Wamisri wambwagia kero rais mpya


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 04 July 2012

Printer-friendly version

SIKU chache baada ya kuingia madarakani, rais mpya wa Misri, Mohamed Mursi (pichani), sasa anakabiliwa na changamoto ya kutatua matatizo ya wananchi yaliyotokana na utawala wa kimabavu wa rais wa zamani wa nchi hiyo, Hosni Mubarak.

Jumapili iliyopita, makundi ya wananchi walikusanyika karibu na eneo la ikulu ili kupeleka malalamiko yao kwa Mursi.

Malalamiko hayo ni pamoja ukosefu wa kazi, kutolipwa pensheni na fidia ya serikali kutokana na ndugu zao kufungwa jela baada ya kukamatwa katika utawala wa Mubarak kwa madai ya kufanya maandamano ya kumpinga Mubarak.

"Jina langu ni Alaa Ahmed Bayoumy na nipo hapa kwa ajili ya kuomba kulipwa pensheni yangu. Nina zaidi ya watoto watano na gharama ya kodi yangu ni kubwa zaidi ya pensheni yangu. Suala hilo halikubaliki kabisa." alisema Bayoumy mmoja wa waandamanaji.

Kati ya watu waliotaka kuonana na Mursi, ni wanawake watatu - Nahed Hussein Abdel Fattah, Marwa Khaled na Nadia Mohamed Ahmed – ambao wanataka kutolewa gerezani kwa baadhi ya ndugu zao ambao walikamatwa wakati wa utawala wa Mubarak.

Hata hivyo, wananchi hao waliruhusiwa kupumzika katika bustani nje ya eneo la ikulu, ambapo walikula na kunywa. Katika utawala wa Hosni Mubarak, wananchi wa kawaida wa Misri hawakuruhusiwa kukaribia katika eneo la ikulu.

Taarifa zinasema kuwa, Mursi akionekana kuwa na shauku ya kuonyesha udhaifu wa serikali iliyopita, alisema kuwa hatakuwa na utani na badala yake atatafuta haki kwa Wamisri wote, wakiwemo wale waliouawa au kujeruhiwa katika maandamano.

Katika utawala wa Mubarak, maandamano ya kisiasa hayakuruhisiwa, wakati kukiwa na ulinzi mkali na idadi kubwa ya polisi waliokuwa wakikamata wananchi waliojaribu kufanya hivyo.

Taarifa zaidi zinasema kuwa, siku hiyo idadi kubwa ya polisi na maofisa wa usalama walikuwa wakijaribu kuwazuia wananchi wakihofia kuwa wataingia eneo la ikulu, na walikuwa wakichukua majina ya watu ambao walikuwa wakiandika maombi ya kuomba msaada.

Mwanamke mmoja mzee, Ahlam Mohamed, aliyekuwa amekaa juu ya mawe alisema “Nataka kazi kwa mtoto wangu. Amekuwa akikaa nyumbani kwa miezi kadhaa sasa na yeye ndiye anayetulisha. Bila yeye tutakufa.”

Haitham Ezzat, 29, yeye alikuwa akitaka kufidiwa na serikali mpya kutokana na kupata majeraha ya usoni yaliyomfanya aache kazi wakati wa vuguvugu la maandamano ya kumwondoa madarakani Mubarak.

"Natumaini kukutana na rais," alisema mwanaume mwingine wa miaka 61,  Sayed Rashad, ambaye alisema kuwa hajafidiwa kutokana na majeraha aliyoyapata wakati wa utawala uliopita.

Katika mkusanyiko huo, wafanyakazi wengi waliokuwa wakifanya kazi wakati wa kipindi cha Mubarak walikuwa wakilalamika na kuorodhesha majina ya kampuni 15 ambazo wanazishutumu kwa kuwafukuza kazi.

"Tupo hapa kumweleza rais atusaidie haraka iwezekanavyo. Tunataka kulipwa na kutimiziwa haki zetu zote," alisema Atef Mondy, 38, kiongozi wa wafanyakzi waliofukuzwa.

Asilimia 40 ya Wamisri wanaishi chini ya dola 2 kwa siku. Uchumi unashuka na idadi ya watu wasio na kazi inaongezeka kutokana na mtikisiko wa kisiasa ulioathiri sekta ya uwekezaji na utalii.

Kutokana na hali hiyo, inaonekana itakuwa vigumu kwa  Mursi kutumia njia yake kujipatia umaarufu. Programu yake ya sera kwa kiasi kikubwa inasukumwa na soko huria katika uwekezaji, huku ikionekana kuongeza maumivu katika uchumi wa nchi hiyo kwa kipindi kifupi kijacho.

Suala hilo linaonekana kuwa litawashtua wananchi wengi ambao wanaonekana kuwa na matumaini na Mursi kuwa atabadilisha mwelekeo wa serikali na kuleta manufaa kwa kiasi kikubwa.

Kwa sasa, Mursi ameahidi kuchukua hatua hasa katika masuala ya kijamii, kudumisha ulinzi, pamoja na kupunguza ugumu katika usambazaji wa mikate, petroli na gesi ya kupikia.

0
No votes yet