Wanapozitaka sifa, wabebe pia lawama


M. M. Mwanakijiji's picture

Na M. M. Mwanakijiji - Imechapwa 08 September 2010

Printer-friendly version
Kisima cha Mjadala

KATIKA kipindi hiki cha kampeni, yatasemwa na kuimbwa mengi. Mazuri na mabaya. Hata hivyo, viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) hawawezi kukwepa lawama na shutuma, kwamba ni mabingwa wa kukana yaliotendeka na kusema hayawahusu.

Lakini nani asiyefahamu kuwa mfumo wa rushwa umejengwa, kulelewa na kukomazwa chini ya utawala wa CCM?

Pamoja na jitihada mbalimbali za kupambana na kutokomeza rushwa, bado adui huyo mkubwa wa haki anaendelea kutamba kama vile mgonjwa wa akili.

Rushwa hiyo, ni zao la mfumo wa utawala. Mahali popote duniani ambapo rushwa imekithiri chanzo chake kikubwa ni mfumo wa utawala wa kisiasa ambao ndio hutengeneza mfumo wa sheria katika nchi.

Hadi sasa, bado tunajua kuwa Taasisis ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU), haijaandaliwa kuwa chombo kinachoweza kupambana na rushwa.

Ukiondoa mazingaombwe ya hapa na pale ambayo huwa wanayafanya kwa ajili ya vyombo vya habari bado hatuna chombo huru na cha kweli cha kupambana na rushwa.

Hili ni zao la utawala wa CCM. Ndiyo maana leo Rais Jakaya Kikwete na wengine wanapopita kupiga kampeni wanatuahidi kuwa ati wakiingia madarakani wataiongeza nguvu na “meno” TAKUKURU.

Mtu mwenye akili timamu ambaye ni huru katika fikra zake, lazima ajiulize kwanini hawakuiongezea meno miaka hamsini au hata mitano iliyopita? Je, kama wanajua inahitaji mabadiliko, kwanini wanaipa meno kwa kibaba?

Kinachohitajika siyo meno bali ni uhuru zaidi, kitu hiki CCM na serikali yake hawako tayari kukiona kinafanyika. Siyo uhuru wa “kukamata” na “kuvizia” la hasha ni uhuru wa kutenda kwa yeyote!

Wizi mkubwa kabisa katika benki kuu ya taifa (BoT) umetokea chini ya utawala wa CCM. Ninapoona wananchi wa Tanzania wamevaa magwanda ya kijani na njano wakiruka ruka kwa furaha huwa najiuliza: Je, wanajua kilichotokea chini ya utawala huo?

Jibu langu ni kuwa wanajua, lakini hawajali. Wanajua kuwa ufisadi mkubwa kabisa ambao hutokea katika benki kuu yoyote duniani, umetokea Tanzania.

Huu siyo wizi wa kawaida wa fedha za umma ambao huwa unatokea hata sehemu nyingine, bali ni mtandao kama wa buibui ambapo wezi wa kimataifa wakishirikiana na wanasiasa na viongozi wa umma walikaa na kuamua kunyofoa utajiri wetu kama waliolaaniwa.

Hata leo hii, kutokana na kukosekana chombo huru cha mahakama, wahusika wa kweli bado hawajasimamishwa. Baadhi yao, leo ni wagombea na wengine watapewa hata na uwaziri iwapo chama chao kitashinda urais.

Ni lazima CCM kikubali kuwa kama wao ndio waliwekwa walinzi wa nyumba na wizi ukatokea wakati lindo ni lao, basi wao ni washukiwa wa kwanza! Katika wizi huu mkubwa wa fedha za umma, washukiwa wa kwanza ni walinzi wakuu ambao si wengine, bali ni chama kilichounda serikali. Hili ni lazima CCM wakubali.

Ubora wa huduma mbalimbali bado umedorora chini ya utawala wa CCM. Moja ya vitu ambavyo vitasikika katika kipindi hiki cha kampeni ni jinsi gani vitu vimeongezwa wingi, badala ya ubora.

Viongozi wa chama hiki watanadi, kuna shule nyingi, barabara, wanafunzi, mipango na mikakati kedekede ya kuleta maendeleo.

Tokea kuanza kwa kampeni wagombea wa CCM kwa ngazi mbalimbali wamekuwa wakitutaka tuangalie wingi wa vitu, kiasi kwamba wengine wamefikia kutuonesha kuwa wingi wa simu na ongezekeko la msongamano wa magari ni dalili ya maendeleo.

Kwa watu ambao hawana uwezo na utayari wa kufikiria kwa makini wanaamini kabisa kuwa maendeleo ni kuongeza wingi.

Maendeleo ni ubora na siyo wingi. Dhana hii ya maendeleo imepotea ndani ya CCM kwa karibu miaka 25 sasa hasa baada ya wao kubadili nadharia ya ubora kama kipimo cha maendeleo na kuwa “wingi ndio maendeleo.”

Matokeo yake, mipango na mikakati yao mingi imejikita katika kuongeza wingi wa vitu, badala ya ubora.

Kwa mfano, kwenye baadhi ya nyaraka za CCM zinayoelezea kuwa kile kinachoitwa “mafanikio ya awamu ya tatu – 1995 hadi 2005” karibu asilimia 100 ya yanayoitwa mafanikio yanazungumzia kuongezeka kwa vitu kuwa kipimo cha maendeleo.

Mathalani, idadi ya shule za msingi za serikali ambapo wanasema imeongezeka kutoka 10,891mwaka 1995 hadi 13,533 mwaka 2004;

huku watoto wanaoandikishwa darasa la kwanza ikidaiwa kuongezeka kila mwaka kutoka 712,593 mwaka 1995 hadi 1,368,315 mwaka 2004 likiwa ni ongezeko la asilimia 47.9.

Katika sekta ya afya, CCM wanasema serikali imejenga hospitali mpya kutoka 194 mwaka 1995 hadi 221 mwaka 2004. Hili ni ongezeko la asilimia 14.

Mgando huu wa kupima wingi kuwa ndiyo maendeleo, limeingia hata katika utawala wa Kikwete. Katika hotuba yake ya kufunga Bunge alitumia kipimo hikihiki kuelezea mafanikio ya serikali yake kuanzia 2005 hadi sasa.

Alisema, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, serikali imepeleka mahamani kesi za rushwa 780. Idadi hii ni kubwa ukilinganisha na kipindi cha miaka 20 iliyopita ambazo zilikuwa 543.

Alijigamba kupandisha kima cha chini cha mishahara ya watumishi wa umma kutoka Sh. 65,000 hadi Sh. 135,000 sawa na ongezeko la asilimia 107.

Mifano hiyo michache, kati ya mingi inapima maendeleo kama kuongeza idadi. Ukiangalia kwa haraka unaweza ukasema kuwa kwa vile vimeongezeka wingi basi na ubora nao umeongezeka. Lakini inabidi tujiulize kama kweli hali iko hivyo.

Ni wazi kwamba mafanikio yote tunayoyasikia wakati huu wa kampeni; porojo zote tunazozisikia na ahadi zote za mema yaliyofanyika chini ya utawala wa CCM kwa miaka mitano iliyopita au hamsini iliyopita ni lazima yawekwe katika mizani iliyo sawa.

Mtu yeyote anayeenda kupiga kura ni lazima apige kura akiwa amepima kwenye mizani hiyo na kujiuliza kama ameridhika na hali iliyopo. Kama mtu atakuwa ameridhika na pande zote hizo mbili ni lazima airudishe CCM madarakani tena kwa furaha huku akijichekelesha kwa furaha.

Hata hivyo, endapo mtu atapima uzito wa kile kilichopo sasa na kuelewa kuwa matokeo ya kukirudisha chama kilichopo ikulu madarakani ni mwendelezo wa pande hizi mbili zilivyo sasa, ni lazima basi afuate dhamira yake na kuchagua chama tofauti ambacho kitamletea yale mabadiliko anayotaka.

Kumbe uchaguzi huu siyo wa vionjo au hisia tena. Uchaguzi huu siyo wa watu wenye njaa tena. Ni uchaguzi wa kiakili. Ni uchaguzi wenye kufuata mantiki. Ni uchaguzi wa kufuata dhamira kuliko rangi na sura, ni uchaguzi wenye kutuata hatima ya taifa kuliko nyimbo za kisiasa. Ni uchaguzi wenye kufuata ukweli kuliko upepo wa ushabiki.

Kama unataka kupiga kura yako vizuri, ni lazima uwe umepima uzito wa sifa unazowapa watawala na lawama wanazostahili kubeba. Kama huamini kuwa wanastahili kubeba lawama yoyote basi wewe ni bora ukae nyumbani.

Lakini, kama hutaki kukubali kuwa kuna mazuri ambayo nayo yamefanyika na wewe hufai, kwani huwi mkweli.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: