Wanawapiga, wanawatia vidole makalioni


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 16 March 2011

Printer-friendly version

WANAWAPIGA viboko wachimbaji wadogo, wanawachoma kwa vijinga vya moto, wanawabamiza kwa vitako vya bunduki, wanawakata kwa mapanga, wanawaingiza vidole matakoni na kuwapora mali zao.

Ni masimulizi yanayoambukiza uchungu na pengine kinyaa. Ni ukatili wa aina yake.

Inadaiwa vitendo hivyo vinafanywa na askari wa hifadhi ya wanyamapori ya Selous mkoani Morogoro.

Wanaotendewa unyama huo ni wananchi wanaochimba dhahabu katika eneo la Lukula, kijiji cha Ketaketa, karibu na msitu wa Korongo, kata ya Ilonga wilayani Ulanga.

Abdi Bakari (47) ni mwenyekiti wa umoja wa wachimba dhahabu katika eneo hilo lililopo mpakani mwa kijiji cha Ketaketa na hifadhi ya wanyama.

Bakari anasema askari wa hifadhi “wamekuwa wakitukamata, kutupiga na kutupa mateso makubwa.”

Ukatili huo umeanza baada ya kugundulika madini ya dhahabu katika eneo hilo. Hapa ndipo kuna watu zaidi ya 4,000 ambao wameweka kambi huku wakichimba dhahabu.

Baada ya watafuta dhabu kuwa wengi, uongozi wa kijiji cha Ketaketa uliamua ufanyike uchaguzi wa viongozi wa umati uliongia na ndipo Bakari akachaguliwa kuwa mwenyekiti.

Taarifa za kugundulika dhahabu zilipatikana Desemba mwaka jana. Mwaka huu Januari “ndipo ikaja taarifa kuwa eneo hilo ni la hifadhi ya selous na kuwataka wachimbaji wadogo kuondoka mara moja.”

Bakari anasema kutokana na eneo hilo kuwa na madini mengi, watu wamegoma kuondoka. Ndipo askari wa hifadhi hiyo walipoanza kuwatoa kwa nguvu ikiwa ni pamoja na kuwapora dhahabu walizopata na mali nyingine.

“Ni adha tupu. Askari wa mbuga za selous wanatumia kuni zenye moto – vijinga –kuwachoma wachimbaji hao kwenye miguu na mikono huku wakiwalazimisha kuonyesha walipoficha madini yao.

“Wengine walipata kipigo kikali, kusechiwa hadi sehemu za haja kubwa kutafuta kuona iwapo wameficha madini huko,” anasimulia Bakari.

Mwandishi amefanikiwa kuona baadhi ya watu waliopigwa na askari wa mbugani na kuona vidonda pamoja na makovu yao.

Miongoni mwa waathirika walioonana na mwandishi ni pamoja na Agustino Nyoni, Ndusu Mwalusamba na Prosepar Nikasi waliochomwa miguuni kwa kijinga cha moto.

Wengine ni Pascal Modest aliyeumizwa karibu na jicho, Emmanuel Stephano aliyeumizwa kwenye paja na Zacharia Nyakunga aliyeumizwa kwenye goti na bado kidonda ni kibichi.

Kwa upande wake, mwenyekiti wa kijiji cha Ketaketa, Ismail Said Maunga amesema matendo yaliyofanywa na askari wa hifadhi ya selous ni ya ukiukaji haki za binadamu.

Maunga anasema anaongea kama mwenyekiti na katika wadhifa huo, miaka yote anajua eneo ilikogundulika dhahabu ni la kijiji.

Anasema ilikuwa baada ya kutokea kwa mgogoro kati ya wasimamizi wa mbuga na kijiji ndipo uongozi wa hifadhi ulijitokeza na kudai kuwa eneo la dhabu liko chini ya sa selous.

Naye diwani ya kata ya Ilonga, Kachengeza Rashid, alimweleza mwandishi kuwa wameomba ofisi ya ardhi wilayani iwapatie ramani ili kujiridhisha juu ya uhalali wa miliki ya eneo hilo.

Diwani Rashid amesema tayari amewasiliana na ofisi ya mhifadhi mkuu wa selous juu ya unyama wa askari wake na vitendo vyao vya kinyama.

Amesema kuwa amekumbusha wakuu wa selous kuwa askari wao hawana haki wala sababu ya kutoa hukumu kwa yeyote.

“Tumewaambia jukumu la polisi wao ni kukamata watuhumiwa na kuwafikisha polisi; baada ya hapo wafikishwe mahakamani na siyo kuwapiga au kuwafanyia vitendo vyovyote vya kinyama,” ameeleza Rashid.

Akiongea kwa kujiamini, Kaimu Mkuu wa Hifadhi, Ramadhan Mkhofoy, amekiri kutuma askari wake kukamata watu wote aliosema wameingia katika eneo la hifadhi.

Hadi sasa wananchi zaidi ya 60 wameshakamatwa na kufikishwa polisi kwa hatua za kisheria.

Mhifadhi huyo alisema hajapata malalamiko yoyote ya watuhumiwa kunyanganywa mali zao au kuchomwa moto na askari wake. Amedai wanachofanya askari wake ni kumwambia mtuhumiwa kuwa yupo chini ya ulinzi pindi anapokaidi amri; ndipo anakamtwa na kufikishwa polisi.

Mkhofoy alisema kwanza walitoa siku tatu kwa watu kuondoka wenyewe, lakini walipokataa kutii amri, ndipo hatua zikachuliwa dhidi yao kwa kukamata na kuwapeleka polisi.

“Ningeshafunguliwa kesi na hao wanaodai kuchomwa moto na kunyang’anywa mali zao,” amesema Mkhofoy.

Amesema watuhuhimiwa wote watapelekwa mahakamani na kufunguliwa mashtaka.

Kwa upande wake kamanda wa polisi wilaya ya Ulanga, Bw. Abed Sanja amekiri kuwepo kwa matukio hayo likiwemo la watu wawili kuomba fomu maalum ya kwenda kutibiwa (P. F3).

Kamanda amesema wamefungua jalada lakini hakuna kati yao aliyerudi kwa ajili ya uchunguzi zaidi kuhusu askari kuwapiga.

Sanja amesema polisi hawahusiki moja kwa moja katika kukamata watu ndani ya hifadhi ya wanyamapori kutokana na mguga kuwa na askari wake.

0
No votes yet