Wanajilipua, kuilipua Sisiem


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 06 June 2012

Printer-friendly version
Waraka wa Wiki

ASKARI yeyote wa miguu anapokuwa kwenye uwanja wa vita huwa mwangalifu kupita kiasi. Haokoti vitu ovyo, wala hapendi kukanyaga sehemu tifutifu.

Hofu yake kubwa ni mabomu ya kutegwa ardhini huku yeye mwenyewe akitembea amejihami kwa bunduki na mabomu ya kurushwa kwa mkono.

Madhara ya bomu la kutegwa ardhini ni makubwa sana na wakati mwingine wanaoathirika zaidi ni raia wasio na hatia. Baadhi ya mabomu hufyatuka kipindi cha vita lakini mengine hulipuka na kuua raia hata baada ya vita kumalizika.

Magaidi wamebuni mtindo mpya wa kujitoa mhanga. Binadamu huvaa bomu na kutembea nalo hadi kwa watu aliokusudia kuwateketeza.

Mtindo huu ni mbaya kwa vile hata rafiki yako anaweza kuvaa bomu akakusogelea, hapo atawasha na kujilipua “puuuuuuu”.

Mtu anayejitoa mhanga amejaa chuki, hasira, ukosefu wa upendo, hana amani moyoni hivyo yuko tayari kufa na anaona heri kufa kuliko kuishi katika madhila hayo.

Mwanzoni walikuwa wanatumiwa vichaa na punguani, lakini leo hata wasomi wa hali ya juu kama waliotumika katika mashambulizi ya 11 Septemba 2001 nchini Marekani.

Marafiki, wanasiasa na makada walioonekana watiifu kwa Sisiem wakateuliwa kuwa mawaziri, wameiga mtindo huu wa “kujilipua” ili kulipua waliokusudiwa.

Dereva wa basi la Sisiem ana hofu, abiria wanahaha, safari ya kuelekea mwaka 2015 imeingia nuksi. Abiria (wanachama) woga wameanza kutokea madirishani kwa usalama wao.

Ndani ya basi kuna mkanyagano, kila mmoja anataka kujiokoa kivyake, kuna vurugu, mtifuano, zogo na baadhi wanarudisha tiketi (kadi), hawataki safari huku makada wakijilipua ili kulipua basi (chama) zima liteketee kabla ya mwaka 2015.

Wanaotisha ni vijana walioaminiwa tangu mwaka 2005 wakapewa kazi ya kusimamia vitalu (maliasili na utalii), bili za umeme (nishati na madini), ufundi mchundo (viwanda na biashara), usafirishaji (uchukuzi) na siha za watu (afya) sasa wanatembea na mabomu mfukoni.

Dereva kaambiwa kuna magaidi na mamluki ndani ya basi, lakini anapogeuka anawaona ni vijana wake kabisa Ezeka Uige, Sirihii Chanini. Wanajua wanachokifanya na aghlabu hata hatima yao.

Anajipa ujasiri; aliwahi kukwepa mabomu ya kurushwa kwa mkono (ufisadi ulioibuliwa na CHADEMA Septemba 2007), mabomu aliyotegewa ardhini na marafiki zake (ufisadi wa Richmond). Hivyo siasa hizi za umamluki kama alivyosema kijana wake wa propaganda kule Kagera, hazimtishi.

Kila akijipa likizo Ulaya, Marekani, Ethiopia kwenye misiba Malawi na mikutano akirudi tafrani ndani ya basi iko palepale; huku Nato wanapiga, kule G8 wanalipua, vijana wanarusha mabomu – vita ya kuelekea uchaguzi mkuu 2015.

Walioko kando ya barabara (wapinzani) wanashangilia kwa furaha wakiwa na uhakika, kwa mwendo ule, basi la Sisiem ambalo nyuma limeandikwa Ari zaidi, Nguvu zaidi na Kasi zaidi litaanguka.

Hali ya hewa ni ya hasira, chuki, kiwewe, masikitiko, na kicheko. Si unajua vita vya panzi ni furaha kwa kunguru?

Waliosimama kando wanaijua vizuri methali isemayo, “ ndugu kwa ndugu wakigombana, wewe chukua jembe ukalime, wakipatana wewe chukua kapu ukavune” na huu ni wakati wa wapinzani kuvuna wanachama wanaokimbia vita. Mafisadi wanapiga na waliopokwa uwaziri wanalipua.

Baadhi wameapa kuuza viti vyao kwa wapinzani mwaka 2015, wengine wanajitabiria basi lao halitafika mwaka 2015 halafu wapo wanaochekea chooni kuona basi ni mkweche.

Angekuwepo Pwagu (marehemu) angecheka kwa nguvu mahokaaaaaaaaaaaaaaaa!

0658 383 979
0
No votes yet