Wananchi washtukia usombaji makaa ya mawe


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 16 March 2011

Printer-friendly version

"TUNAONA wanasomba kwa malori; wanapeleka bandari ya Ndumbi kwenye Ziwa Nyasa. Hatujui kinachoendelea."

Hiyo ni kauli ya mwalimu mstaafu, Martin Zamtanga wa kijiji cha Liyombo, tarafa ya Namsweya, kata ya Ruanda, wilayani Mbinga katika mkoa wa Ruvuma.

Ni kuhusiana na mkaa wa mawe kutoka “Machimbo ya Mkaa ya Ngaka,” wilayani Mbinga ambako unachukuliwa mkaa “kwa ajili ya uchunguzi iwapo unafaa kwa matumizi viwandani.”

Kampuni ya TANCOAL Limited ndiyo inafanya uchunguzi wa mkaa wa mawe katika kata ya Ruanda ambako vijiji vipatavyo sita vinatajwa kuwa juu ya mkaa wa mawe.

Mwalimu Zamtanga anasema, “Kwa zaidi ya miezi miwili mfululizo, tumeshuhudia tani na tani za mkaa wa mawe zikipitishwa na mzungu katika malori ya tani saba na kupelekwa bandari ya Ndumbi, tayari  kusafirishwa nje ya nchi."

Hata katika vijiji vya Ngaka, Mbalawala na Mburuya, vilivyo eneo la machimbo, mjadala ni juu ya mkaa wa mawe “unavyosafirishwa nchi za nje” bila wananchi kushirikishwa wala kunufaika na lolote.

Wasiwasi mkubwa wa wananchi katika vijiji hivi na vingine, unatokana na taarifa kuwa vijiji vyao viko juu ya mwamba wa mkaa wa mawe ambao uchimbaji wake unatarajiwa kuanza Mei mwaka huu.

Kama kutakuwa na uchimbaji mkaa, basi kutakuwa na uhamishaji wananchi wengi kutoka eneo hili. Kama kutakuwa na uhamishaji, basi sharti kuwe na fidia kwa wote watakaohamishwa.

Bali hadi sasa hakuna hata tetesi juu ya ulipaji fidia; lakini wananchi wanaona mzungu akisimamia usombaji mkaa wa mawe hadi bandari ya Ziwa Nyasa.

Wananchi wanaona mzungu ndiye anasimamia zoezi zima la usafirishaji wa mkaa wa mawe – upandishaji na ushushaji mkaa katika bandari ya Ndumbi.

“Tunahisi tunaibiwa. Hata meli inayopakia mkaa tumeona ina bendera mbili – ya Malawi na Tanzania – lakini katika muda wote wa upakiaji hakukuwa na viongozi wa serikali, maafisa madini wala viongozi wa wilaya,” ameeleza mkulima Josephat Kwembe.

Kinacholeta woga mkubwa ni kwamba kama tangu hatua za awali, wazungu ndio wanaendesha ubabe, basi wananchi wasubiri ubabe mkubwa zaidi wakati wa kuwahamisha na kutowalipa fidia pindi uchimbaji mkubwa ukianza.

Yaweza kuwa hadithi ileile ya kila palipo na madini nchini: wananchi huswekwa, ama kwa ushawishi au kwa mabavu kwa matumizi ya polisi na kuondoshwa eneo lenye utajiri.

Mgodi wa Ngaka umekadiriwa kuwa na zaidi ya tani 400 milioni za mkaa wa mawe. Kiasi hicho, kwa mujibu wa wataalam, kinaweza kuchimbwa kwa kipindi cha zaidi ya miaka 100.

Aidha, wananchi wanadai tayari mazingira ya kihasama yameanza kuonekana kati ya wananchi na watakaochimba mkaa. Hiki ndicho wanaita “utumwa mpya” hata kabla mgodi haujaanza rasmi.

Hilo linahusishwa na vijana ambao wamekuwa wakipakia na kupakua magunia yaliyojaa mkaa wa mawe kulipwa Sh. 100 kwa kupakia gunia moja na kiasi hichohicho kwa kupakua.

Naye Bw. Gordon McCormack, meneja anayesimamia uchimbaji wa mkaa wa “sampuli,” anasema tayari amesambaza tani 1,000 za mkaa wa mawe kwa wadau mbalimbali na kwamba mkaa huo umekubalika.

Afisa Madini Mkoa wa Ruvuma, Stanslaus Mutalemwa amesema mkaa wa mawe uliosafirishwa umepelekwa Afrika Kusini na katika viwanda vya kutengeneza saruji vya Mbeya Cement na Tanga Cement.

Hata hivyo, Mutalemwa anakiri kutojua meli iliyokuwa ikisomba tani 1,000 za mkaa wa mawe kutoka bandari ya Ziwa Nyasa.

Tancoal Limited ni kampuni iliyoanzishwa tarehe 3 Aprili 2008. Ni ubia wa Shirila la Taifa la Maendeleo (NDC) lenye asilimia 30 ya hisa na kampuni ya Pacific ya Afrika Mashariki (PCEA) inayomiliki asilimia 70 za hisa.

Meneja Mkuu wa Tancoal Limited, Bw. Emmanuel Constantinides amesema ujenzi wa mgodi utaanza “hivi karibuni na unatarajia kukamilika ndani ya kipindi cha mwaka mmoja.”

0
No votes yet