Wanasiasa wanajijali tu, elimu wameitupa


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 02 March 2011

Printer-friendly version

KILA unapoibuka mjadala kuhusu elimu nchini, wengi hukimbilia kudai kiwango kimeshuka katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni si zamani.

Wengine wanadai vijana wengi wanaomaliza kidato cha nne na sita, hawajui Kiingereza. Kwao, Kiingereza ni kigezo cha kushuka kwa kiwango cha elimu.

Wanasiasa wameingia mtegoni; lakini kauli na majibu yao yanathibitisha tatizo ni kubwa kuliko inavyofikiriwa.

Kama kutojua au kubabaika kuzungumza ‘kimombo’ ni kigezo, basi mbunge mmoja wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), atakuwa kitanzini.

Mbunge aliyeomba kuwa mbunge wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), aliwaacha wabunge wote hoi.

“Tutajie kirefu cha SADC jumuiya ambayo wewe unataka kuwa mbunge?” aliulizwa kwa Kiingereza.

Majibu: “Aah… SADC sijui, nadhani kila mmoja hajui.”

Akabandikwa swali la pili, “Tueleze SADC ilianzishwa lini.” Akajikanyaga na kusababisha kicheko bungeni.

Kama mbunge anataka kuwa mwakilishi wa wananchi katika chombo ambacho hakijui, maana yake ni nini? Kama mbunge hajui mambo anayopaswa kuyajua, si moja ya vigezo kukosa sifa?

Mbunge wa Mbinga Magharibi, John Komba ni mfano mwingine kwamba hata waliosoma zamani wanatia shaka juu ya kiwango chao kielimu.

Akichangia hotuba ya Rais Jakaya Kikwete ya uzinduzi wa Bunge mwaka jana, kuhusu kipengele cha elimu, Komba alikiri hata yeye hakufaulu mtihani lakini leo ni “mheshimiwa mbunge.”

Komba alitaka kusemau kwamba kushindwa mtihani si kushindwa katika maisha. Kauli hiyo haikupaswa kutolewa na mtu wa aina yake anayepaswa kuhimiza ubora wa elimu unaoambatana na kufaulu mitihani.

Komba hakujua anawaambia wananchi wa jimbo lake kwamba wanaongozwa na mtu aliyefeli mtihani? Hivi hajui kilichomsaidia si ufaulu ila kigezo cha kujua kusoma na kuandika?

Komba hajui kwamba kuvuka ngazi moja, yaani kutoka ya chini kwenda ya juu, lazima ufaulu, lakini hauhitajiki ufaulu kuwa mbunge? Bungeni, kuna wabunge wengi walioishia darasa la saba na ni wamiliki wa biashara kubwa, lakini wanasheria, madaktari, wahandisi ni wasomi wenye ufaulu wa juu. Kama mbunge hajui hili, kiwango chake cha uelewa kinatia shaka.

Mbunge wa Viti Maalum, Martha Mlata hakufikiria mara mbili aliposema “zisingekuwepo shule hizi za kata kusingekuwa na sifuri hizi tunazozungumzia.”

Mbunge huyo alitaka kuonyesha kwamba wingi wa sifuri ni sehemu ya mafanikio katika mikakati ya serikali ya CCM kuboresha elimu.

Ni kweli kusingekuwa na shule hizi mbovu za kata kungekuwa na shule bora, zenye vifaa vya kufundishia na kujifunzia, vitabu, maabara, maktaba, walimu bora na kwa hiyo, kusingekuwa na sifuri hizo.

Inasikitisha kuona kuwa wanasiasa ambao wanapaswa kukerwa na sifuri nyingi na kuwa sehemu ya kutafuta ufumbuzi, wanatoa kauli zinazotia shaka juu ya kiwango chao na ushabiki wa vyama.

Marupurupu

Miezi ya Septemba na Oktoba mwaka jana ilikuwa ya hekaheka za kampeni na uchaguzi wa rais, wabunge na madiwani. Walimu walitumika kutengeneza wanasiasa, sasa wanadharaulika.

Baada ya kutia mguu bungeni, kila mbunge amelamba Sh. 90 milioni kwa ajili ya kununua gari la kutembelea. Mwalimu amepewa nini? Kila mbunge analamba Sh. 12 milioni za mshahara na marupurupu mengine kwa mwezi. Mwalimu anaondoka na kiasi gani?

Kwanini siasa imetukuzwa na kufanywa kazi rahisi hata kwa aliyefeli, lakini ndiyo inayolipa kuliko wafanyakazi wasomi katika sekta nyingine?

Wanasiasa wanajua hadhi ya walimu ilivyoporomoka ikilinganishwa na wa miaka ya 1970? Wanajua mfumo uliopo hausaidii kuinua elimu ila kudidimiza kiasi kwamba walimu hawatembei kifua mbele, hawajivunii kazi yao na hawaheshimiwi hata na serikali yao?

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: