Wananchi wanalia, rais analia


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 09 March 2011

Printer-friendly version
Tuseme Ukweli

KATIKA hotuba yake ya mwisho wa mwezi wa Februari 2011, Rais Jakaya Kikwete alikiri kwamba hali ya maisha ni ngumu. Akajitetea, hata wakati wa uongozi wa Mwalimu Julius Nyerere maisha yalikuwa magumu pia.

Kwa kauli yake alisema, "Hayo si matatizo ya kumalisika ndani ya siku tisa. Mzee Nyerere aliongoza kwa miaka 23 na hakuyamaliza matatizo ya maendeleo ya nchi hii. Na wale wa umri wangu au kunizidi wanakumbuka hali ilivyokuwa wakati anang'atuka. Hakuacha nchi ikiwa tajiri.

"Mzee Mwinyi kakaa miaka 10 hakuyamaliza, mzee Mkapa pia amekaa miaka 10 na hakuyamaliza. Mie nimekaa miaka mitano hayakwisha na nitamaliza mitano mingine hayataisha yote. Lililo muhimu kuliko yote ni kuwa katika kila awamu nchi yetu imekuwa inapiga hatua ya kusonga mbele katika kujiletea maendeleo.

"Hali iliyokuwa wakati ule sivyo ilivyokuwa mwaka 1985, wala 1995 au 2005 na ilivyo sasa. Katika miaka mitano hii kuna maendeleo yanayoonekana."

Kauli hii ni uthibitisho kuwa Rais Kikwete wa sasa ni tofauti na Jakaya Kikwete aliyekuwa anaomba kipindi kingine cha miaka mitano ya uongozi.

Kikwete aliyekuwa anaomba urais kipindi kingine cha miaka mitano aliwatumainisha watu kukabili na kumaliza matatizo kwa ari zaidi, nguvu zaidi na kasi zaidi.

Baada ya siku 100 na ushee madarakani, Kikwete amesalimu amri, analalama ni kweli maisha magumu na haonyeshi ufumbuzi wa kuyatatua isipokuwa kuegemeza utetezi kwa waliomtangulia.

Wananchi wanalalamika, vyama vya siasa – Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Chama cha Wananchi (CUF), NCCR-Mageuzi vinalalamika na rais Kikwete analalamika? Ajabu! Nani atayatatua?

Hata kabla ya Mwalimu Nyerere kung'atuka madarakani, hali ya maisha ilianza kuwa ngumu na wananchi walianza “kumpasha” kuhusu ugumu huo. Salamu ya Kidumu Chama Cha Mapinduzi' ambayo ilikuwa inaitikiwa na wananchi wote 'Kidumuuuuuu' ilianza kuitikiwa kwa kejeli 'Kigumuuuuuuu.’

Kiitikio hicho mbadala ulikuwa ujumbe tosha kwamba sera za uchumi za Chama Cha Mapinduzi (CCM) haziwezi kuwaondoa kwenye lindi la umaskini.

Huo ulikuwa uthibitisho usio na shaka mbele yake kwamba, wananchi walihitaji mwelekeo mpya wenye matumaini mapya. Kwa bahati mbaya hakukuwa na chama mbadala maana mfumo wa vyama vingi vya siasa uliondolewa mwaka 1962 badala yake ukakumbatiwa mfumo wa chama kimoja.

Jambo moja lililowazi na ambalo rais Kikwete inabidi alisema pia, pamoja na hali ngumu ya maisha, wananchi walimpenda Nyerere kwa vile alikuwa mkweli na walifurahia umoja, upendo na mshikamano wa dini na makabila alioujenga.

Uthibitisho wa wazi ni kwamba alipong'atuka madarakani hakuondoka na mgodi wa Kiwira, hakuchota fedha za EPA, hakuwa na hisa katika makampuni ya kibepari ya ndani na nje, wala hakujilimbikizia mali.

Nyumba moja alijengewa na CCM na nyingine kubwa ya kisasa alijengewa na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWT) na wananchi walimzawadia vitu mbalimbali.

Sababu kubwa ya kuvurugika uchumi wa nchi katika miaka ya mwanzoni mwa 1980 ni vita ambayo nchi iliingia dhidi ya Iddi Amini wa Uganda.

Nchi wafadhili na mashirika ya fedha kama vile Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) yalitoa mapendekezo kadhaa namna ya kuchepua uchumi uliooharibika. Masharti aliyopewa Mwalimu Nyerere yalikuwa shubiri kwa msimamo wake wa kukataa kupunguza thamani ya shilingi.

Ni kweli hali ilikuwa tete, bidhaa zilikosekana madukani na hizo chache zilifichwa ili ziuzwe kwa bei ya juu.

Hicho ndiyo kipindi waliibuka walanguzi na wahujumu uchumi. Hicho ndiyo kipindi ilitungwa sheria ya kupambana na wahujumu uchumi na kamanda wake Waziri Mkuu Edward Sokoinne aliisimamia kikamilifua.

Wahujumu uchumi sawa na mafisadi leo walisakwa usiku na mchana, walitangazwa wazi kwenye vyombo vya habari, walishtakiwa na mali zao zikataifishwa.

Hicho ndiyo kipindi kulikuwa na foleni ndefu kwa ajili ya kununua bidhaa muhimu na adimu – sukari, chumvi na nguo. Dawa ya mateso hayo, wafadhili walimwambia Mwalimu Nyerere ni kupunguza thamani ya shilingi lakini alikataa. Kwa sababu ya umbumbumbu wa wananchi, waliandamana kumpongeza rais wao anavyoipeleka nchi kwenye shimo la uchumi.

Tatizo lililokuwepo wakati ule ndani ya CCM na serikali ni woga. Baadhi ya viongozi walikuwa hodari kuzungumzia matatizo hayo nje na siyo kwenye vikao; walimpamba na kumsifu Nyerere lakini walilalamika walipokuwa nje. Viongozi wa aina hii ndio wanaomzunguka Kikwete leo.

Kiongozi pekee aliyetofautiana na Mwalimu Nyerere na akaonyesha msimamo wake wa kukubali masharti ya wafadhili, japo kwa wakati ule, alikuwa Waziri wa Fedha na  Mipango ya Maendeleo, Edwin Mtei; akajiuzulu wadhifa wake kwa kuwa rais wake alikuwa haambiliki. Miezi michache baada ya Mtei kujiuzulu, shilingi ilishushwa thamani.
   
Kwa hiyo, Rais Kikwete aliposema Mzee Nyerere, Mwinyi, Mkapa hawakumaliza matatizo ya kimaendeleo ni kweli, lakini tofauti na Mwinyi na Mkapa, rais Kikwete hakurithishwa nchi masikini. Alikuta fedha kibao na deni la taifa likiwa limepunguzwa sana.

Kilichoshuhudiwa ni Kikwete kupiga kiguu na njia nchi za nje kwa madai ya kujitambulisha, kutafuta kocha mkuu wa Taifa Stars, kutafuta makabaila wa kuwapa vipande vya ardhi kwa kisingizio cha uwekezaji katika kilimo na madini.

Rais Kikwete hawezi kujilinganisha na Mwalimu Nyerere ambaye wahujumu walishughulikiwa ipasavyo, ilhali sasa serikali ya CCM inapigishwa magoti na mafisadi. Wala Kikwete hawezi kujilinganisha na Nyerere ambaye aliwashughulikia wala rushwa serikalini wakashtakiwa na kufungwa, wakati serikali yake sasa imewapa madaraka makubwa walarushwa na mafisadi ndani ya chama na serikali.

Vilevile Rais Kikwete hawezi kujilinganisha na Mwalimu aliyehubiri amani, upendo na mshikamano wa makabila na dini zote wakati huu utengano wa dini umehubiriwa ili upatikane ushindi

Mfumo wa huduma ya afya kwa asilimia kubwa ni ulioachwa na Mwalimu Nyerere kwani zilizojengwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita hazina wahudumu wala dawa.

Katika elimu Rais Kikwete ameweka rekodi ambayo haitasahaulika muda mrefu kwa hatua yake ya kujenga shule holela na kuzifungua zikiwa hazina vifaa, vitabu wala walimu. Matokeo yake, asilimia 88 ya wahitimu wamefeli.
 
Umaarufu

Haya ndiyo yanauweka shakani umaarufu wa Rais Kikwete na hata CCM wanajua. Mwaka 2005 alishinda kwa asilimia 82, lakini mwaka jana hakufikisha hata idadi ya wana CCM ambao ni mtaji wa chama. Kwa hiyo, hakupigiwa na wanachama wake wengi na alikosa kura za mashabiki akaishia asilimia 61.

Kilichoporomosha umaarufu wake ndicho kimewapa umaarufu CHADEMA – vita dhidi ya rushwa na ufisadi. Jaribio lolote la CCM au serikali ya CCM kuwatwanga virungu CHADEMA kwa madai eti kuna njama za kuangusha serikali, zitakuwa juhudi nyingine za kuidhoofisha serikali na kupaisha bure umaarufu wa CHADEMA. Tunasubiiri.

0753 626 751
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: