kujulikana bayana kuwa ni dhahabu, watu waliokuwa wanakwenda kusaka vitu hivyo kwenye miti ya nkola, walikuwa wanasema kwa Kisukuma, wajakujukakola – amekwenda kutafuta.

“Hii ndiyo historia ya majina Kakola na Bulyang’hulu. Barrick wanaandika Bulyanhulu,” anasema mzee Kisambale.

Ugunduzi huo ndio ulivuta watu wengi Kakola. Walikuja kuchimba madini. Wenyeji, akiwamo Kisambale waliacha kuchunga na kulima; wakajigawia maeneo ya kuchimba dhahabu na mwaka 1974  kijiji kikasajiliwa.

Baada ya uchimbaji wa madini kushamiri, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ilianza kununua dhahabu ili kuwapa urahisi wa soko hadi mwaka 1994 serikali iliporuhusu uwekezaji mkubwa katika sekta ya madini.

Pamoja na uwekezaji mkubwa kuruhusiwa, tarehe 19 Februari 1993, Rais Ali Hassan Mwinyi, wakati akifungua kituo cha polisi kata ya Lunguye alisema, pamoja na mambo mengine, kuwa wachimbaji hawatahamishwa.

Historia inatengeneza kalenda rasmi ya kilichowasibu wananchi wa Kakola.

Tarehe 23 Machi 1993, Afisa Mfawidhi wa Madini anaandika barua kutambua miliki ya Emmanuel John, mmoja wa wachimbaji wadogo.

Lakini Septemba 1994, serikali inaipa leseni kampuni ya KMCL. Mbunge wa Msalala, Bhiku M.S Bhiku ananasa mkataba uliotiwa saini, ambamo serikali inamwambia mwekezaji, KMCL kwamba anapewa eneo lisilo na kiumbe chochote (au lisilo na binadamu isipokuwa miti na ndege?).

Juni 16, 1995, baadhi ya wachimbaji wadogo kupitia umoja wao wanakubali kuondoka lakini walipwe fidia ya dola 5.6 milioni.

Wachimbaji wanafungua kesi katika Mahakama Kuu kanda ya Tabora, kupinga kuondolewa kwenye eneo hilo bila kulipwa fidia.

Januari 1996, Waziri wa Nishati na Madini, William Shija anakwenda Kakola kuwataka wananchi wahame kwa madai kuwa ni “wavamizi.”

Julai 30, 1996, waziri Shija analiambia Bunge kwamba wachimbaji wadogo wamepewa mwezi mmoja kuondoka Bulyanhulu.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Jenerali Tumainiel Kiwelu anafika Bulyanhulu akiwa na polisi; anawaambia wachimbaji waondoke katika muda wa saa 24 na kunukuliwa na wananchi akisema, “…zibaki zinasikika sauti za ndege tu.”

Agosti 2, 1996, Jaji Lawrence Mchome aliyekuwa anasikiliza shauri hili anatoa zuio kwa KMCL na polisi kuhamisha wachimbaji. Zuio hilo lilitangazwa na Redio Tanzania.

Agosti 7, 1996 mabuldoza ya KMCL, kwa usimamizi wa polisi, yanaanza kusafisha eneo na kufukia machimbo ambayo baadhi yaliripotiwa kuwa na watu chini.

Mwishoni mwa Agosti 1996, polisi wanaitwa Bulyanhulu kufukua mashimo ili kujiridhisha iwapo kweli kuna watu waliofukiwa. Polisi wanakataa.

Baadaye polisi wanakubali. Kazi inafanyika lakini harufu kali ya uozo, funza na nzi wanapoanza kutoka, polisi wanaamuru kazi ya ufukuaji kusitishwa na wananchi wanaoshuhudia ufukuaji wanafukuzwa.

“Polisi walisitisha kazi ya kufukua; wakafukuza watu kwa viboko. Wakaamuru greda lifukie,” anaeleza Kisambale.

Baada ya hapo polisi wakaandika ripoti inayoonyesha hakukuwa na mauaji na kwamba kampuni ilijiridhisha kwanza juu ya suala la usalama wa watu kabla ya kuanza kufukia.

“Sasa tumebaki tunaishi maisha ya kipumbavu. Serikali imetuletea umaskini huu. Nilikuwa na wafanyakazi 351; wote nikiwalipa mshahara. Leo sina kitu; kama hivi unavyoniona,” anasema.

0
No votes yet