Wananchi wamechoka kuvumilia


Eligius Mulokozi's picture

Na Eligius Mulokozi - Imechapwa 05 August 2008

Printer-friendly version

HIVI karibuni Rais Kikwete, akiwa katika ziara ya mkoa wa Tanga alisema, "Maisha ni magumu; Watanzania waendelee kuvumilia."

Kwa kauli hiyo tu, inatosha kututafakarisha kuwa ahadi ya maisha bora kwa kila Mtanzania aliyoitoa wakati wa kuomba kura, haiwezi kutekelezwa wala kufanikiwa.

Kauli hii ni mwiba mkali kwa Watanzania. Ni kauli ya kukatisha tamaa hasa kwa wananchi wa kawaida wanaoshindwa kupata hata mlo mmoja kwa siku.

Sasa maisha bora ni njozi. Lakini kwa upande mwingine, hata rais mwenyewe ameanza kukata tama; kwani kile alichoahidi kwa kuamini kwamba kinawezekana, kumbe kimemshinda. Hivyo anawataka wananchi waendelee "kuvumilia" ugumu wa maisha.

Anataka wananchi wanaoshinda njaa waendelee kuvumilia njaa yao. Mjamzito aliyejifungulia sakafuni aendelee kuvumilia pia. Rais Kikwete anaujua ukweli kwamba Watanzania wana maisha magumu. Ndiyo maana aliahidi kuwaletea maisha bora.

Kauli yake ya kuleta maisha bora ilileta matumaini kwa waliokata tama lakini kwa kauli yake ya sasa, Kikwete ameonyesha dhahiri kuwa bado hajapata suluhu ya ugumu wa misha yanayowakabili wananchi wake.

Tatizo hapa ni kwamba rais hakusema wananchi wavumilie hadi lini. Hajasema washinde njaa mpaka lini. Waendelee kujifungulia sakafuni mpaka lini. Haya hajasema. Badala yake amesema, "Maisha magumu, wananchi waendelee kuvumilia."

Rais anajua kuwa wananchi tayari wamevumilia kwa kujifunga mikanda mpaka tundu la mwisho. Lakini hawajaona mabadiliko. Badala yake, wanaishia kulishwa maneno matamu na watawala.

Sina shaka rais anajua ni watu wa aina gani anawaambia waendelee kuvumilia. Hawa ni Watanzania wa kawaida na ambao ni wengi. Wasaidizi wake hawamo katika kundi hili. Hii ndiyo maana wakati yeye anasema ?maisha ni magumu,? wasaidizi wake wanaendelea kutanua.

Ongezeko la mishahara halisaidii, maana nyongeza yote inaishia kulipia nauli au kugharimia bidhaa au huduma ambazo zimepanda kutokana na gharama za mafuta. Hii maana yake ni kwamba serikali inatoa kwa mkono wa kulia na kuchukua au kushirikiana na wengine kuchukua kwa mkono wa kushoto.

Kwa utajiri wa madini, ardhi na raslimali nyingine, uliomo nchini humu, ni aibu kwa taifa hili kulia na kusaga meno; lakini pia ni kashfa kwa watawala kuwaambia wananchi kwamba wavumilie hali mbaya ya uchumi.

Nani anakula madini ya Tanzanite? Nani anachota dhahabu, almasi na madini mengine hadi kuzoa hata mchanga? Nani anavuma misitu na wanyama wetu? Nani anachukua mapande makubwa ya ardhi kwa uwekezaji na hailipi serikali?

Nani hasa anafukarisha taifa hili na kumomonyoa akili za watawala kiasi cha kuwafanya wawe butu kwa maisha na matakwa ya wananchi na kufikia hatua ya kuwaambia wananchi kuwa wavumilie matatizo?

Ni wazi kwamba wananchi wanakufa kwa umasikini huku rasilimali zao zinazoporwa na wale waliowapa madaraka na vibaraka wao. Na wakati hayo yakifanyika, wananchi wanaendelea kuwa wageni ndani ya nchi yao.

Tatizo lililotufikisha kwenye kuvumilia ugumu wa maisha ni ugawanyaji mbovu wa rasilimali za nchi. Wananchi wangekuwa radhi kuvumilia kama wangeona jitihada za kurejesha fedha za EPA na harakati za kuwafikisha wezi mahakamani. Badala yake wanapozwa na ahadi tamu zisizotekelezeka.

Mwaka 2009 vuguvugu la uchaguzi mkuu linaanza kwa kuanzia na chaguzi za Serikali za Mitaa. Sijaona mikakati ya kuboresha maisha ya wananchi. Badala yake tunaona uimarishaji wa ununuzi wa kura wakati wa uchaguzi.

Na hili linathibitishwa na ugoigoi katika utekelezaji wa ahadi za rais kwa wananchi.

Ni bora rais ajue kwamba wananchi wameshavumilia vya kutosha. Wameshachoshwa na kauli zake kwamba na wenzake kwamba "uchumi unakua, bajeti ni finyu, ndege ya uchumi inapaa, tufunge mikanda, tuendelee kuvumilia."

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: