Wamiliki mgodi North Mara wabanwa kila upande


Mwandishi Maalum's picture

Na Mwandishi Maalum - Imechapwa 05 May 2010

Printer-friendly version
Gumzo

KUPORA, kujeruhi na kuua – vitendo ambavyo vimekuwa sura ya wamiliki na walinzi wa mgodi wa dhahabu wa North Mara – kunaendelea kuwachefua wakazi wa Nyamongo.

Ingawa serikali haichukui hatua, inajua hilo. Hakuna kiongozi wa serikali ngazi ya kitaifa aliyeshuhudia kuchefuka huko kama Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja.

Ni Ngeleja ambaye alishawekwa kikaangoni kuhusiana na ukimya wa serikali juu ya uporaji unaofanywa na kampuni ya Barrick inayomiliki mgodi wa North Mara.

Ilikuwa karibu na mwishoni mwa bunge la bajeti mwaka jana. Mahali: Nyangoto Centre – makao makuu ya kata ya Nyamongo wilayani Tarime mkao wa Mara.
 
Ngeleja alikumbana na wananchi uso kwa uso. Walilenga kuwasilisha kilio chao dhidi ya kampuni ya Barrick. Walimuuliza maswali matatu ambayo hatasahau maishani:

Swali 1: Ukiwa waziri mwenye dhamana ya Wizara ya Nishati na Madini, tuonyeshe mipaka kati ya mgodi huu wa North Mara na makazi ya wananchi.

Swali 2: Ukiwa mwanasheria na waziri wa nishati na madini, tuonyeshe umbali unaotakiwa kisheria kutoka mgodini hadi makazi ya watu.

Swali 3: Kwa kuwa sisi hatujui sheria, tusomee sheria inayoruhusu mgodi kulipua mawe, yakaruka na kuanguka kwenye nyumba za wananchi; pia tueleze sheria hiyo ni ya mwaka gani.

Aliyeuliza maswali yote matatu ni mwananchi mkazi aitwaye Christopher Iroga, ofisa mstaafu wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ).

Ni Iroga ambaye nusu ya shamba lake la ekari tatu na nusu limeporwa na mgodi huku kuta za nyumba zake nyingine zikipata nyufa kutokana na milipuko ya baruti mgodini isambazayo mtetemeko.

Maswali hayo yalimtesa Ngeleja kwa sababu inadaiwa aliishawajuwa wakazi wa Nyamongo kuwa wanashirikiana na mwanaharakati Tundu Lissu wa Chama cha Wanasheria wa Mazingira (LEAT). Tundu Lisu amekana kufanya kazi na Ngeleja.

Ngeleja alisimama, akakohoa kidogo kwa njia ya kusafisha koo, akashika kipaza sauti na kuanza kujibu: “Hatua mita tano…”

Hapo ndipo umati ulipolipuka. Ukaanza kumzomea. Alionekana kujibu swali la pili la umbali kutoka kwenye mgodi; lakini sehemu hiyo ya utangulizi ghafla ikajenga utata.

Iwe “mita tano” kutoka wapi – kwenye machimbo ambako kuna mpasuko au kutoka uzio unaotenganisha eneo la mgodi na makazi ya wananchi ambako umbali ni kama mita 150?

Vyovyote iwavyo, hata wananchi walio mita 300 kutoka uzio, wana malalamiko yaleyale ya nyumba zao kupigwa mawe yatokayo mgodini na kuta zake kupata nyufa kwa tetemeko litokanalo na mipasuko ya baruti mgodini.

Ngeleja alikuwa katika ujumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Mazingira na Maliasili chini ya mbunge wa Kongwa, Job Ndugai.

Waliokuwepo wanasema “hali ya hewa ilichafuka na polisi wakaingilia kati kutuliza hasira na ghadhabu za wananchi waliotaka kumrudi waziri.”

Mkutano wa Nyangoto Centre ulikuwa wa tatu baada ya ile ya Kewanja na Nyarwana ambako wanaathiriwa na maji yenye sumu inayoingia katika mto Tigithe kutoka mgodini. 

Kuna taarifa kuwa Ngeleja aliwahi kutembelea maeneo haya na kutamka kuwa anataka kuona kampuni ya East Africa Goldmine (EAGM) iliyochukua kwa hila, mashimo ya madini na mashamba ya wananchi, ikiwafidia wakazi hao.

Vilevile alinukuliwa akiwaambia wananchi kwamba mgodi unapaswa kuwa mbali na makazi ya watu.

Ndiyo maana alipochanga vema karata zake na kuwa mbunge; na baadaye kuteuliwa kushika wadhifa wa naibu waziri wa nishati na madini, Ngeleja alikwenda Nyamongo kuwapa matumaini juu ya madai yao.

Wakati huo waziri alionya, hata hivyo, kwamba hakuwa na kauli ya mwisho kwa vile hakuwa “waziri kamili.”

Lakini miezi michache baadaye alipoteuliwa kuwa waziri kamili wa wizara hiyo, Wanyamongo walimshangilia kwa nguvu wakiamini waziri huyo kijana atavunja vikwazo vyote vinavyozuia haki zao.

Kumbe wananchi walijenga matumaini hewani. Ngeleja wa sasa siyo yule waliyemfahamu. Leo hawataki kumwona.

Maswali aliyouliza Iroga ndiyo kilio cha wakazi wote wa Nyamongo hadi leo. Mashamba, nyumba, viwanja na machimbo yao madogo; vyote vilikumbwa katika hekta 671 zilizouzwa kinyemela na viongozi wa vijiji kwa mgodi wa North Mara.

Baada ya Iroga pamoja na wamiliki wengine wa mashamba na mali kadhaa kugundua wameporwa haki zao, walianza mapambano dhidi ya EAGM mwaka 1998.

Walifanya vikao na viongozi wa vijiji, wenyeviti na maofisa watendaji kupata ufumbuzi. Waliandika barua wilayani kuomba msaada na hadi kwa Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Gideon Cheyo.

Mgogoro na kampuni ulianza mwaka 1998 baada ya kampuni kuanza kuhamisha watu kwa nguvu kupisha upanuzi wa machimbo ya Nyabirama.

Iroga anasema, “Baadhi ya watu walipokea kiasi kidogo cha fidia lakini wengine tulioona fidia ni ndogo, tukaikataa. Mimi sikupokea fidia.” anasema Iroga.

Mwaka 2000 kampuni ilianza kuvunja na kung’oa miti ya matunda, nyumba, mashamba na waliobaki katika eneo hili wakawa wanalima chini ya ulinzi wa polisi.

“Katika shamba langu kulikuwa na nyumba nne, choo, kisima cha maji ya kumwagilia shamba na miti ya matunda; vyote wakang’oa kwa nguvu,” anasema Iroga.

Akionyesha kuwa katika hali ya masikitiko, Iroga anaonyesha, “Sehemu hii ambayo ni nusu ya shamba langu la ekari tatu na nusu ilivunjwa kwa mabavu na ndipo wamepanulia shimo; wanachimba dhahabu sasa.”

Kutokana na upinzani mkali na harakati ambazo aliongoza, Iroga  anasema alifunguliwa kesi yenye mashitaka tisa. Alifanikiwa kupangua mashtaka sita lakini akatiwa hatiani kwa mashtaka matatu na kufungwa kwa miaka mitatu.

Mashtaka yaliyosababisha afungwe yalikuwa kuingia kwenye mgodi, kukaa mgodini na kuchochea wananchi kuingia mgodini. Anasimulia kuwa akiwa jela, EAGM ilimtega.

“Nikiwa jela kampuni ilituma wanasheria kuja kunishawishi kwamba nikikubali kuhama eneo langu la Nyabirama wataniachia jela. Mimi niliwaambia siachii eneo langu, mimi ni kama Mandela; kama nitafia jela basi nife, lakini siwezi kuachia dhuluma itawale kwenye haki yangu,” alisema.

Iroga alifungwa pamoja na wakazi wenzake saba wakiwemo Raphael Dede (mwenyekiti wa kitongoji cha Nyabigeni, Masiaga Meng’eni (diwani wa kata ya Kemambo), Augustino ‘Neto’ Sasi mkazi wa kijiji cha Kewanja. Walishinda karika rufaa na kuachiwa mwaka 2003.

Aidha, hiyo haikuwa mara ya kwanza kwa Iroga kufunguliwa mashitaka. Mwaka 1998 alifunguliwa kesi kwa kile kilichoitwa kukataa kuhama kwenye eneo ambalo mgodi ulianza kudai kwamba ni lake.

Hata hivyo, kesi iliyokuwa inamkabili yeye na wenzake sita, haikufika mbali. Mgodi uliamua kuifuta na kuwalipa gharama zote za uendeshaji kesi, nauli na posho.

Wengine waliokuwa wamefunguliwa mashtaka katika kesi hiyo ni ndugu zake wawili Maselo Iroga na Mustafa Iroga. Wengine ni Daniel Nyamahe, John Marecho na Steven Msaroche.

“Hadi leo hatujafidiwa wala kufanyiwa tathmini ya mali zetu kama alivyoagiza aliyekuwa mkuu wa wilaya, Stanley Kolimba,” anasema.

Mwaka 2003 ulikuwa wa mwisho kwa Wanyamongo kupambana na EAGM kwani kampuni iliuza hisa zote kwa kampuni ya Placer Dome ambayo pia mwaka 2006 iliuza hisa zote kwa Barrick.

Kwa mujibu wa nyaraka zilizopo, tarehe 10 Novemba 1995 ndipo serikali ya Kijiji cha Ujamaa Nyangoto ilimpa Iroga eneo ambalo analalamikia sasa.

Pamoja na kuwa na hati halali, wananchi wa vijiji vyote, hasa Nyangoto wametoswa na serikali za wilaya, mkoa na taifa hadi leo. Lakini juhudi za wananchi kutafuta ufumbuzi zimekuwa zikiendelea.

Tarehe 4 Juni 1999 kijiji cha Nyangoto kiliitisha kikao cha dharura kwa ajili ya kupitia majina yaliyoorodheshwa na wenyeviti wa vitongoji kwamba hawakufanyiwa tathimini ya mali zao na kwa hiyo hawakufidiwa.

“Baada ya wenyeviti wa vitongoji kuthibitisha kuwa hayo majina waliyoandika ni ya kweli na hao watu wanahitaji mali zao zifanyiwe tathmini, serikali ya kijiji imemuomba mthamini wa mali wa wilaya ya Tarime aje afanye tahmini ya mali za wananchi hao,” inasema sehemu ya muhtasari wa kikao hicho.

Viongozi waliohudhuria kikao hicho ni kutoka vitongoji vya Nyangoto, Mjini Kati, Nyabikondo, Nyabichune na Kwimange.

Tarehe 6 Juni 1999, afisa mtendaji wa kijiji cha Nyangoto alipokea muhtasari wa kikao cha serikali ya kijiji na akautumia kuandika barua kwa mthamini mfawidhi wa wilaya ya Tarime ili aende Nyamongo kufanya tathmini. Hadi leo hakuna kilichofanyika.

Tarehe 18 Julai 2003 aliyekuwa Mbunge wa Tarime, Kisyeri Chambiri alijitosa kwenye sakata hilo kwa kumtaka Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi Gideon Cheyo aingilie kati. Mbunge huyo alipuuzwa.

Katika barua yake aliyoipa kichwa “Malalamiko juu ya mwenendo mzima wa zoezi la ukadiriaji wa mali na makazi eneo la Gokona kijiji cha Kewanja na kijiji cha Nyangoto”, Kisyeri alisema wananchi wake wananyanyaswa na kampuni ya EAGM.

“Pamoja na barua hii naambatisha barua ya wananchi wa Gokona… Wananchi hao wananyanyaswa na Kampuni ya EAGM na mali yao imethaminiwa kulipwa fedha ambayo hailingani na thamani yake. Wakilalamika hawasikilizwi na tatizo linaendelea,” alisema Kisyeri.

Hadi sasa si mthamini mfawidhi wa wilaya wala mawaziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi; Nishati na Madini wala Mazingira waliojaribu kutafuta ufumbuzi wa matatizo ya wananchi.

Mapambano ya wakazi wa Nyamongo yameelekezwa dhidi ya Barrick iliyonunua hisa zote za mgodi mwaka 2006 kutoka Placer Dome iliyokuwa inauendesha tangu mwaka 2003 ilipoununua kutoka kwa EAGM.

Mwaka 2008 Barrick iliridhia kuundwa kamati ndogo ya wanasheria pamoja na wananchi wa vijiji vitano vya Genkuru, Kewanja, Kerende, Nyangoto na Nyamwaga. Kampuni ilimwita pia Iroga ili wafikie suluhu.

“Barrick waliniita kwa majadiliano Mwanza. Tukafanya kikao na wanasheria wao. Walitaka wafanye tathmini shamba lililopo; mimi nikakataa. Nikawaambia watumie hati za kisheria zilizopo wanifidie eneo lote pamoja na lililolimwa. Tumekwama hapo,” anasema Iroga.

Taarifa ya kamati ndogo ya maridhiano ya kupitia mikataba ya uchimbaji madini iliyoketi tarehe 21 Oktoba 2008 inaonyesha kilipitiwa kiambatisho Na. 7 kisemacho “Ardhi kwa shughuli za uchimbaji.”

Kamati inasema, “Ardhi iliyokwisha chukuliwa bila fidia ifidiwe sasa ikiwa ni pamoja na watu waliofidiwa mazao pekee kuanzia mwezi Januari 2008.

“Watu waliohamishwa na mgodi bila kujengewa nyumba, wajengewe kwa kuwa ni haki yao. Pia Matongo na Nyakunguru wapewe mrabaha kwa ardhi yao iliyochukuliwa na kampuni ambayo ni hekta 225…” inasema taarifa ya kamati.

Barrick imekuwa “kichwa ngumu” na wananchi wanaendelea kudhulumiwa huku serikali ikiendelea kuwa kimya, hata wakati huu wa kuelekea uchaguzi mkuu.

0
No votes yet