Wanamlilia Gaddafi au fedha zake?


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 26 October 2011

Printer-friendly version
Tafakuri

TANZANIA imeamua kumlilia aliyekuwa kiongozi wa Libya, Kanali Muammar Gaddafi, aliye uawa na wananchi wake wenyewe mithili ya kibaka ashughulikiwavyo na wananchi wenye hasira. Gaddafi amekufa kifo cha aibu, mwili wake umeonyeshwa kama wa mnyama ukiwa hauna staha yoyote.

Msimamo wa Tanzania ulitolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe wiki iliyopita. Kwa msimamo huo, serikali imeweka bayana kwamba Watanzania hawana tabia wala utamaduni wa kusherehekea kifo cha mtu hata kama ni adui yake. Aliweka msisitizo kwa kusema, “Tumesikitishwa na kifo cha Gaddafi namna kilivyotokea.”  
 
Ni jambo jema na ni uungwana kutokusherehekea kifo cha mtu. Hili linaeleweka. Lakini nani anachagua aina ya kifo chake? Hili ni swali ambalo sote ingefaa tujiulize. Kuna usemi unasema kuwa mtu hupamba kaburi lake mwenyewe. Usemi huu unabeba maana nzito.

Kwamba unavyoishi ndivyo unajenga heshima yako kwa jamii, ama muungwana na mtetezi wa wanyonge, kimbilio la wenye shida au jitu katili, lisilokuwa na huruma, bazazi, mwenye mikono iliyojaa damu, na kwa maana hiyo huruma ya watu wengine kwako wakati wa siku yako ya mwisho mara nyingi inategemea sana na ulivyoishi.

Miongoni mwa mambo ambayo yamekuwa kwenye mjadala kuhusu kuuawa kwa Gaddafi ni uwezo wa Umoja wa Afrika (AU). Wapo wanaojiuliza kama AU ina kazi hasa inaposhindwa kuingilia kati migogoro mingi, mmojawapo wa Libya?

Nitapanua kidogo juu ya AU na kutaja hata zele jumuiya za kikanda katika bara la Afrika. Hapa nitagusa Jumuiya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC); Jumuiya ya Uchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) na hata Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Wakati majeshi ya Umoja wa Kujihami wa Nchi za Magharibi (NATO) yalipoanza kuitwanga Libya yakitekeleza azimio la Umoja wa Matifa namba 1973 la kupigwa marufuku kwa ndege za Gaddafi kuruka (no flying zone), hakuna kiongozi wa bara hili alisimama na kulaani hatua huyo. Hakuna! AU kama kawaida yake iliendelea na tabia yake ya ukilema kwa kutofanya lolote. Hii ni jadi na ndiyo msimamo wa viongozi wa bara la Afrika.

Kwamba viongozi wa bara hili wamegeuza nchi zao shamba la bibi. Wamechochea vita vya wenywe kwa wenyewe, mateso makubwa kwa raia wake, na kila aina ya ukiukaji wa haki za binadamu.

Kuanzia Madagascar, ambako kijana mdogo tu Andry Rajoelina akiwa ni meya wa jiji la Antananarivo alikoendesha uasi dhidi ya rais aliyechaguliwa kidemokrasia, Marc Ravolmanana, 10 Machi 2009.

SADC ilijitutumia kuingilia kati, lakini hadi sasa hakuna kinachoendelea, Rajoelina bado yuko madarakani licha ya kutokuwa na sifa ya kuwa raia kwa maana ya umri.

Nchini Zimbabwe, rais Robert Mugabe hakushinda uchaguzi uliyopita. Lakini kwa kiburi tu, akaendelea kung’ang’ania madaraka. SADC ikiajitutumua lakini hakuna ilichovuna mbali ya kuendelea kumkumbatia Mugabe.

Hali ni hiyo hiyo kwa mataifa ya ECOWAS. Rais Laurent Gbagbo, hakushinda kwenye uchaguzi wa mwaka jana, akang’ang’ania madaraka. ECOWAS hawakufanya lolote hadi vikosi vya Alassane Ouattara, ambaye ndiye alishinda uchaguzi huo vilipomfurusha na kumtia mbaroni akiwa amejificha kwenye mtaro. Ni kama alivyojificha Gaddafi na kama ambavyo alipata kujificha Saddam Hussein wa Iraq.

