Waliosababisha maafa Zanzibar waadhibiwe


editor's picture

Na editor - Imechapwa 14 September 2011

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

MSIBA mzito umetukuta tena. Watu takribani 200 waliokuwa wakisafiri kutoka Unguja kwenda Wete, Pemba walifariki dunia baada ya meli ya Spice Islander 1 waliyokuwa wakisafiria kupinduka na kuzama.

Taarifa za awali zilizotolewa juu ya sababu za meli hiyo kuzama alfajiri ya Jumamosi iliyopita katika mkondo wa Nungwi zinaonesha haikuwa na hitilafu bali ilizidiwa na uzito wa mizigo na abiria.

Akihutubia wananchi juzi Jumatatu jioni baada ya dua ya kuombea marehemu, Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein alisema watu waliopatikana wazima ni 619 na waliopatikana wamekufa ni 197 huku wengine wakihofiwa kuwa ndani ya chombo kilichozama.

Taarifa ya Dk. Shein inaonesha meli hiyo inayodaiwa inapaswa kubeba abiria 600, ilipakia zaidi ya 800 mbali ya mizigo ambayo haijulikani uzito wake.

Habari hizi za kusikitisha ni kielelezo cha uroho na tamaa ya hali ya juu ya fedha ya wamiliki wa meli, lakini pia uzembe wa nahodha na Mamlaka ya Usafiri wa Majini na Nchi Kavu na viongozi wa Shirika la Bandari na serikali.

Wamiliki wanajua uwezo wa meli hiyo, lakini wakaamua kupakia zaidi ya uwezo wake huku maboya ya wokozi yakiwa 300 tu hivyo waliokosa na ambao hawakuwa na uwezo wa kuogelea ndio waliokutwa na umauti.

Viongozi wa Shirika la Bandari, Mamlaka ya Udhibiti wa Vyombo vya Usafiri Majini na Serikali wakaacha wajibu wao wa kukagua usalama wa chombo kabla hakijaondoka badala yake wakafumbia macho.

Msiba huu umetokana na uzembe wa watu waliopewa kazi ya kukagua na kutoa leseni au kuruhusu chombo kusafiri. Meli hiyo ingekuwa inafanyiwa ukaguzi halali bila kujali wamiliki isingeruhusiwa kusafiri.

Ripoti zilizopo zinaonesha meli hiyo ilitengenezwa nchini Ugiriki mwaka 1967, yaani miaka 44 iliyopita na ilipewa jina la Mariana. Mwaka 1988 iliuzwa na kupewa jina la Apostolos na 2007 iliuzwa kwa kampuni ya nchini Honduras, Marekani Kusini, na kupewa jina la Spice Islander 1.

Tunawapa pole Wazanzibari hasa ndugu na jamaa wa waliofiwa, lakini pia tunashauri waliohusika na uzembe huu  waadhibiwe.

Mungu awajalie majeruhi wapone mapema, pia awalaze pema marehemu. Amina.

0
No votes yet