Wanaotaka urais Zanzibar kupitia CCM matumbo moto


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 07 July 2010

Printer-friendly version
Gumzo

NANI atapenya Zanzibar? Nani ataishia njiani? Nani ataibuka Mgombea Mwenza wa Jakaya Kikwete? Jibu litapatikana baada ya vikao vya uteuzi.

Vikao hivyo vya Chama Cha Mapinduzi (CCM), vinatarajiwa kufanyika Julai 9 na 10 mwaka huu.

Bali, kati ya wagombea watano kati ya 11 waliopendekezwa na Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) na ambao majina yao yatapelekwa Kamati Kuu (CC); yeyote anaweza kuteuliwa, ingawa sifa zao zinapishana.

Kwa utaratibu wa CCM, wagombea watatu miongoni mwa hao watano, ndio wanatarajiwa kufikishwa NEC kwa ajili ya kupigiwa kura.

Wagombea waliopenya katika tundu la kwanza la mchujo na ambao wanaweza kushinda bila upinzani mkubwa ni paamoja na Makamu wa Rais wa Jamhuri, Dk. Ali Mohammed Shein.

Dk. Shein (62) ambaye kuingia kwake katika kinyang’anyiro cha urais Zanzibar kumewashutua wengi, anapewa nafasi kubwa ya kuteuliwa.

Kwanza, kabla ya kujitosa katika kinyang’anyiro cha urais Viswani, Dk. Shein alikuwa na nafasi kubwa ya uongozi Zanzibar. Hivyo haitarajiwi atoswe mapema au hata baadaye katika kinyang’anyiro hiki.

Pili, Dk. Shein hatokani na kundi lolote miongoni mwa makundi mawili makubwa yanayokizana – kundi la Karume na lile la Dk. Gharib Bilal.

Kwa zaidi ya miaka 10 sasa, uhasama mkubwa umeibuka Zanzibar kwa makundi haya mawili, hasa lile la Dk. Bilal ambalo limekuwa likijiapiza kilipiza kisasi.

Tatu, Dk. Shein, nje ya vyama vya upinzani, ndiye anatajwa na wengi kuwa ana ubavu wa kuifikisha Zanzibar inakostahili kwenda – kurejesha umoja na utulivu na kusimamia serikali ya umoja wa kitaifa.

Katika hili, rais Karume tayari amejiandikia historia yake. Naye hatapenda kumuachia madaraka mtu ambaye atafuta historia aliyoiandika.

Nne, Dk. Shein anaungwa mkono na rais Karume jambo ambalo linarahisisha kampeni zake za urais. Katika hali ya kuviziana, kuogopana na kulindana, iliyojikita ndani ya CCM, wanasiasa wengi, hasa kutoka Zanzibar hawatapenda kukwaruzana na Karume.

Wanajua hatari ya kufanya hivyo. Kwamba pamoja na kwamba Karume atakuwa ameachia madaraka ya serikali, lakini bado ataendelea kuwa mmoja wa viongozi wa CCM.

Tano, Rais Jakaya Kikwete hatapenda kufanya kazi na mtu ambaye hawafahamiani vema. Hakika hatapenda mpole wa kondoo wala kingang’anizi cha “bwana haambiliki” na asiyeweza kupokea maagizo yake na kuyatekeleza.

Bila shaka, Kikwete atataka kufanya kazi na yule wanayefahamiana vizuri mapungufu yao. Hata serikali yake ya kwanza aliyounda, inaonekana kuwa ilijikita katika misingi hiyo. Alitanguliza mbele “maswahiba” wake.

Ikiwa hivi ndivyo, hapa Dk. Shein atakuwa amepata mtaji mwingine wa kisiasa.

Sita, mtaji mwingine wa Dk. Shein ni kule kuwa anatoka kisiwani Pemba. Viongozi wengi waliopo sasa, akiwamo Karume mwenyewe, wangependa kuvunja utamaduni wa miaka mingi wa rais kutotoka Pemba. Tangu Mapinduzi ya 12 Januari 1964, kisiwa cha Pemba hakijawahi kutoa rais.

Hata hivyo, kuna madai kuwa katika mazingira ya uchaguzi huru Zanzibar, hakuna hata mmoja miongoni mwa wagombea “anayeweza kumshinda mgombea wa CUF.”

Hili hasa linasemwa na upande wa upinzani unaodai pia kuwa katika mazingira ya uchaguzi wa mizengwe, wizi wa kura na vitisho vya vyombo vya dola, hata Shein aweza kuibuka kidedea.

Pamoja na mapungufu hayo, baadhi ya wananchi wa kawaida, na hasa wanaojua Zanzibar ilikotoka, ilipo sasa na inakoelekea, wanamuona Shein kama mtu mwafaka wa kupewa dhamana ya uongozi kwa wakati huu.

Mwingine ambaye anapewa nafasi kubwa, ni waziri kiongozi mstaafu, Dk. Mohammed Gharib Bilal (65). Huyu anaingia katika kinyang’anyiro hiki kwa mara ya tatu.

Viongozi wengi Tanzania Bara wanamuona Dk. Bilal kuwa ndiye pekee mwenye ubavu wa kumshinda mpinzani mkuu wa CCM, Maalim Seif Sharif Hamad, kutoka Chama cha Wananchi (CUF).

Hata hivyo, Dk. Bilal bado anaandamwa na vikwazo vilevile vilivyomzuia kuteuliwa mwaka 2000 na 2005. Kikubwa kinachompoza ni kubeba watu ambao tayari wanatuhumiwa kuifikisha Zanzibar ilipo sasa.

Kwa zaidi ya miaka mitatu ya utawala wa mwisho wa Dk. Salim Amour, ambapo Bilal alikuwa waziri kiongozi, serikali ilishindwa kulipa mishahara ya wafanyakazi.

Serikali ilituhumiwa kukubuhu kwa wizi. Ni katika utawala wa Dk. Bilal serikali ilipoingizwa mkenge baada ya kununua gari chakavu aina ya benzi kwa ajili ya matumizi ya rais, kutoka kwa mfanyabiashara binafsi, na bila kufuata taratibu za manunuzi.

Ni katika utawala wa Bilal, serikali ilituhumiwa kuuza ndege ya rais iliyokwenda matengenezo nchini Uingereza. Hadi sasa, si Dk. Bilal wala Dk. Salmin aliyejibu tuhuma hizo.

Katika mazingira hayo, Dk. Bilal atahitaji watu shupavu wa kumtetea ndani ya CC ingawa siyo rahisi kuwataja kwa majina kwa sasa.

Makamu mwenyekiti mstaafu wa CCM, John Malecela aliyekuwa akijtambulisha kuunga mkono Bilal, hatapenda kukwaruzana na Kikwete au Karume iwapo viongozi hao wawili watakuwa na mgombea wao mbali na Bilal.

Kiongozi pekee ambaye aweza kumtetea Dk. Bilal ndani ya CC – hata kama Kikwete na Karume hawamtaki, ni Spika wa Bunge la Jamhuri, Samwel Sitta.

Lakini naye ni lazima atapima hatua yake hiyo. Hii ni kwa sababu Sitta anajua kuwa tayari kambi ya Bilal “imefunga ndoa” na kundi la akina Edward Lowassa na Rostam Aziz.

Lowasa alikuwa waziri mkuu. Alijiuzulu na siyo kustaafu, kutokana na kashfa ya mkataba wa kufua umeme ya Richmond. Rostam ametajwa katika kashfa nyingi zikiwemo za Richmond na Kagoda.

Jingine linaloweza kumkwamisha Bilal, ni kule kumpinga Karume mwaka 2000. Wapo wanaosema wazi, kwamba kwa mahali ambapo Karume na Bilal wamefikia, Karume anaona ni afadhali Maalim Seif, kuliko Dk. Bilal.

Ni kwa sababu hiyo Karume hatapenda kukabidhi madaraka kwa yule anayedaiwa ataangamiza mbegu aliyoipanda.

Pamoja na hayo, hata madai kuwa wafuasi wake wametoa kauli za kutisha, kama ilivyoripotiwa katika vyombo vya habari, bado Dk. Bilal aweza kurejea Zanzibar kidedea.

Mwingine, ni mgombea mdogo kuliko wote, Shamsi Vuai Nahodha (48). Huyu anaweza kuwa mmoja wa washindani wakubwa wa kutoa upinzani thabiti.

Kwanza, huyu ndiye waziri kiongozi ambaye Rais Karume amefanya naye kazi kwa miaka 10 mfululizo. Iwapo kuna mazuri ambayo serikali ya Karume itajivunia, basi hawezi kumuweka upandeni Vuai. Iwapo kuna mabaya, naye yatamgusa.

Pili, mtaji mkubwa ambao Vuai anajivunia ni kuwa “ndiye mgombea pekee aliyefikia wajumbe wengi wa NEC Tanzania Bara.” Wengi wanamfahamu kwa kumtembelea na yeye kuwatembelea.

Baadhi ya safari zake zimekuwa za siri na haziripotiwi kwenye vyombo vya habari.

Hata hivyo, hakuna mwenye uhakika kama Rais Karume anaweza kuwekeza kwake. Hii ni kutokana na madai kwamba amekuwa haridhiki na baadhi ya utendaji wake na hasa katika eneo la ushauri.

Lakini kule “kuchongwa” kwa Ali Juma Shamhuna na kumkabidhi cheo “bandia” cha naibu waziri kiongozi mara baada ya uchaguzi wa mwaka 2005, kunaweza kuthibitisha kuwa Karume na Vuai, ni wawili tofauti.

Lakini kule kubahatika kulelewa na viongozi waandamizi katika chama na serikali – Benjamin Mkapa, Kikwete, Karume na Shein, kunaongeza mtaji wa Vuai.

Katika orodha hiyo ya wagombea waliopitishwa na Kamati Maalum, yumo Ali Juma Shamuhuna (66). Ni mwanasiasa ambaye kauli na vitendo vyake mara nyingi havikutani.

Hana msimamo unaofahamika katika itikadi ya kukipenda chama chake. Pale anapopambana na mawimbi, haraka huliacha jahazi analoliongoza.

Shamhuna ni miongoni mwa wana-CCM waliokuwa wakituhumiwa kudhoofisha serikali kwa kutoa kauli kali ndani na nje ya Baraza la Wawakilishi.

Hiyo ilikuwa kabla ya Shamhuna kuwa waziri wa Habari, Michezo na Utamaduni, katikakati ya miaka mitano ya kwanza ya utawala wa Rais Karume.

Katika uchaguzi uliopita wa ndani ya CCM (2007), Shamhuna alishindwa kuchaguliwa kuwa miongoni mwa wajumbe wanne wa NEC kutoka nyumbani kwake, Kaskazini Unguja.

Wanaomkandia Shamhuna wanadai aweza kuwa na siasa za kulipizana kisasi iwapo atapewa nafasi ya kuwa rais wa Zanzibar. Historia imejaa mifano inayokinzana na utabiri wa aina hiyo na Shamhuna aweza kushangaza wanaomtuhumu.

Lakini mgombea mwingine ambaye hatajwi sana, bali wanaomfahamu wanasema, “anaweza kuwaunganisha Wazanzibari,” ni Mwalimu Haroun Suleiman.

Hata hivyo, huyo anakabiliwa na kibarua kigumu kupenya kutokana na rangi yake. Haroun ana asili ya bara la Asia.

Tayari mwenyewe aliliambia gazeti hili wiki iliyopita, “…Nihukumiwe kwa matendo yangu, si rangi yangu.”

Kihistoria, Haroun aliyekuwa mwalimu wa Sekondari, alipanda hadi kufikia kuwa mkurugenzi wa mipango katika wizara ya elimu.

Mwaka 2000 alichaguliwa kuwa mjumbe wa Baraza la Wawakilishi katika jimbo la Makunduchi, nafasi iliyomfanya kuchaguliwa kuwa waziri wa elimu Zanzibar.

Mbali na kuwa waziri, ni mbunge wa bunge la Jamhuri na mjumbe wa NEC. Wanaomfahamu wanasema, ni yeye na Shein pekee, kama wakipewa nafasi wanaoweza kusimamia kikamilifu kile ambacho Karume anataka kitendeke – Serikali ya Umoja wa kitaifa.

Hata hivyo, jambo moja ni wazi. Uamuzi wa Kamati Maalum si wa mwisho. Bado wagombea wengine sita ambao majina yao hayakupendekezwa, wanaweza kufikishwa (CC) na hata NEC.

Wagombea waliotemwa na ambao wanaweza kuibukia Dodoma, ni Balozi wa Tanzania nchini Italia, Ali Karume, naibu waziri wa Afrika Mashariki, Mohamed Aboud, mfanyabiashara Mohammed Raza, Omari Sheha, Hamad Mshindo na Mohammed Yusuf Mshamba.

Lakini uwezekano wa wagombea hao, kuibukia Dodoma, ukimuacha Aboud ambaye kuondolewa kwake kunaonekana kulipangwa, bado ni finyu. Wengi wa walioshindwa kupenya, hawakuwa washindani, bali wasindikizaji.

Aboud ambaye ameondolewa kutokana na kile kinachoitwa “kukizana kwa maelezo ya elimu yake,” ndiye anayeonekana kukubalika zaidi kisiwani Pemba miongoni mwa wagombea ndani ya CCM.

Hakuna asiyejua umuhimu wa kura za Pemba katika uchaguzi wa Zanzibar. Katika chaguzi tatu zilizopita, Chama cha Wananchi (CUF) na mgombea wake urais, Maalim Seif Sharif Hamad wameweza kudhihirisha umwamba kwa CCM kisiwani humo.

Miongoni mwa wabunge 20 wa kuchaguliwa wa chama hicho, wabunge 19 wamepatikana Pemba.

Bali Aboud anakabiliwa na “dhambi ya ubaguzi.” Dhambi ileile ambayo wafuasi wake wa sasa walimtwisha Dk. Salim Ahmed Salim mwaka 2005.

Mbarouk Msabaha Salum, ambaye sasa ni mmoja wa wapigadebe wakuu wa Aboud, ndiye mwaka 2005 “aliyejipa kazi” ya kumchafua Dk. Salim kwa maelekezo maalum kutoka “kundi la mtandao” lililomuingiza madarakani Rais Jakaya Kikwete.

Jingine analokabiliwa nalo, ni historia yake ndani ya CCM. Wapinzani wake wanamuita mwanachama mchanga. Hata hivyo, CCM inakariri kauli zake kuwa “kila mwanachama ana haki sawa na mwingine.”

Jingine linaloweza kutokea, ni CC kupeleka kwa NEC, jina la mgombea mmoja ili kupigiwa kura. Habari zinasema, mkakati wa kupeleka jina moja katika mkutano wa NEC una baraka za vigogo karibu wote wa juu wa chama hicho, akiwamo Rais Kikwete.

Maelezo yanayotolewa ni kwamba, hatua ya kupeleka jina moja itasaidia kumaliza makundi. Lakini ni suala la “tusubiri tuone;” huku matumbo ya wagombea yakisagika.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: