Wanaompigia Kikwete kampeni, wanaogopa nini?


M. M. Mwanakijiji's picture

Na M. M. Mwanakijiji - Imechapwa 14 April 2009

Printer-friendly version

KUNA kundi la watu woga ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Kundi la wasiojiamini na wasioamini kuwa Rais Jakaya Kikwete anaweza kuchagulika tena 2010.

Sasa kundi hili limeanza kuonesha dalili ya kutetemeka na kama wapambe wanaoogopa kupoteza ujiko wao, limeanza kujitokeza na kuimba wimbo wa “Kikwete mgombea tena 2010 ndani ya CCM.”

Hivi hawa wanaogopa nini? Je, kwa kujitokeza kwao kusema ‘chaguo lao ni Kikwete’ kunamsaidia Kikwete au kunaonesha udhaifu wake uliopo kuelekea 2010?

Inaonekana wanatambua kitu ambacho wengine hatukitambui; yaani, ndani ya CCM kuna mtu zaidi ya Kikwete ambaye anatamani kugombea urais mwakani.

Mtu huyo nina uhakika si John Shibuda kwani Shibuda alifanya hivyo hata mwaka 2005 na sidhani kama anawatisha hivyo. Kitendo cha mtu aliyekuwa Waziri Mkuu, kitendo cha mtu aliyewahi kuwa Spika na jumuiya mbalimbali za CCM mikoani kuanza kujitokeza na kusema Kikwete ndiye atakuwa mgombea wao, ni dokezo kuwa kuna mtu mwingine ndani ya CCM anataka kuwania nafasi hiyo.

Mtu huyo ni nani? Ana ubavu gani wa kushindana na mtu aliyeshinda nafasi ya urais kwa asilimia 80 ya wapiga kura?

Kama kuna mtu huyo ndani ya CCM basi ina maana ya kuwa mwaka 2005 Watanzania walifanya makosa kumchagua Kikwete. Kwa sababu kama kuna mtu ambaye anaweza kumshinda Kikwete leo hii ina maana mtu huyo tulikuwa naye 2005 na hatukumpa nafasi.

Jinsi ambavyo watetezi wa uteuzi wa Kikwete wanavyozungumza ni kana kwamba wako tayari kuendelea na makosa yaleyale 2010 bila kuyasahihisha hata kama wakipewa nafasi hiyo.

Woga hawa wanaamini kuwa ni bora kuendelea na kosa lao kuliko kulisahihisha na hivyo wao hawajali jingine lolote isipokuwa hawako tayari kumuona mtu mwingine yoyote akigombea nafasi ya urais zaidi ya Kikwete.

Sasa kama wananchi leo wamegundua kuwa walifanya makosa na wanataka kuyasahihisha, hawa woga wa CCM wanataka kuwanyima wananchi nafasi ya kubadilisha uamuzi wao kwa njia ya kura?

Mwaka 2005 Kikwete hakuwa na rekodi ya kuonesha uongozi wake na kama ingekuwa katika nchi nyingine kuna mambo ambayo angetakiwa kutolea maelezo, ndio maana walimkwepesha kufanya midahalo na wagombea wengine ili watu wampime.

Kulikuwa na masuala ya IPTL na tuhuma za kupokea fedha toka Iran na Oman. Bahati mbaya waandishi na wana CCM wengi walikuwa wamepigwa ganzi ya mapenzi kiasi kwamba hakuna aliyethubutu kumhoji maswali magumu na hivyo tukampitisha kwa kuangalia vile ambavyo si vya msingi.

Sasa hata hivyo, ana rekodi ambayo yeye mwenyewe anaweza kuisimamia. Watetezi hawa wa Kikwete wanatuambia kuwa anaongoza mapambano ya ufisadi wakitolea mfano wa kesi uchwara zilizofikishwa mahakamani (ndiyo nimesema uchwara).

Hawa wanataka tumaini kuwa watu kufikishwa mahakamani (tusiangalie mashtaka yenyewe ni yapi), basi mapambano dhidi ya ufisadi yanaendelea chini ya Kikwete.

Lakini rekodi yake sasa ni kubwa zaidi na ambayo mwana-CCM yeyote anayo haki ya kuipa changamoto, kuihoji na kumpa nafasi Rais Kikwete kuitetea.

Je, Kikwete anahusika vipi katika kuwaleta Dowans? Je, alihusika vipi katika suala la Richmond pale ambapo baadhi ya watumishi walipotaka mkataba huo usitishwe?

Je, alihusika vipi na kuwaacha watoto wa Kitanzania wasote ugenini na kupigwa baridi kwa kitu kimoja cha kuomba elimu na kuwalazimisha kuwarudisha kwa aibu na kwa nguvu toka Ukraine? Kwanini hadi leo serikali yake haijaomba radhi kwa hilo?

Rekodi yake ipo na ninaamini hawa woga walioibuka siku hizi wanajua hawezi kuitetea. Lakini uzuri ni kuwa kwa kumpambanisha na mwana-CCM mwingine basi tunampa nafasi rais kuona makosa yake, kukiri makosa ya wazi lakini pia tunampa nafasi ya kujipanga upya.

Utamaduni mbovu ambao ndugu zetu watetezi wa Kikwete wanataka uendelezwe ni ule wa “kumwachia rais aliyeko madarakani mihula yake miwili.” Dhana hii ni potofu, ya kibabe na haina mfanano wowote na utawala wa demokrasia.

Kama hili lingekuwa zuri, CCM si ndiyo wana Bunge na wana rais, kwanini wasiamue kubadilisha Katiba na kuweka awamu ya rais kuwa ni muhula mmoja wa miaka kumi?

Urais unashindaniwa kila baada ya miaka mitano na hakuna garantii kuwa ukiwa rais basi mhula wako wa pili utapewa kwa dezo. Ni lazima Kikwete apambanishwe ndani ya CCM kama tulivyofanya 2005 na kabla yake.

Utawala wa demokrasia unatutaka tutoe nafasi sawa kwa mtu yeyote anayetaka kugombea nafasi yoyote ya uongozi. Ni kwa sababu hiyo naamini mojawapo ya mambo ambayo yafanyike mwaka huu ni pamoja na Bunge kubadilisha sheria ili kuruhusu mgombea binafsi wa nafasi yoyote ya uongozi. Mambo ya kulazimishwa kuwa mwanachama wa chama usichokubaliana nacho hayana msingi.

Hata hivyo, ndani ya CCM kama kuna watu wanaamini wanaweza kuliongoza taifa letu vizuri zaidi, kwa kuthubutu zaidi na kuliamsha kuelekea mafanikio na maendeleo ya kweli (ya watu siyo vitu), basi watu hawa wako huru kujitokeza bila kuona haya kama alivyofanya Shibuda. 

Watetezi wa Kikwete wasitumie jina la CCM kuwatisha watu wengine ambao wako ndani ya chama hicho. Kama wao wanaogopa kuwa Kikwete asipochaguliwa tena 2010 basi utakuwa ni mwisho wao na madudu yao yatajulikana, basi hayo ni matatizo yao.

Vinginevyo, kama woga hawa wanajua kuwa Kikwete hawezi kushinda akipambanishwa na mtu mwingine CCM, basi ushauri wangu ni kuwa wawatimue wale wote ambao wanaonesha nia ya kutaka kupambana na Kikwete; wawanyang’anye na uraia ili wasirudi.

Wakishafanya hivyo, waamue kufuta sheria inayoruhusu vyama vingine ili tuwe na chama kimoja chenye mgombea mmoja tu wa CCM ili taifa zima limpigie kura za  “Ndiyo” au “Hapana.”

Na kama akipata kura nyingi za Hapana, basi wamwapishe  kuwa ni rais kwani atakuwa bado amepata kura nyingi.

Vinginevyo, wamuache Rais Kikwete afanye kazi yake na akitaka kugombea mwakani agombee, akiamua kupumzika apumzike na kuwapisha wengine.

Alipotaka kugombea ilikuwa ni kwa miaka mitano, na kama kwa sababu zake zozote akiamua kutokugombea, basi asijisikie shinikizo la kugombea ili kuwaridhidha watu fulani ambao muda wao wa kisiasa umeshapita.

Vinginevyo, mwana CCM anayetaka kugombea na kushindana na Kikwete asiwaogope woga hawa mambo leo na asione haya kuonesha nia yake hiyo na wala asionekane adui. Yeyote ambaye hapendi akimbilie baharini ajitose.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: