Wananchi ndio watabomoa ufisadi


Bashiru Ally's picture

Na Bashiru Ally - Imechapwa 28 October 2009

Printer-friendly version

NAPENDA kuchangia mjadala kuhusu suala la mpasuko katika Tanzania. Mpasuko huu unajibainisha katika sura nyingi kama vile pengo kubwa kati ya wenye kipato cha chini na wenye kipato cha juu.

Kuna mpasuko katika lugha ya kisasa. Huu unajibainisha zaidi kwa jina la umaskini. Kwa muda mrefu tumekuwa tukipambana na umaskini, ingawa umaskini unaongezeka. Mbinu za kila namna zimetumika ikiwa ni pamoja na kuweka vigezo na viwango vya umaskini.
Hivi sasa wapo maskini wakubwa na wadogo, maskini wa kike na kiume, maskini wa mjini na wa vijijini, maskini mwenye njaa na masikini wa kipato, maskini anayeishi katika mazingira hatarishi na kadhalika.
Mifuko ya uwezeshaji imeanzishwa, taasisi za fedha za kukopesha maskini zimeanzishwa, mafunzo ya ujasiriamali yameendeshwa hadi vyuo vikuu. Yote haya hayajapunguza kiwango cha umaskini
Katika kutafuta majibu ya kwanini umaskini nchini unaongezeka ingawa vita dhidi ya tatizo hili inapamba moto, ufisadi ikaonekana kuwa ndio chanzo kikuu.
Wakajitokeza wananchi kutoka kada mbalimbali kupambana na ufisadi. Kadri mapambano hayo yanavyozidi kupamba moto, ndivyo ufisadi, kama ulivyo umaskini, unavyoongezeka.
Tatizo hapa ni kwamba vita dhidi ya ufisadi havilengi kukabiliana na vyanzo vikuu vya ufisadi pamoja na vikwazo vya mapambano ya ufisadi. Hata mapambano ya umaskini nayo yanakabiliwa na tatizo hilohilo.
Hakuna mkakati wa kuwaunganisha wananchi ambao ni waathirika wa umaskini na ufisadi ili washiriki katika mapambano dhidi ya maadui wa maendeleo yao. Mikakati iliyopo inawagawa zaidi na kuwakatisha tamaa.
Bila ushiriki wa wananchi wengi, ushindi dhidi ya umaskini na ufisadi hautapatikana.
Ni vyema tukatambua kuwa matatizo ya umaskini na ufisadi ni dalili ya ukosefu wa mfumo mbadala wa kisiasa na kiuchumi. Hili si tatizo la Tanzania peke yake bali la nchi zote za Dunia ya Tatu.
Kwa hiyo mapambano dhidi ya mfumo huu yanapaswa kuwa na sura ya kisiasa katika ngazi ya kitaifa na kimataifa. Ingefaa sana tukapanua mjadala wetu na kuupa sura ya kisiasa ambayo itayasambaza mapambano haya nchi nzima na pia kuyaunganisha na mapambano yanayoendelea kwingineko.
Hivi ndivyo mifumo ya ukoloni na ukaburu ilivyosambaratishwa. Kila mtu bila kujali dini, rangi, jinsia, tabaka au kabila alishiriki kupambana na ukoloni na ukaburu. Ikiwa tutashindwa kufanya hivyo, muda sio mrefu mapambano haya yatakuwa na sura ya ukabila na udini.
Inahitajika mikakati. Kwanza, kuendeleza mijadala kuhusu mbinu muafaka za kujenga mshikamano miongoni mwa wananchi kitaifa na kimataifa na kuieneza mijadala hiyo kadri iwezekanavyo.
Pili, kuunda vikundi huru vya kiraia vyenye malengo ya kisiasa ya kupambana na mifumo ya kifisadi popote ulipo.
Vikundi hivi vipambane dhidi ya wizi wa kimataifa wa raslimali zetu, kama ardhi na madini; ufisadi wa kidini unaofanya huduma za kiroho na kijamii kuwa biashara; ufisadi wa makuadi wa soko huria, unyanyasaji wa wanawake na watoto; wizi wa kura, uroho wa madaraka, rushwa, udini, ukabila, na ufisadi wa kisomi unaowakilishwa na woga na unafiki.
Ili tuweze kufika huko, uongozi wa kisiasa, kisomi, kidini na kijamii utahitajika. Hata hivyo mshikamano wa wananchi ndio utakaotuwezesha kupata uongozi mzuri. Hata mjadala juu ya viongozi bora sharti uwe mpana na wazi zaidi.

0
No votes yet