Wamevujisha majibu kuficha aibu


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 14 December 2011

Printer-friendly version
Tuseme Ukweli

MATUKIO na malalamiko ya kuvuja kwa mitihani ya taifa nchini yamekuwa yakisikika tangu lilipoanzishwa Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) mwaka 1973.

Baadhi ya wazazi wenye fedha au nafasi serikalini au taasisi za umma, -wakishirikiana na wafanyakazi wasio waaminifu wa Necta, wamekuwa wakiiba mitihani na kuiuza.

Hata hivyo, wizi na uvujishaji ulipamba moto katikati ya miaka 1980 hadi mwanzoni mwa miaka ya 2000.

Habari za kuvuja au wanafunzi kupatiwa majibu ya mitihani ziliripotiwa sana ilipokaribia na wakati wa mitihani ya kuhitimu elimu ya msingi au sekondari.

Matukio yaliyowahi kuandikwa sana kwenye magazeti na wilaya kwenye mabano ni kama: Wanafunzi wabambwa na majibu ya mtihani kwenye rula (Bagamoyo).

Wanafunzi wabadilishana majibu kwenye karatasi za rafu (Morogoro) Msimamizi wa mitihani abambwa akitafuna karatasi ya majibu (Seerengeti) Walimu saba wanaswa na polisi wakiandaa majibu kwa ajili ya watahiniwa (Tabora) Msimamizi mkuu aenda sokoni akiacha watahiniwa kwenye chumba cha mtihani (Magu) Mtihani wa hisabati wapelekwa ofisini walimu wasaidie majibu (Mara) Walimu wanaswa na msimamizi mkuu wa wilaya wakiandaa majibu ofisini (Muleba) Hivi ni visa vichache vilivyoripotiwa kuhusu ukiukwaji wa usimamizi wa mitihani ya kuhitimu elimu ya msingi. Kati ya mwaka 2000 na 2005 baadhi ya maafisa elimu na wakuu wa shule walihusishwa kwenye njama za kufaulisha wanafunzi.

Katika ngazi ya sekondari, wizi na uvujaji wa mitihani umekuwa mkubwa sana na tukio lililoiabisha serikali ni lile la mwaka 1998 ambapo hata mama lishe walikutwa wakiuza karatasi za mtihani kwa Sh. 200 tu.

Mitihani yote ilifutwa na ukatungwa mwingine.

Mwaka 2008 mtihani wa hisabati ulivuja na ukafutwa, ukatungwa mwingine. Hakukuwa na taarifa za wizi wala uvujaji wa mitihani mwaka 2009 na 2010 isipokuwa mikakati ya kufelisha wanafunzi.

Mwaka huu mitihani ya kuhitimu elimu ya sekondari na msingi haikuvuja na wala haikuibiwa ila, majibu ya mtihani wa elimu ya msingi ndiyo yamevuja. Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Phillip Mulugo aliwaambia waandishi wa habari kwamba wanafunzi wote 515,187 waliofaulu kuingia kidato cha kwanza 2012 watafanya mtihani upya kupima tena uwezo wao.

Kwanini? Mulugo alisema ni kutokana na kuwepo kwa kiwango kikubwa cha udanganyifu mwaka huu. Hapa serikali inatafuna tu maneno. Anachosema ni kwamba wanafunzi wengi wamepewa majibu ndiyo maana hata makosa yanafanana.

Kisiasa, Mulugo anafurahia wanafunzi 567,567 kufaulu sawa na asilimia 58.28 ya 983545 waliofanya mtihani, na akatamba hilo ni ongezeko la asilimia 4.76 la matokeo ya mwaka jana.

Lakini anapotazama ripoti ya usahihishaji mitihani, Mulugo anakiri waliofaulu kihalali ni wachache sana, udanganyifu umekuza idadi hiyo.

Mulugo anasema, kutokana na kuwepo kwa kiwango kikubwa cha udanganyifu mwaka huu, serikali imeweka mtihani wa majaribio ambao utafanywa na wanafunzi hao waliochaguliwa kabla ya kuanza kidato cha kwanza ili kuwafukuza watakaobainika kufaulu huku hawajui kusoma, kuandika na kuhesabu.

Hapa serikali haiamini kwamba wanafunzi 9,736 ambao wamefutiwa matokeo ni wao tu; baadhi wamepenya na kupata nafasi ya kuingia sekondari.

Ukweli ulivyo Matokeo haya ya darasa la saba ni usanii ulioandaliwa kiufundi na maafisa elimu wa wilaya na walimu wakuu wa shule ili kufunika aibu nyingine ambayo serikali ilipata kwa matokeo ya kidato cha nne.

Matokeo ya kidato cha nne mwaka 2010 yaliyotangazwa Januari mwaka huu, yalionyesha kwamba asilimia 88 ya wanafunzi walifeli. Kufeli kwa kiwango kikubwa cha wanafunzi hao na hata wa ‘darasa la saba’ mwaka huu, kuliandaliwa tangu mwaka 2008.

Katika mkutano na maofisa elimu, walimu wakuu wa shule na vyuo, wataalamu wa elimu na wasomi uliofanyika ukumbi wa Ubungo Plaza, Dar es Salaam, Rais Jakaya Kikwete alipendekeza kwamba mitihani ya kidato cha pili na darasa la nne isiwe kikwazo katika “juhudi za kuimarisha elimu.” Pendekezo hilo likawa amri kwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi wakati ule, Prof. Jumanne Maghembe. Akatangaza bungeni mitihani hiyo miwili ‘imefutwa’.

Wabunge wakashangilia.

Alisema mitihani itakuwepo lakini haitatumika kuchuja vijana waliofeli ila wataendelea na masomo ya kidato cha tatu na darasa la tano.

Madhara ya kufutwa mitihani ile ndiyo yanaonekana sasa. Vijana walioingia kidato cha kwanza mwaka 2006 walipaswa kumaliza kidato cha nne mwaka 2009. Lakini waliofeli mtihani wa kidato cha pili mwaka 2007, walirudia darasa hilo mwaka 2008 wakawa pamoja na walioanza kidato cha kwanza 2007.

Kwa kuwa, baada ya kufutwa mtihani wa kidato cha pili mwaka 2008 waliofeli wote waliingia kidato cha tatu mwaka 2009 hadi kidato cha nne mwaka 2010, matokeo yakawa mabaya kupita kiasi.

Kwa upande wa shule za msingi, wanafunzi waliofanya mtihani wa darasa la VII mwaka huu, mwaka 2008 walikuwa darasa la nne.

Ulipofutwa mtihani wa darasa la nne, wanafunzi hata wale wasiojua kusoma, kuandika na kuhesabu wakaserereka hadi darasa la saba bila kikwazo.

Wanafunzi wale mwaka 2009 walikuwa darasa la V, mwaka 2010 walikuwa darasa la VI na mwaka 2011 wakahitimu darasa la VII.

Mikakati iliyowekwa na walimu wakuu na shinikizo kutoka kwa maafisa elimu kukwepa aibu kama ya kidato cha IV mwaka jana, kazi ikawa ‘kusaidia’ kupata matokeo mazuri.

Hatua ya serikali kuwapima tena wanafunzi walioingia kidato cha kwanza, inamaana wanashaka na ufaulu wa asilimia 58.28, inaona wamebebwa. Je, wakifeli nani watajaza nafasi zao? Mwezi uliopita nilitembelea shule za msingi wilayani Mbinga nikiwa na waandishi watatu wa mkoani Ruvuma. Katika baadhi ya shule za kata za Liwundi na Ngumbo, wazazi walisema wanachangishwa fedha za “kuimarisha ufaulu” wa watoto wao.

“Mitihani ya kumaliza elimu ya msingi inapokaribia, walimu wakuu hutaka wazazi wachangie fedha kwa kile wanachodai kuimarisha ufaulu wa watoto wetu,” alilalamika mzazi mmoja, ambaye mtoto wake anasoma shule ya msingi Mkili.

“Tabia hii, husababisha watoto wenye uwezo mdogo kwenda sekondari,” anaeleza mkazi mwingine wa kijiji hicho.

Charles Kapinga, ambaye ni makamu mkuu wa shule ya sekondari ya Ngumbo inayochukua watoto waliofaulu kutoka shule za msingi kata za Liwundi na Ngumbo, alilalamika kwamba baadhi ya wasiojua kusoma na kuandika wako shuleni kwake.

Tulimuuliza, “Wamepitaje hawa?” Alijibu, “Kawaulize walimu wao wa shule ya msingi!” Mwenye majibu mazuri kwa kadhia hiyo ni Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Ruvuma, Dk. Anselim Tarimo ambaye amewasimamisha walimu wakuu saba kwa kuchangia “kuimarisha ufaulu” wa watoto. Kati yao wawili wanatoka shule za msingi za Mnazi Mmoja na Rulala wilayani Mbinga.

0789 383 979
0
No votes yet