Wanawake UWT wavuana nguo 


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 25 November 2009

Printer-friendly version
Waziri Sophia Simba aongoza mashambulizi
Apuuza na kukejeli ujumbe wa Rais Kikwete
Waziri wa Utawala Bora, Sophia Simba

KIKAO cha Baraza Kuu la Umoja wa Wanawake (UWT) kilichofanyika Dodoma wiki iliyopita, kiliishia kuwa cha matusi ya nguoni yaliyoongozwa na Waziri wa Utawala Bora, Sophia Simba.

Mlengwa mkuu wa matusi yaliyorushwa kwa siku nne mfululizo alikuwa Katibu Mkuu wa umoja huo, Husna Mwilima, MwanaHALISI limeelezwa.

Taarifa za ndani ya kikao zinasema  wajumbe walimshambulia Husna hadi akaishiwa nguvu na kulazimika kukimbizwa hospitali kuu ya mkoa iliyoko mjini Dodoma ambako alilazwa kwa saa 17.

Imeelezwa kuwa Simba hakwenda hata kumwona katibu wake hospitalini.

Kwa mujibu wa mtoa taarifa, wasemaji wakuu na ambao walimvurumishia matusi Husna ni pamoja na Sophia Simba mwenyewe, Makamu Mwenyekiti wa Zanzibar, Asha Bakari Makame na Naibu Katibu Mkuu wa UWT Tanzania Bara, Amina Nassoro Makilagi.

Wengine walionukuliwa wakirusha matusi kwa Husna ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) Catherine Peter Nao anayekabiliwa na tuhuma nzito za kutokuwa raia wa Tanzania na Mary Chitanda ambaye ni katibu wa CCM mkoani Arusha.

Wajumbe wengine kwenye orodha ya kutoa mashambulizi ya kauli ni Katibu wa UWT mkoa wa Dar es Salaam, Tatu Mariaga na wajumbe Amina Kanyogotwa na Nenburis Kimbele ambaye ni Mwenyekiti wa UWT mkoa wa Arusha.

Mvua ya kejeli, kebehi na matusi ilianza mapema wakati wa ufunguzi wa kikao, asubuhi ya tarehe 16, Jumatatu iliyopita wakati Simba akifungua kikao.

Katika hotuba yake Simba alisema hana msaada wowowte kutoka kwa Katibu Mkuu. Alisema, “…maandalizi yote ya mkutano huu mnayoyaona ni kazi ya naibu wenu, Amina Nassoro Makilagi. Makbrasha yote ni Amina, fedha za mkutano ni Amina.”

Baada ya kumwaga sifa kwa naibu katibu, mtoa taarifa ameeleza, Simba aliuliza wajumbe, “Sasa mnataka nini?” Kama vile wamepangwa, sauti zikasikika, “Mpe ukatibu. Anafaa huyo…”

Huku baadhi ya wajumbe wakiwa bado wamepigwa na butwaa, Simba aliendelea kuporomosha vijembe kwa kusema, “Umegawa kadi za harusi ya mwanao kwa kila mtu. Unataka kila mtu akuchangie. Mara wakuchangie. Arusha wakuchangie. Iringa wakuchangie. Acha hizo!”

Kama anayemfunda Husna, Simba ameripotiwa kusema, “Wewe Husna unavaa sana. Unajipenda. Unataka kufanana na Mama Salma Kikwete. Mama Salma akivaa kilemba na wewe uvae. Sisi wenzako aka… Tunajipendekeza?”

Mtoa taarifa amemnukuu Simba akisema, “…harusi ni kati yako na mumeo. Unataka kutumia UWT kutafuta umaarufu. Ondoka hapa.” Wakati wote Husna alikaa kimya akitafakari yote haya yametoka wapi, ameeleza mtoa taarifa.

Kikao cha baraza kuu kilikuwa cha siku moja kilichohudhuriwa pia na Katibu Mkuu wa CCM, Yusuph Makamba. Ilikuwa mwishoni mwa kikao hicho, taarifa zimeeleza, tena baada ya kikao kufungwa, Simba alileta hoja ya kumtuhumu katibu mkuu kuwa hana ushirikiano naye na kwamba katibu hamsikilizi.

Alinukuliwa akisema kuwa hawezi kufanya kazi na Husna na hivyo kuwaomba “wamuondoe.”

Baadhi ya wajumbe walisimama na kumwambia Simba kuwa hoja yake haikuwa imeanzia kwenye kamati ya utekelezaji, hivyo pale hapakuwa mahali pake.

Mtoa taarifa anasema ndipo Simba aliamua yaishe kwa siku hiyo na kesho yake akaitisha kikao cha kamati ya utekelezaji, chini ya usimamizi wake na kuorodhesha tuhuma 12 dhidi ya katibu mkuu.

Miongoni mwa tuhuma dhidi ya Husna ni kutomtii mwenyekiti, matumizi mabaya ya fedha, kujivuna na kutomfuata mwenyekiti ofisini kwake na badala yake kuta yeye ndiye afuatwe.

Siku tatu zilizobaki zilikuwa za semina iliyoandaliwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Tume ya Haki za Binadamu na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA).

Kwa mujibu wa taarifa, katibu mkuu alikabidhiwa tuhuma siku ya pili ambayo ilikuwa siku ya kwanza ya semina na kutakiwa kuzijibu palepale.

Hata kabla Husna hajaweza kujibu tuhuma, baadhi ya wajumbe wakaamsha mikono wakitaka kuchangia na kuruhusiwa na mwenyekiti.

Alikuwa Catherine Nao aliyenukuliwa akisema, “Mheshimiwa mwenyekiti, huyu Husna anaringa sana. Namshangaa. Huyu nani kwani? Huyu si boi tu… Anaringa nini…?” huku baadhi ya wajumbe wakishikwa na butwaa.

Catherine alifuatiwa na Mary Chitanda ambaye alisema, “Mwenyekiti wewe ndiye umetuletea huyu mtu…  sijui ulimwokota wapi halafu ukamleta humu ndani. Tuondoshee huyu hatumtaki.”

Chitanda amenukiliwa akisema, “Yeye … kujipamba tu, hana jingine. Hajui kazi, hana lolote analolijua zaidi ya umbea na kutuibia fedha zetu. Tupishe bibi tufanye kazi zetu.”

Taarifa zinasema Chitanda alifika mbali zaidi na kusema, “Hata kama watu watapeleka ujumbe kwa ‘bwana mkubwa,’ kikao hiki ni cha mwisho, hakuna mwenye uwezo wa kutuingilia.”

Ujumbe kwa “bwana mkubwa” umeelezwa kuwa ni ujumbe wa simu ya mkononi kutoka kwa Rais Jakaya Kikwete ambao haikuwezekana kuthibitishwa.

Imedaiwa kuwa wakati wa kuporomosha matusi kwa Husna, kuna aliyepeleka ujumbe kwa Kikwete kueleza hali ilivyo ukumbini. Imedaiwa kuwa Kikwete aliandika juu ya ujumbe huo maneno, “Mtendeeni haki Katibu,” na kuupeleka kwa kiongozi mmoja wa CCM.

“Mimi ninao hapa, lakini siwezi kukuachia unukuu. Unajua ninyi waandishi mna mengi,” ameeleza mmoja wa wajumbe. Imeelezwa kuwa mmoja wa maofisa wa umoja huo aliusambaza kwa wajumbe wengi.

Baadhi ya wanaotajwa kusambaziwa ujumbe huo ni pamoja na Simba, Mary Chitanda, Catherine Nao na Nenburis Kimbele, mjumbe wa Baraza kutoka Arusha.

Hata hivyo Chitanda amenukuliwa akisema, “Haya mambo ni yetu sisi. Watu wanapeleka umbea kwa bwana mkubwa. Baraza hili ndilo lenye uwezo na mamlaka ya mwisho ya kuamua nini kifanyike, mwenyekiti muondoe huyu mtu…”  

Ilikuwa baada ya mashambulizi haya, Husna aliomba kujibu tuhuma. Kwa mujibu wa mtoa taarifa, naye alianza kwa jazba akishambulia wenzake, lakini mjumbe Zaria Madabida ndiye amenukuliwa akisema, Husna “Anasakamwa kwa mambo yasiyokuwa ya msingi.”

Alisema haoni kosa lolote na bali anaona kuna njama zilizopangwa na baadhi ya watu kwa malengo binafsi.

Wengine waliomtetea Husna ni Zainab Vulu, Dk. Zainab Gama, mwenyekiti wa UWT Manyara ambaye amejulikana kwa jina la Maria na Amina Masenza, mkuu wa wilaya wa Shinyanga.

Maria alisema, “haiwezekani mtendaji mkuu akashambuliwa na watu tukakaa kimya.”

Kauli ya Maria iliungwa mkono na Amina Masenza, ambaye alimtaka Simba kuachana na njama za kumsakama katibu wake.

Alhamisi ya tarehe 19, baada ya wajumbe wengi, mmoja baada ya mwingine, kushambulia katibu mkuu, na yeye akiwa amesimama akitaka kusoma utetezi wake, Asha Bakari Makame, Makamu mwenyekiti UWT Zanzibar alimrukia na kudai kuwa siyo utaratibu kwa mtuhumiwa kusoma utetezi wake.

Ndipo Simba akasoma utetezi wa Husna ambamo alikana tuhuma zote. Aliamriwa kutoka nje wakati wanajadili na kupitisha maamuzi ambao imefahamika kuwa ni “onyo kali.”

Habari za ndani ya UWT zinasema chanzo cha ugomvi kati ya Husna na Simba ni Naibu Katibu Mkuu wa UWT, Tanzania Bara, Amina Makilagi, ambaye inadaiwa anatamani nafasi ya Husna. Amina hakupatikana …

Makamu mwenyekiti Zanzibar Asha Bakari Makame alipoulizwa kuhusu sakata hili na hatua gani zimechukuliwa dhidi yake, alisema hawezi kuongea na waandishi wa habari mmojammoja. Alisema angeongea na vyombo vya habari jana.

Naibu katibu mkuu Zanzibar Salama Aboud amesema yuko kwenye kikao na kwamba asingeongea lolote kuhusu suala hilo.

Naye Sophia Simba alimwambia mwandishi wa habari hizi kwa maneno mawili ya Kiingereza, “No comment” – sina la kusema.

Simu ya Mary Chitanda iliita bila kupokelewa; naye Amina anayedaiwa kutaka nafasi ya Husna, hakuweza kupatikana. Simu yake iliita bila kupokelewa.

Husna alipotakiwa kuzungumzia sakata hili, alisema ni kweli alituhumia lakini akaongeza, “Sijawa katika nafasi nzuri ya kuzungumzia suala hili.”

Hata hivyo, kikao cha baraza kuu hakina uwezo wa kumvua madaraka katibu mkuu bila kurejea kwenye Kamati Kuu ya CCM.

Katika kipindi cha wiki tatu, Simba amemsifia aliyekuwa waziri mkuu Edward Lowassa kuwa ni “mwanaume wa shoka” na amewaparura Mzee John Malecela na mkewe Anne Kilango kwa madai kuwa wamewahi kufadhiliwa na Jeetu Patel ambaye sasa ni mmoja wa watuhumiwa wa ufisadi nchini.

Katika kipindi hichohicho, Simba ametangaza kuwa katika CCM hakuna aliye safi.

Mashambulizi ya sasa dhidi ya Husna yanachukuliwa kuwa mwendelezo kwa wale ambao haafikiani nao.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: