Wanaopanga kumpinga Kikwete 2010 wamekumbuka vya kunyonga vya Mkapa


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 20 May 2008

Printer-friendly version

KUNA uvumi uliotamalaki kwamba ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), lipo kundi la watu linalojiandaa kumpinga rais wao mwaka 2010.

Kwamba sasa hawautaki ule utaratibu wa CCM ambao haujaandikwa kokote wa kumuacha rais atetee vipindi viwili vya miaka mitano kila kimoja. Sasa wanataka kumpinga katika kipindi cha pili.

Huu ni uvumi ambao umekuwako kwa muda sasa. Hakuna ushahidi wa kuthibitisha haya isipokuwa kwa kuwa ni mambo yanayosemwa si vema kuyapuuzia, yafaa tu kuupa umuhimu uvumi huu.

Katika hali ya kawaida mtu angejiuliza maswali magumu kidogo; kwamba wakati hata Rais Jakaya Kikwete hajamaliza nusu ya muda wake wa miaka mitano ya kwanza amewakosea nini wenzake hadi waanze kufikiria kumpiga?

Swali hili ni gumu kwa sababu kwa rais aliyeshinda kwa wingi wa kura kama za Kikwete, na kwa sifa alizokuwa akimwagiwa wakati wa kampeni, inakuwa ni vigumu kujua kilichotokea hadi wenzake sasa wafikiri kumpinga 2010?

Kubwa zaidi, watu wanajiuliza nini kinapeka mawazo ya watu mwaka 2010 wakati hapa katikati kuna mambo mengi tu ya kimsingi ya kujadili kuhusu maendeleo na mustakabali wa taifa hili? Sina majibu ya maswali haya yote.

Hata hivyo, tafakari ya kina inasogeza mawazo yangu kwamba uvumi huu wa watu wanaoutaka urais ndani ya CCM mwaka 2010 unachochewa na watu ambao hawafurahishwi na mwendeno wa mambo ndani ya serikali ya awamu ya nne.

Watu hawa wasiofurahishwa na mwenendo wa mambo, wanadaiwa kuwa na hasira dhidi ya Kikwete kwa sababu kuu moja.

Kwamba, amekuwa ni rais mlaini mno anayeruhusu watu kuichononoa serikali yake, kuchokonoa mawaziri wake, kuchokonoa maamuzi ya serikali kiasi cha kufanya watu waliozoea kufanya mambo watakavyo kuwa na wakati mgumu.

Watu hawa wanaompinga Kikwete wanaufananisha utawala wake na ule wa mtangulizi wake, Benjamin Mkapa. Wakati wa utawala wake, Mkapa hakuruhusu hata serikali yake kunyooshewa kidole achilia mbali kuwatikisa mawaziri wake.

Watu hawa wenye hasira na Kikwete wanasukumwa na sera mpya za uwazi za Kikwete tofauti na uwazi wa Mkapa ambao kwa hakika ulikuwa uimla na usiri usioelezeka.

Wanaotaka kumpinga Kikwete mwaka 2010 wanasumbuliwa na kitu kimoja tu, kwamba kwa nini serikali ikubali kuchukua hatua kwa kila tuhuma inayotolewa dhidi yake, wakati ingeweza tu kupuuza na kuacha mambo kama yalivyokuwa.

Ni hasira za mwizi anayehoji sababu ya mwenye mali kushtuka kwamba anaibiwa wakati mwizi anaamini ana haki ya kujichukulia tu mali ya watu atakavyo.

Kwa maana hiyo, basi kitendo cha Rais Kikwete kuruhusu Bunge kuunda tume kujadili suala la Richmond ambalo liliishia kuvunjwa kwa Baraza la Mamwaziri; kukubali ukaguzi ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kupitia Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) na hatua yake ya kuruhusu uchunguzi wa mikataba ya madini katika migodi mikubwa.

Hatua ya Kikwete kukataa kuwatetea mawaziri wake wenye kashfa na hivyo kulazimika kujiuzulu kama Edward Lowassa, Dk. Ibrahim Msabaha, Nazir Karamagi na hivi karibuni kabisa Andrew Chenge; kwa ujumla ni mambo ambayo hayawafurahishi watu waliozoea kuvuruga mambo na kutetea na Rais wao.

Ndiyo! Tunakumbuka Rais Mkapa akitetea polisi walipoua wananchi kule Pemba, 27 Januari 2001; tunakumbuka Mkapa akitetea mikataba ya ovyo kabisa ambayo viongozi wetu waliitumia kuitumbukiza nchi katika vifungo vya kiuchumi.

Kubwa zaidi, wananchi wanakumbuka jinsi Mkapa alivyokuwa na ujasiri wa kutetea maovu na maamuzi ya ovyo kabisa ya utawala wake, bali pia alithubutu kuwatukana wananchi.

Alisema kwamba ni wavivu wa kufikiri na wengine wana wivu wa kijinga pale wanapohoji ukwasi wa kupindukia na wa ghafla wa watawala wetu!

Kwa maana hiyo viongozi waliolelewa na sera na mikakati ya kibabe ya Mkapa, kauli za kuwabeza na kuwakejeli wananchi, matamshi ya kuwadhalilisha wampinzani kuwa ni wachumi na wanasiasa ucharwa; sasa wanajihisi kubanwa katika awamu hii.

Hawaoni raha tena waliyokuwa wanapata chini ya Mkapa. Viongozi hawa ndio wanaojipanga na kueneza uvumi kwamba mwaka 2010 ni lazima Kikwete apingwe.

Wanampinga Kikwete si kwa sababu wana mkakati wa ziada wa kuharakisha maendeleo ya wananchi, ila wanataka kumweka kibaraka wao ambaye atahalalisha uharamia kama ulivyowahi kuhalalishwa huko nyuma.

Hawa ni watu waliochoka, walafi na wanasukumwa na tamaa ya kurejesha Watanzania utumwani. Ingawa watu wanaokusudia kumpinga rais Kikwete mwaka 2010 wanajenga hoja kwamba serikali ya awamu ya nne imepwaya kwa sababu rais wake amekosa umakini (soften) na kwa maana hiyo kumuachia aongoze nchi mapaka 2015 ni sawa na kulitumbukiza taifa kwenye maafa, ukweli wa mambo unabakia kuwa mmoja, hawana jipya wanalokusudia kuleta isipokuwa kuendekeleza ubinafsi wao.

Ebu tufikiri kwa kina zaidi! Ni vigumu kutathmini matatizo ya Tanzania nje ya mfumo mzima wa utawala ulioasisiwa na CCM. CCM ina kila sababu ya kubebeshwa mzingo kuhusu matatizo ya nchi hii. Kama ni rushwa nchini imeletwa na CCM! Kama ni uporaji wa mali ya umma nchi hii umeletwa na CCM kama ni viongozi wazembe nchi hii CCM ni namba moja kwa viongozi wazembe, kuanzia walioko kwenye chama hadi walioko serikalini.

CCM ni muasisi wa matatizo ya taifa hili. Ndiyo maana sisi tunapowatazama watu wanaojitutumua kuutaka urais mwaka 2010 tunawaona kama watu wanaosukumwa na kitu kimoja tu, ubinafsi na tamaa ya kutaka kuendeleza ya kale. Ni watu wasiotaka mabadiliko, ni watu wasiofurahishwa na mwenendo mpya wa uwajibikaji wa kila mmoja kwa makosa yake. Ndiyo maana wanataka kumwengua Kikwete ili warejeshe "zimwi likujualo halikuli likakwisha". Laiti wangelikuwa ni watu wapenda mabadiliko ya kweli, umma ungesimama nyuma yao, lakini kwa historia yao ni watu wanaolililia kurejea ukale wao.

Kwa Wakristo wanafahamu kwamba Musa alipowaongoza wana wa Israel kutoka utumwani Misri kwenda nchi ya ahadi, Kaanani, wapo waliofika njiani na kutamani kurejea utumwani kwa sababu walikumbuka nyama za bure. Wanopanga kumpinga Kikwete 2010 wamekumbuka vya kunyonga, wamekumbuka nguvu zao za kujichukulia kila walichotaka bila kuhojiwa kokote, wamekumbuka utukufu waliojitwalia miaka ya nyuma wanatamani hali hiyo. Hakika nia yao si kuwatumikia wananchi.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: