Wanyarwanda wapata ‘koloni’ Muleba


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 23 November 2011

Printer-friendly version

WAFUGAJI wa Kinyarwanda wamevamia mkoa wa Kagera na sasa wanajigamba kuwa wana “koloni” katila wilaya ya Muleba.

Wakiwa na ng’ombe wao wenye pembe ndefu wa aina ya “ankole;” Wanyarwanda wametapakaa katika kata ya Rutoro wilayani Muleba.

“Wanalisha ng’ombe wao kule wanakotaka; hata katika mashamba yetu. Ukiwaambia wanakujibu haraka: ‘Hili koloni letu,’” anaeleza mkazi mmoja wa Rutoro.

Wanyarwanda wako katika eneo lililokuwa likimilikiwa na Ranchi ya Taifa (NARCO) na vijiji vya jirani.

Taarifa zilizopo zinaeleza kuwa NARCO ilibinafsisha vitalu vyake vya kufungia mwaka 2006. Vilichukuliwa na wananchi. Wananchi nao wamebinafsishia vitalu hivyo kwa Wanyarwanda wenye ng’ombe.

Kuingia kwa Wanyarwanda katika eneo la Ranchi ya Kagoma, wilayani Muleba lenye jumla ya vitalu 18, kumeleta mahusiano mapya na hatari.

Wananchi wakazi wa maeneo ya ranchi wapatao 11,000 wanalazimishwa kuhama ili kutoa nafasi kwa wafugaji ambao inakadiriwa wana ng’ombe wapatao 11,908 (hesabu ya wafugaji); lakini wananchi wanakadiria kuna ng’ombe zaidi ya 40,000.

Kata ya Rutoro ina vijiji vinne vyenye jumla ya vitongoji 16. Zipo shule nne za msingi ambazo ni Rutoro, Byegeragere, Mishambya na Kyarutare.

Kinachoendelea Rutoro na ambacho tayari mbunge wa Muleba Kaskazini Charles Mwijage ameishaelezea bungeni, ni “ukatili wanaofanyiwa wananchi” katika kata hii.

Mwijage analaani “wavamizi” – Wanyarwanda kwa kuingia nchini, lakini anakerwa na polisi na baadhi ya watendaji serikalini kwa kuwalinda na kuwatetea wafugaji kutoka Rwanda.

Wakati wafugaji Wanyarwanda wanaishi – wao na mifugo yao nchini Tanzania – kwingineko nchini viongozi wa serikali wanawafukuza wafugaji wazawa wa nchi hii; wakiwaamuru “warudi makwao.”

Wakazi wa Rutoro wanaeleza kuwa wafugaji wanalipa kwa serikali ya eneo hilo Sh. 20,000 kwa kila ng’ombe kwa mwaka.

Hata kama wangekuwa wanalipa zaidi, hakuna ajuaye fika ni idadi gani ya mifugo waliyonayo Wanyarwanda na inaongezeka kwa kiasi gani.

Lakini hoja kuu ni wameingiaje nchini? Mbona hawajasajiliwa kama wahamiaji, wakimbizi au wanaosubiri kupewa uraia? Je, wanapata wapi jeuri na ujasiri wa kutukana, kubeza na hata kutishia wakazi wa miaka yote wa Rutoro?

Hoja hii inapanuka na kuleta maswali mengi zaidi. Mtu anayekuja na ng’ombe wake ndani ya Tanzania, hasa anawekeza nini?

Kwanza, hajulikani ana mifugo kiasi gani. Pili, haijulikani amekuja na watu wangapi. Tatu, anachowekeza kwa manufaa ya nchi hii hakijulikani. Huyu aweza kuitwa “mwekezwaji” badala ya kuitwa “mwekezaji.”

Hivi sasa uvumi umeenea Rutoro na wilayani Muleba – kwenye magulio na katika vilabu vya pombe – kwamba ng’ombe wa Wanyarwanda ni wa Paul Kagame, rais wa Rwanda na kwamba “analenga kukamata ardhi ya Tanzania.”

Tayari Mwijage anashikilia kuwa wavamizi ndio walichoma kanisa katika Kitalu Na. 15; moja ya matukio yanayoashiria kuvunjika kwa amani Rutoro, Muleba na hata nchi nzima.

Mbunge aliishafikisha suala hili bungeni kwa kusema, “Mheshimiwa Mwenyekiti…  nilizungumzia suala la wafugaji haramu wanaotoka nchi jirani kuja kufuga katika eneo letu na kulisha mifugo kwenye mashamba ya wananchi.

“Ningetaka… kujua serikali inatusaidiaje kwa kuwa watu wa Kagera wameniagiza niiombe serikali itoe msaada wa Jeshi la Wananchi,” anasomeka Mwijage katika kumbukumbu za bunge (hansard) ukurasa 186 kwa mkutano wa bunge la bajeti, 27 Julai 2011.

Naye Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, David Mathayo anarekodiwa na hansard akisema, “Mheshimiwa mwenyekiti, kilio chake (Mwijage) ni halali kabisa. Sisi hatuwezi kwenda Rwanda wala Burundi kufuga kule kwao na wala Uganda! Kwa hiyo si halali kwa watu kutoka nje na kuvamia eneo letu.”

Miongoni mwa matukio ya kustusha ambayo yanahusiana na “uvamizi wa Rutoro,” ni lile la mwalimu wa Shule ya Msingi Kyarutare kupigwa risasi na polisi wanaodaiwa “kukodishwa” na mmoja wa wahamiaji haramu ili kuwadhibiti wananchi wanaopinga mifugo kulishwa kwenye mashamba yao.

Inadaiwa Mwalimu Filbert Paulo (33) alipigwa risasi na polisi mnamo Aprili 27 mwaka jana. Ilikuwa katika kijiji cha Kyobuheke ambako wananchi walikuwa wakipinga wavamizi kulisha mifugo yao katika eneo la Shule ya Msingi Kyarutare.

Katika tukio hilo, Mwalimu Filbert alipigwa risasi kifuani kushoto. Iliripotiwa kuwa watu wengine walijeruhiwa kwa kipigo cha polisi.

Filbert alilazwa hospitali teule ya Rubya na baadaye kuhamishiwa hospitali ya Kagondo ili awe akitibiwa wakati akifundisha Shule ya Msingi Kagondo.

Wakati akiuguza majeraha katika hospitali  Teule ya Rubya wilayani Muleba ambako alikimbizwa muda mfupi baada ya kupigwa risasi, polisi walimfungulia keshi wakidai  alikaidi kutiwa mbaroni pamoja na kusababisha watu wengine kujeruhiwa.

Hata hivyo, Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Muleba, C.F Waane alifuta kesi hiyo (Na. 168/2010), hapo Mei 27 baada ya polisi “kushindwa kujitokeza mahakamani na bila taarifa” kwa kipindi kirefu.

Taarifa za kitababu za hospitali ya Rubya na baadaye Bugando ambako mwalimu huyo alitibiwa, zinathibitisha kuwa alipata madhara makubwa kutokana na majeraha ya risasi.

Rekodi za hospitali zinaonyesha kuwa matatizo ya Filbert ya kupumua kwa shida “…yanasababishwa na majeraha aliyoyapata baada ya kupigwa risasi na polisi.”

Maelezo ya daktari yanaonesha kuwa alikuwa amelowa damu, mlegevu na alionesha kupauka alipofikishwa hospitalini baada ya kupigwa risasi.

“Kuna jeraha la sentimita 10 ambalo huenda linahusisha misuli na mfupa kwenye mkono wake wa kushoto; na majeraha madogo yaliyosambaa urefu wa sentimeta 15 juu na ? sentimeta kwenda ndani” inasomeka sehemu ya taarifa ya uchunguzi wa daktari uliofanyika hospitali ya Rubya muda mfupi baada ya kupigwa risasi na polisi.

Naye mkazi wa eneo hilo aliyefahamika kwa majina ya Chrisostom Mutahyabarwa alijeruhiwa kwa risasi kwenye bega la kushoto.

Mwalimu Filbert bado ana maumivu huku polisi waliosababisha unyama huo wakiwa bado hawajachukuliwa hatua yoyote ya kisheria.

Wakati polisi wanadai kuwa walimpiga risasi Filbert kwa kuwa alitaka kukimbia ili kuepuka kukamatwa, kuna taarifa kuwa alipigwa risasi akiwa amefungwa pingu mikono yake yote miwili.

Isitoshe, wakati wa tukio hilo polisi wanadaiwa kuwakamata watu 23 baada ya kutembeza kipigo; wakikabiliana na wananchi kwa shabaha ya kulinda wavamizi.

Waliokamatwa usiku wa tukio, waliswekwa rumande mjini Muleba na kuachiwa siku ya nne bila maelezo yoyote na ikabidi watembee kwa miguu karibu kilometa 250 hadi Rutoro.

Baadhi ya waliotiwa mbaroni wamedai kuwa imekuwa kawaida kwa polisi wilayani Muleba kukamata watu kiholela na hatimaye kuwasweka ndani kwa “mashtaka ya kubambikiza.”

Machi mwaka huu, wananchi wilayani Muleba walimpokea Waziri Mkuu Mizengo Pinda kwa mabango. Walikuwa wakilalamikia polisi kuwabambikizia kesi.

Polisi walijitahidi kuwatimua wananchi na kuchana mabango yao kabla ya kuwasili kwa waziri mkuu lakini wananchi hawakuishia hapo. Wakati wa kuwasilisha hoja mbalimbali kwa waziri mkuu; bado wananchi walieleza kero zao kuhusiana na polisi.

Ilikuwa baada ya ziara ya Pinda, baadhi ya maafisa wa polisi wilayani Muleba, akiwamo mkuu wa polisi wa wilaya (OCD) na Afisa wa Upelelezi (OCCID) walihamishwa.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Ardhi na Maji nayo ilitembelea Rutoro kwa ombi la  mbunge wa Muleba Kaskazini.

Wakati wa mkutano wa hadhara, kwenye shule ya msingi Rutoro, tarehe 1 Novemba mwaka huu, kamati iliyoongozwa na Profesa David Mwakyusa, ilielezwa taarifa za kusikitisha ambazo zilifanya baadhi ya wabunge kububujikwa machozi.

Alikuwa Said Mohammed aliyesimama na kueleza kuwa polisi walimbambikizia kesi na kumsweka rumande kwa karibu miezi sita. Aliporejea kutoka rumande alikuta mkewe amefariki.

Inadaiwa kuwa kifo cha mkewe kilitokana na kupigwa na “wahamiaji haramu” alipokaidi amri ya kuondoka kwenye makazi yake ili walishe ng’ombe wao.

Mohammed alidai kuwa baada ya kifo cha mkewe, watoto wao watatu waliachwa bila msaada wowote. Hali hiyo iliwahuzunisha sana wabunge kwa kuwa afya za watoto wao zilionekana kudhoofika.

Diwani wa Kata ya Rutoro, Abbakar Said Bushumbilo anasema kuwa watoto hao wamekuwa wakiishi maisha ya taabu baada ya baba yao kuwekwa rumande na baadaye mama yao kuaga dunia.

Diwani huyo alisema alijitolea kuwahifadhi watoto hao kwa kuwapa mahali pa kuishi. Watoto waliletwa mbele ya wajumbe wa Kamati ya Bunge kama kielelezo cha madhara ya ukatili unaofanyika dhidi ya raia katika kata ya Rutoro.

Hatua hiyo si kwamba iliwaacha baadhi ya wabunge wakibubujikwa machozi, bali pia ilimfanya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba, Bi. Oliver Vavunge kuagiza watoto hao kupelekwa kwake ili agharamie matibabu yao na kurejesha afya zao.

Katika mkutano huo, mama mmoja aliyejitabulisha kwa jina la Ana-Joyce Emmanuel alilalamikia vitendo vya wahamiaji haramu kuwalazimisha kufanya nao ngono ili wasilishe ng’ombe kwenye mashamba yao.

Alidai anajua matukio kadhaa ya baadhi ya akinamama wanaodaiwa kubakwa wakati wa kadhia hiyo.

Mbunge Mwijage alikuwa miongoni mwa viongozi waliofuatana na kamati ya bunge. Katika hatua ya kupinga wananchi wake kunyanyaswa na anaowaita “wavamizi kutoka Rwanda,” alisusa hafla ya chakula cha mchana iliyokuwa imeandaliwa na kampuni ya Ranchi ya Taifa kwa ajili ya wabunge.

Mwijage anasema aligomea chakula hicho ikiwa njia ya kupeleka ujumbe kuwa hawezi kula chakula kilichoandaliwa na watu ambao kwa kiwango kikubwa wanahusika na uonevu unaoendelea dhidi ya raia wakazi wa Rutoro.

Tukio la mbunge huyo kugomea chakula lilikuja siku chache baada ya kudai kuwa endapo serikali haitasikiliza kilio cha wananchi na kutatua matatizo yao, basi angeachia wadhifa wake wa ubunge.

Mwijage amesema tayari amekabidhi kwa waziri mkuu, kanda yenye picha zinazoonyesha wananchi wanavyoteseka katika nchi yao, na kumweleza mengi, ikiwa ni pamoja na mwalimu aliyepigwa risasi na polisi.

Balozi Hamis Kagasheki, naibu waziri wa mambo ya ndani, anasema alikuwa hajapata taarifa juu ya tukio linalohusisha mwalimu na polisi na kwamba ndio alikuwa analipata kutoka kwa mwandishi.

Hata hivyo, amesema inawezekana hilo ni moja ya matukio ya aina hiyo ambayo huhusisha polisi wenye mienendo mibovu na ambao hutuhumiwa katika matukio mbalimbali dhidi ya raia.

Amesema jeshi la polisi nchini limejitahidi kuchukua hatua dhidi ya vitendo vya unyanyasaji unaofanywa na baadhi ya maafisa wake, hususan walioko mikoa ya pempezoni ikiwamo Kigoma na Kagera.

Alisema miongoni mwa hatua zilizochukuliwa kukabiliana na mienendo mibovu ya baadhi ya askari ni pamoja na kuhamisha na kuwaachisha kazi baadhi yao.

Katika hotuba yake kwenye Bunge la Bajeti mwaka jana, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Shamsi Vuai Nahodha alitoa takwimu zinazoonyesha malalamiko ya wananchi dhidi ya uonevu wa polisi.

Waziri Nahodha alisema kuwa wizara hiyo ilikuwa imepokea malalamiko 300 katika kipindi cha 2010-2011 na kwamba kati yake malalamiko 150 yalikuwa ya kubambikiziwa kesi.

Katika taarifa iliyotolewa na Afisa Mtendaji wa kata ya Rutoro, Josephat Kweyamba wakati wa ziara ya Kamati ya Bunge ya Kilimo, Maji na Mifugo, watu wanane wamejeruhiwa kwa risasi za moto na polisi mwaka huu.

Aidha, taarifa hiyo inaeleza kuwa watu 32 wamefukuzwa kwenye maeneo yao karibu na kitalu Na. 3 wakati wananchi wapatao 21 walilalamikia kuharibiwa kwa mashamba  yao.

Wananchi wengine tisa wanadaiwa kuwekwa ndani kwa siku tatu baada ya kukamatwa na hatimaye kuachiwa bila kufunguliwa mashtaka.

Taarifa hiyo ya mtendaji, ambayo pia ilitiwa saini na diwani wa kata hiyo, Abbakar Bushumbilo inaonyesha kuwa watu wawili,  Bukuru James na Method Bidimba, walipotea katika mazingira ya kutatanisha.

Joas Kaijage ni mwandishi wa The Citizen
0
No votes yet