Wanaoisaidia CCM hutupwa kama ‘katapila’


John Kibaso's picture

Na John Kibaso - Imechapwa 01 December 2010

Printer-friendly version
Jamvi la Weledi
John Samweli Malecela

UJASIRI wa kisiasa uliowahi kuonyeshwa na aliyekuwa Makamu mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), John Samweli Malecela ni pale alipowaambia viongozi wenzake waandamizi kuwa wanamtumia kama katapila.

Katapila ni gari kubwa linalotumika kutengeneza barabara; kuchonga, kuangusha miti mikubwa kama mibuyu, kubeba au kusukuma kando mawe na kukandamiza kokoto na udongo ushikane.

Mwisho wa siku barabara ikikamilika, katapila hupigwa marufuku kupita katika barabara nzuri iliyolitengenezwa, lakini magari madogo ambayo hayakuhusika katika utengenezaji wake ndiyo huachwa yatumie.

Kwa muundo wake, katapila kupita popote. Lakini kwa vile hutumia mnyororo kama matairi, baada ya barabara kutengenezwa, haliruhusiwi tena kupita. Hata yale yanayotumia matairi makubwa bubebwa kwenye magari maalum.

Malecella alitumia mfano huo, baada ya kukaa na kutafakari kwa kina mchango wake katika chama chake na mtazamo walionao viongozi waandamizi kwake.

Ajifananisha na katapila

Malecela ni miongoni mwa viongozi waliowahi kushika nafasi mbalimbali za kichama na serikali. Amewahi kuwa waziri mkuu na baadaye makamu mwenyekiti wa CCM upande wa Tanzania Bara.

Amekuwa akitumika katika shughuli nyingi ndani ya chama na serikali na wakati wa chaguzi ndogo ambazo huitishwa baada ya mbunge kufariki dunia au matokeo kutenguliwa na mahakama. Malecela amekuwa akihakikisha unapatikana ushindi wa kishindo.

Lakini pale anapogusa ‘mahali patakatifu’ yaani pale akiomba kupitishwa na chama chake kuwania urais, maombi yake yamekuwa yakipokewa kwa hisia tofauti.

Kwa mara ya kwanza, maombi ya kuwania urais ya Malecela yalikumbwa na kizingiti mwaka 1995 kwa ushawishi wa Mwalimu Julius Nyerere kupitia kitabu chake cha ‘Uongozi wetu na hatima ya Tanzania’. Jina lake lilikatwa na Kamati Kuu ya CCM.

Mwalimu Nyerere hakufurahishwa na kile alichoita kumshauri vibaya Rais Ali Hassan Mwinyi katika sakata la wabunge wa CCM kutaka kupitisha azimio la kufanyiwa marekebisho Katiba ya Jamhuri ili kuwe na mfumo wa Muungano wa Shirikisho badala ya huu wa sasa.

Katika sakata hilo ambalo vinara wake walikuwa Mbunge wa Lupa, Njelu Kasaka na Mbunge wa Mbulu, Phillipo Marmo, lengo lilikuwa Tanzania Bara iwe na serikali yake baadala ya kuongozwa na serikali ya Muungano.

Malecela alidhani kuwa baada ya Mwalimu Nyerere kufariki dunia Oktoba 14, 1999 kizingiti cha urais kilikuwa kimeisha. Lakini alipojitokeza tena mwaka 2005, alikumbana na mzimu uleule wa kukatwa jina lake.

Hapo ndipo Malecela alipoamua ‘kuwatolea uvivu’ viongozi wa chama hicho akisema wanamtumia kama katapila.

Matamshi haya mazito yalilenga kupeleka ujumbe kwa viongozi waandamizi wa CCM kwamba, wanamtumia sana katika kupata ushindi kwenye majimbo magumu, lakini inapofika wakati wake yeye kuomba nafasi ya kuongoza serikali anakataliwa.

Sababu kubwa eti ni ile ile ya kuruhusu mjadala wa Muungano bungeni wakati alipokuwa waziri mkuu.

Kauli ile ya Malecela ndiyo imenisukuma kuandika mada hii ya leo. Hapana ubishi kilio cha Malecela kilikuwa na ukweli ndani yake.

Kimsingi hakuna binadamu aliyekamilika katika kutekeleza majukumu yake.
Kwa nini Malecela aendelee kushikiwa bango eti aliwahi kukataliwa na Mwalimu Nyerere hivyo ni sababu ya kukata jina lake kila mara chaguzi za kuwania nafasi ya urais zinapowadia?

Wangapi ndani ya CCM, waliwahi kufanya madudu ya kuchukiza lakini wakaendelea kudunda na vyeo vikubwa katika serikali ya chama tawala cha CCM?

Haya yaliyomkuta Malecela yameendelea kuwakuta makada wengi, wazuri wa CCM pindi chaguzi zinapokamilika. Kama ilivyoada, kinapofika kipindi cha uchaguzi, CCM inawatafuta makada wazuri wa kukipigia debe katika nyanja zote nyeti na muhimu, lakini kiwewe kinawapata hao makada pale chaguzi hizo zinapomalizika.

Bila kuathiri utaratibu uliowekwa na CCM ya jinsi gani chama kinateua makada wake kuwa viongozi ndani ya chama au Serikali, na pia bila kuonyesha upendeleo wowote kwa baadhi ya makada, ukweli CCM inakawaida ya kuwatupa makada wake walioonyesha umakini na uhodari katika kukisaidia chama kupata ushindi.

Mathalani katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, CCM ilitumia makada kadhaa waliotumia kalamu zao kusaidia kupunguza kasi ya wapinzani wao Chama cha Demokrasi na Maendeleo (CHADEMA). Hao waliandika habari na makala za ushauri lakini mwisho wa siku wanabaki ‘makatapila ya CCM.’

Si hivyo tu, mara baada ya CCM kupata ushindi, kila kiongozi huwa anakuwa na kawaida ya kubeba mkoba uliosheheni majina ya washirika wake; wajomba, wajukuu, mashemeji, kaka na madada kumpelekea Mwenyekiti wa CCM aweze kuwateua katika nyadhifa ambazo Rais amepewa kwa mujibu wa Katiba.

Hawa makatapila wa CCM, wasio na viongozi waandamizi wa kuwapigania ndani ya chama watabaki wakipiga miayo wakiwabebea mikoba wateule kwenda kwenye semina na ziara za nje.

Hili ni tatizo kubwa ndani ya CCM na ambalo ingefaa mwenyekiti Jakaya Kikwete alitupie macho. Ikiwezekana aunde Tume kuchunguza viongozi waliopo kuanzia ngazi za wilaya na mikoa ambao ni wale wa kuteuliwa kwa Mujibu wa Katiba.

Tume ianze kwa kuwahoji makatibu wa kata kote nchini. Kuna Makatibu ambao wamekaa kwenye nafasi hizo kwa muda mrefu na hakika wana uwezo mkubwa, lakini unapofika kwenye uteuzi wa makatibu wa wilaya wao wanabaki kuwa makatapila wa CCM.

Hali hii inatokana na utamaduni uliojengeka wa kuwapokea na kuwateua mamluki kwenye nafasi nyeti za CCM.

Jambo hili limeleta simanzi na manung’uniko makubwa ndani ya CCM kwa makatibu wa ngazi ya chini ambao wanahisi kuthaminiwa tu wakati wa uchaguzi lakini uchaguzi ukikamilika wanabaki kuwa makatapila wa CCM.

<p> Mwandishi wa makala haya ni kada wa CCM na anapatikana kwa simu 0713399004</p>
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: