Wangeanza hawa taifa lingekuwaje?


M. M. Mwanakijiji's picture

Na M. M. Mwanakijiji - Imechapwa 22 June 2011

Printer-friendly version
Kisima cha Mjadala

MASHAMBULIZI dhidi ya Mwalimu Julius Nyerere yameendelea kwa nguvu katika mitandao ya intaneti. Binafsi, siamini kuwa wanaochafua Nyerere wametumwa na watawala.

Hata hivyo, katika kujaribu kuwapima watawa wetu wa sasa na Mwalimu Nyerere haraka utaweza kujiuliza: Tanzania ingekuwaje kama Rais Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete wangeongoza miaka ya mwanzo ya uhuru?

Je, Tanzania ya Mwinyi aliyekuja na sera ya “ruksa,” Mkapa aliyekuja na ubinafsishaji na Kikwete aliyetinga na uwekezaji wa kimataifa, sasa ingekuwaje?

Pamoja na kuwa na Mwinyi kwa miaka 10, Mkapa 10 na Kikwete mitano, wananchi bado wanamuangalia Nyerere. Kwamba Nyerere aliweka maslahi ya taifa mbele.

Ndiyo maana baadhi yetu tunadhani kuwa Nyerere alikuja mapema. Kwamba angekuwa rais wetu sasa yumkini kuna mambo ambayo yangefanyika ambayo tunaona wazi hayafanyiki.

Nyerere alikuwa mbele sana kiasi kwamba hoja na nadharia zake za maendeleo zilikuwa hazina nafasi katika ulimwengu wa zama zake – japo nadharia hizo hizo leo zinakumbatiwa na mataifa makubwa na matunda yake yanaonekana.

Tukitumia kigezo cha “ruksa” kama msingi wa sera zake za kiuchumi ni wazi kuwa taifa la wakati huo lingeweza kuwa na vitu vingi kutoka nje?

Tanzania ingeweza kujitegemea katika kuzalisha baadhi ya vitu vyake kama vile nguo, viatu, mashine, viwanda na vitu vingine mbalimbali kwa sababu ya sera ya ruhusa ambayo ingevifanya kushindwa katika ushindani?

Katika hilo ni wazi kuwa Mwinyi angeendeleza sera ya kuruhusu raslimali za taifa kwa wafanyabiashara wa kimataifa. Mfano hai, ni uuzaji wa mbuga ya wanyama ya Loliondo kwa familia ya kifalme.

Naye Benjamin Mkapa kama angekuwa rais wa kwanza wa Tanganyika na baadaye Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, taifa hili lingebinafsisha karibu kila kitu kilichoachwa na wakoloni.

Chini ya utawala wake, mashirika yote ya umma yangeuzwa kwa watu waliopo karibu yake ikiwamo familia yake. Angalia upindishwaji holela wa sharia mbalimbali na udhoofishwaji wa vyombo vya dola uliofanyika katika utawala wa Mkapa utakubali kuwa hicho kingetendeka.

Angalia uuzaji wa mgodi Kiwira na suala la viwanja kadhaa vilivyopo jijini Dar es Salaam ambako Mkapa anatajwa kujimilikisha. Kwa hakika, kama Mkapa angekuwa katika kipindi hicho, angefanana na aliyekuwa rais wa Misri, Hosni Mubarak.

Angeweza kutumia maneno mazuri na ushawishi kuendeleza urafiki na nchi za magharibi, huku akiendelea kuweka mazingira magumu kwa watu wake.

Taifa lisingekuwa na majengo makubwa na majumba makubwa, huku kukiwa na tofauti kubwa ya maisha kati ya wale walio karibu na chama tawala na wale walio nje.

Mkapa kwa kweli angeweza kutuelezea mafanikio ya utawala wake, lakini wakati huo huo akiwa amesababisha kinyongo kwa maelfu ya wananchi. Tanzania ya kwanza chini ya Mkapa ingetisha.

Tusingekuwa taifa moja, watu wake wasingekuwa na mahusiano mazuri, wala mamilioni ya walalahoi wasingeweza kujenga na kuishi maisha mazuri.

Tukiangalia jinsi kundi la watu walio karibu na chama tawala walivyofanikiwa wakati wa utawala wa Mkapa, ni wazi kwamba Tanzania ya kwanza chini yake ingetengeneza tabaka kubwa – kama hili lililopo sasa. Kwamba ili ufanikiwe sharti uwe mdau na chama tawala. Hata upinzani usingekuwapo.

Na hili alilithibitisha mwaka jana kwenye kampeni ya mwisho ya Rais Kikwete pale katika viwanja vya Jangwani ambapo Mkapa alinukuliwa akisema pasipo kuuma maneno, kwamba “tuko tayari kwa serikali ya mseto Zanzibar, isipokuwa lazima serikali hiyo iongozww na CCM.”

Hadi leo hii, Mkapa hajaeleza kama CCM ndio chama pekee chenye hati ya kutawala nchini.

Kwa upande wake, Rais Kikwete asingetaka wakoloni waondoke nchini ama angejaribu kukaa nao na kuona ni jinsi gani wanaweza kumsaidia kuendesha serikali.

Wakati Nyerere katika zama zake alikuwa anahangaika kwenda kwa wakubwa kudai uhuru, Kikwete bila ya shaka angeweza kwenda zaidi kutafuta misaada bila kujali kama kuna uhuru au la.

Sera zake za uwekezaji wa kimataifa zingesababisha ujio wa makampuni makubwa kuingia katika sekta nyeti chini ya mikataba mibovu.

Inafahamika kuwa Kikwete amekuwa waziri wa fedha na amekuwa waziri wa Nishati na Madini. Ni katika kipindi chake mikataba mibovu kama ule wa kuzalisha umeme wa njia ya mafuta wa IPTL na uchimbaji wa dhahabu katika baadhi ya migodi ilifungwa.

Hivyo basi, tungeweza kusema kabisa kuwa angekuwa ni rais ambaye anajua matatizo ya sekta hizo vizuri zaidi. Lakini tukiangalia anavyoshughulikia sekta ya fedha au nishati na madini na hasa hizi taarifa za juzi za watumishi wa kampuni inayomilikiwa na serikali kutuhumiwa kushiriki katika utoroshaji wa wanyama hai usiku wa manane, hatuna budi kufikia hitimisho la kuogofya.

Sijui kama miaka hamsini baadaye tungekuta simba na pundamilia katika mbuga zetu.

Lakini upande mwingine wa kutisha zaidi ni kuwa uvumilivu wake wa maneno ya kichochezi ambayo yamekuwa yakitolewa katika mazingira ya kidini na hasa kuruhusu sumu ya udini na ukabila kumwaga kwenye vyombo vya habari ni wazi kuwa kama yeye ndiye angekuwa rais miaka ile ya mwanzo tunajua wapi taifa hili lingekuwepo.

Angebakia “kukemea udini” huku akiwalinda wa dini wa zama hizo na matokeo yake kungekuwa na mgongano mkubwa kati ya Wakristu na Waislamu – kama ambao naweza kuuona unazidi kujengwa taratibu.

Kwa vile ni muumini wa uwekezaji mkubwa wa mataifa ya kigeni na mtu ambaye anaamini kuwa wawekezaji wanatupenda sana na kwa vile ni mtu ambaye hataki kuchukua hatua kushughulikia sumu za udini na ukabila – zaidi ya kunung’unika kama mtu asiye na madaraka – Tanzania ya Kikwete ya wakati huo ingekuwa ni kama Nigeria.

Upande mmoja taifa linaonekana kufanikiwa (mabarabara ya juu kwa juu, mabilionea bwelele na vyuo vikuu vya kila aina – huku likisheheni matapeli wenye PhD) lakini upande mwingine taifa lililogawanywa kwa misingi ya kidini na kikabila.

Katika Tanzania hiyo ya mwanzo ya Kikwete mgongano kati ya watu wa dini mbalimbali na makabila mbalimbali ungezidi kukuzwa na yeye asingeweza kuchukua hatua yoyote kwa kuogopa kuonekana mdini.

Ni kwa sababu hiyo basi, ninapowaweka marais hawa watatu na jumla ya mambo yote waliyoyafanya na kuwapima kwenye mizani huko upande mwingine yuko Nyerere, naweza kusema kuwa Nyerere anawazidi kwa uongozi. Hata wao wanakiri hilo.

Mipango na sera za Nyerere vilisimama kama ushahidi wa mashtaka mazito dhidi ya viongozi waliokuja kumrithi watatu hawa. Na ninaamini kuwa majina yao yatasahauliwa katika histori na onawezekana kizazi kijacho kitawasahau haraka ila Nyerere atakumbukwa zaidi na kupendwa zaidi.

Ni kwa sababu hiyo, jaribio la kuliharibu jina la Nyerere halitofanikiwa. Nyerere bado anasimama kama alama ya makosa ya watawala wa sasa.

mwanajijiji@jamiiforum.com
0
Your rating: None Average: 4 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: