Walitaja Mungu, sasa waunda tume inayohojiwa


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 21 September 2011

Printer-friendly version
Kalamu ya Jabir

INATIA huzuni. Tunalazimika kuendelea kujadili matokeo baada ya meli ya Spice Islander 1 kuzama katika mkondo mkubwa wa bahari eneo la Nungwi.

Mazingira ya ajali hii ndiyo yanatusukuma kudadisi. Nilianza kueleza shaghalabaghala ya takwimu za serikali. Zimejaa matundu. Nikagusia kuwa ubabaishaji kama huo ndio chimbuko la ajali yenyewe.

Viongozi wanaopewa dhamana hawawajibiki inavyotakiwa. Kutowajibika kwao huko kunaleta matukio mabaya. Hizi ni athari za viongozi kushindwa kuwajibika.

Kweli takwimu zimejaa matundu. Kwa bahati mbaya, matundu hayajazibwa, inatangazwa tume ya Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, ya kuchunguza mazingira na chimbuko la ajali hii.

Lipo swali halijajibiwa. Meli ya Spice Islander 1 ilikuwa na watu wangapi wakati inazama?

Hakuna ajuaye. Manifesto ya ndani ya meli haitoi idadi kamili ya abiria waliokuwa chomboni. Huwezi kuipata idadi kamili kwa Mkaguzi wa meli, Shirika la Bandari na Mamlaka ya Usafiri wa Baharini na Nchi Kavu. Mote humo hakuna orodha ya waliosafiri.

Hata ukiipata orodha ya wasafiri, haitakueleza takwimu sahihi. Haielezi kwa sababu hazikuandikwa popote.

Yetu ni Zanzibar, nchi ya visiwa ambayo lolote lisiloweza kutokea kwingineko, huweza kutokea. Ni ajali tu kwamba hatuna hata jambo moja lililostahili kuingizwa katika orodha ya maajabu ya dunia.

Ni kwa sababu hizo si sifa nzuri. Ni sifa mbaya. Sifa zinazotakiwa ni zile zinazotambulisha wananchi wa Unguja na Pemba kama binadamu waliokamilika kiakili na kimantiki. Tunatenda mambo yetu kwa uadilifu na ufanisi.

Lazima tuamini utendaji wenye ufanisi dhidi ya ule uliochoka. Tukijali watu na maslahi yao, tutaamini kutenda kwa viwango. Watu wanaotenda mambo yao kwa kuzingatia na kufuata kanuni na taratibu.

Lipo jingine muhimu. Serikali inatakiwa kujali maoni ya wananchi kabla ya kuamua chochote ambacho athari zake hugusa maslahi yao .

Tumeona wazamiaji wa Afrika Kusini walivyoondoka bila ya kupata matokeo tuliyoyatarajia. Kilichotokea ni nini? Ni kweli hatukuwapa taarifa za kina mapema za asili ya ajali hivo wakaja na zana zisizotosheleza kufika kwenye kina kirefu?

 Wamesema hawawezi kufika kwenye kina walichokibaini cha mita zikaribiazo 40 kwa sababu zana zao hazitoshelezi mahitaji yao .

Pamoja na kasoro hiyo, wanastahili sifa nyingi maana katika muda mfupi wa kupenya baharini eneo ilipozama meli, wamesema ukweli. Hawataki kubahatisha. Jamani, hawa wamefunzwa wakafunzika.

Sasa serikali ijibu zilipo takwimu sahihi. Mbunge wa Ziwani, Ahmed Juma Ngwali, amekuja na zake na amezieneza. Anataja idadi ya waliokufa katika ajali ya meli kuzama kuwa 1,741.

Ngwali, mtoto wa Mzee Juma Ngwali, mwanasiasa mkongwe na muaasisi wa Chama cha Wananchi (CUF), anasema meli ilikuwa na zaidi ya watu 2,300.

Baada ya kupita maeneo mbalimbali ya Pemba na kukutana na familia za waliokuwa kwenye meli, anasema watu ambao hawajaonekana ni 108 jimbo la Kojani, Ole 157, Micheweni 88, Mgogoni 184, Wete 149, Gando 418, Konde 96, Mtambwe 214, na watu 182 katika jimbo lake la Ziwani.

Anajiapiza, “Ninachosema ndio ukweli wa jambo hili. Ikibainika ninasema uongo, nitajiuzulu ubunge.”

Idadi inaweza kutofautiana, lakini sayansi ya takwimu inahimiza yule anayezipinga, atoe zake ili aaminike. Mbunge anataka kuaminika na kwa kutoa takwimu hizi, baada ya kuzungumza na familia za wafiwa, aweza kuaminika.

Unatarajia tume ije na idadi inayoaminika. Idadi itakayofuta ile ya serikali, inayopingwa. Kila mtu anaimani waliozama na meli ni wengi.

Iwapi tume hii itakayoleta majibu haya? Tayari ni utata mtupu namna mashitaka yalivyoandaliwa. Unamkamata mmiliki wa meli ambaye si katika watendaji wa meli, unampa kesi. Unataka iweje?

Meli ilipaswa kukaguliwa, haikukaguliwa; nahodha na msaidizi wake walipaswa kubeba abiria na mizigo kwa kiwango kinachotajwa kitaalamu, haikuwa hivyo; hawa ndio wa kushika na kushitaki.

Unasikia shitaka moja linasomwa nahodha akiwa hajulikani alipo. Watu wakiamini wanachosikia kwamba amezuiwa kwenye vikosi, watakosea? Usiri katika kazi ya serikali ni dhambi.

Haya ni mambo ya aibu. Hivi ina maana meli haikusajiliwa? Wanaosajili meli ni wamiliki chini ya kampuni. Haijulikani? Nani wanalipa kodi za uendeshaji wa Spice Islander?

Inajulikana wenyewe wapo, serikali ikagoma kutaja. Ni nani Visiwani Shipping Co? Ni nani Makame Hasnuu Makame? Nani Salum Batash? Nani Yussuf Jussa Suleiman?

Kumbe wanataja majina yasiyokuwepo na bila ya sababu za msingi wanaficha wale halisi. Kwani kutaja wamiliki ni jinai? Meli ilikuwa na wanaoiongoza, liko wapi tatizo ukitaja wamiliki?

Ukisoma historia ya meli hii, unakuta Makame Hasnuu anatajwa ndiye mnunuzi aliyeelekeza meli iondoke nchini Oman kupelekwa Tanzania .

Katika safari hiyo, ilipofika 27 Septemba 2007, meli ilipata hitilafu eneo la mwambao wa Somalia baada ya injini zake kuzima kutokana na mafuta machafu yaliyowekwa.

Manuwari ya jeshi la Marekani iitwayo USS James E. Williams iliigundua na kusaidia kuwapa mafuta safi ili kuwasha tena injini. Wamarekani hao pia waliwasaidia wafanyakazi wa meli chakula na maji. Hatimaye ikaendelea na safari yake.

Serikali haijifunzi. Ikapeleka mahakamani mmiliki mmojawapo, Jussa, na kumsomea shitaka la kufanya uzembe kazini na kusababisha ajali ya meli iliyosababisha vifo.

Serikali ifike mahali iache mzaha katika mambo yanayohusu maslahi ya umma. Watu wanataka utendaji wenye tija na unaojenga shauku ya matumaini ya maendeleo.

Pale mahakamani, hati ya mashitaka haikuwa na taarifa za kina za watuhumiwa, udhaifu uliomsukuma wakili wao, Hamidu Mbwezeleni, anayejua vizuri utendaji wenye mazonge wa kazi za kimahakama, kulalamika.

Mwanasheria kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka wa Zanzibar alitamka mahakamani kuwa watuhumiwa wengine hawapo mahakamani. Mmoja wao ni nahodha wa meli, Said Abdallah Kinyanyite, 58, mkazi wa Mbagala Charambe, jijini Dar es Salaam .

Serikali ina mtihani. Mahakama Kuu imekubaliana na hoja ya wakilio Mbwezeleni aliyeomba kesi hiyo isimamishwe ili kupisha tume ya rais ya kuchunguza chanzo cha ajali hiyo kufanya kazi yake.

Hatimaye watuhumiwa ambao walikuwa rumande tangu wiki iliyopita, wameachiwa kwa dhamana ya maandishi hadi kesi hiyo itakapokuja kusikilizwa baada ya uchunguzi kukamilika.

Hilo likitendeka kuihusu kesi, tayari watu wanahoji hadhi ya tume iliyoundwa kwa kuwa baadhi ya wajumbe wake, wana uhusiano wa damu na au kikazi na watendaji wa mamlaka za usimamizi wa masuala ya usalama wa usafiri bandarini.

Mjumbe mmoja ambaye ni mwanasheria mahiri, ni mmoja wa wajumbe wa Bodi ya Shirika la Bandari Zanzibar, moja ya taasisi zinazolaumiwa kwa kutojenga mtandao wa ukaguzi na usalama wa vyombo japo inakusanya mapato mengi kila mwaka.

Muendelezo wa shaghalabaghala.

0
No votes yet