Mwaka 2007 Afrika Mashariki ilishuhudia umwagaji mkubwa wa damu ambao haujawahi kuonekana baada ya uchaguzi kuchezewa nchini Kenya. Rais Mwai Kibaki wa nchi hiyo hakushinda.

Ilikuwa wazi, aliiba uchaguzi, inajulikana, lakini Kibaki bado yuko madarakani kwa kisingizio cha serikali ya umoja wa kitaifa kama ile iliyoundwa kule Zimbabwe ambayo imeshindwa kufanya kazi. EAC haikufanya lolote kwa Kenya. Kinachosaidia sasa ni Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) ambayo imewashitaki baadhi ya wanasiasa wa Kenya.

Kimtiririko bara la Afrika limebakia kuwa ni klabu zisizokuwa na tija yoyote ya maana, ndiyo maana AU imekuwa ni mwangalizi tu na imeendelea kufanya hivyo wakati viongozi wengi wa bara hili wanafanya mambo ya ajabu, wengine wakiwachinja raia wao. AU haina nguvu yoyote sana sana ni kuhalalisha tu maovu barani humo kwa kuendelea kutambua wauaji na kukaa nao vikao kwa pamoja.

Tukirejea kwa Gaddafi kuna kila sababu ya kujiuliza maswali magumu ili kujipa fursa ya kusema kwamba Tanzania ilipaswa kumsikitikia au la; Gaddafi ni kiongozi mwenye mikono yenye damu; damu ya wananchi wake, damu ya wana wa Afrika wengine, na damu ya raia wengine wa nchi za Ulaya na Marekani.

Gaddafi amesaidia sana mapinduzi mengi barani Afrika, alitumia vibaya nguvu zake za fedha, kutokana na utajiri wa mafuta kusaidia kuondolewa madarakani kwa viongozi wengi wa bara hili. Matatizo makubwa ya nchi kama Chad, Uganda na Niger, katika mfululizo wa umwagaji damu na kupinduliwa kwa tawala ni kazi ya kichwa, mikono na fedha za Gaddafi.

Pamoja na Tanzania kupokea misaada ya Libya, mingi ikiwa ni ujenzi taasisi za kidini, Gaddafi ana damu mikononi mwake kwa mauaji ya vita ya Kagera ya mwaka 1978-79 ambayo ilisababishwa na Nduli Iddi Amini. Ni vigumu sana msemakweli na muungwana kuona lolote la maana la kumfikiria Gaddafi kama mtu anayestahili kuliliwa na taifa hili.

Kama nilivyosema awali, kwamba kila binadamu hupamba kaburi lake mwenyewe, lakini wengine hujipangia mazingira ya vifo vyao, kwa Gaddafi alichagua na kupanga vyote. Ni dhahiri hasira ya raia wa Libya dhidi ya kiongozi wao ambaye alikaa madarakani kwa miaka 42 akiwa ameanza kushika dola akiwa na umri wa miaka 27 tu, ilitengenezwa na Gaddafi mwenyewe.

Alitengeneza mwisho wake mbaya kwanza kwa kuwageuza wananchi wenzake mali yake, kuendesha mauaji ya ovyo na ya kutisha dhidi yeyote aliyefungua mdomo kumpinga, hadharani au sirini. Aliua bila huruma. Aliua watu wake. Alijenga maadui na uasi ndani ya roho za Walibya kwa miaka mingi.

Si jambo la kawaida wananchi kumshambulia kiongozi wao mkuu kama kibaka wa mtaani, ni kielelezo cha kuchokwa, kupaniwa na kisasi cha hali ya juu. Mwenye kutengeneza hali yote hiyo, ni kiongozi mhusika. Katika hali ya kawaida, ni vigumu kudhani kwamba Tanzania kama taifa linatenda lolote jema machoni mwa Walibya, wapenda amani, wapenda haki, hata pale hoja za kumtetea Gaddafi zinapokuwa ni nyepesi kiasi hiki ikilinganishwa na ushenzi aliofanyia dunia hii.

Tunajua kuwa Gaddafi alikuwa anamwaga fedha kwa viongozi wengi wa Afrika; bajeti ya AU kwa kiwango kikubwa ilikuwa inamtegemea sana yeye; wengi walimgeua mgodi, ATM. Kuondoka kwake vilio tunavyoona si dhidi yake kama binadamu bali kilio dhidi ya fedha ambazo hazitapatikana tena. Hiki ni kilio na maombolezo ya fedha si ya Gaddafi.

0
Your rating: None Average: 5 (1 vote)