Wapelelezi wa SFO waiumbua TAKUKURU


Stanislaus Kirobo's picture

Na Stanislaus Kirobo - Imechapwa 13 May 2008

Printer-friendly version

HAKUNA ubishi kuwa "ufisadi" ni neno lililochukua nafasi kubwa zaidi magazetini katika awamu hii ya uongozi wa nchi kuliko huko nyuma.

Hata Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, anayetetea uamuzi wa serikali wa kushindwa kufikisha watuhumiwa ufisadi mahakamani, anafahamu hili.

Katika kipindi cha miezi 28 ya uongozi kwa Rais Jakaya Kikwete, ufisadi limetamkwa na kuandikwa mara nyingi zaidi.

Wakati hiyo ndiyo hali halisi, inaonekana Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) yenye dhamana ya kuchunguza na kuchukua hatua kukomesha ufisadi, inafanya dhihaka kubwa.

Inachofanya TAKUKURU ni kupiga kelele zaidi na kujipipendekeza. Na hilo hawawezi kulipinga kwa sababu hawawezi kuonyesha vinginevyo kwa wananchi.

Viongozi wa TAKUKURU hawawezi kujitapa kuwa wanafanya kazi waliotumwa bila kutaja idadi ya kesi za vigogo ambazo wamezisimamia na wahusika kufikishwa mahakamani, achilia mbali kutiwa hatiani na mahakama.

Mfano mzuri ni uchunguzi wa sakata la rada. Hapa ndipo TAKUKURU inapoonekana kioja.

Katika sakata hili, wajanja wachache serikalini wameshirikiana na mfanyabiashara wa kiasia, na kufanikiwa kuingiza mkenge serikali kwa kuizia mtambo huo wa kuongozea ndege kwa bei kubwa ya dola za Marekani 36 milioni, sawa na zaidi ya Sh. 40 bilioni za Tanzania.

Pamoja na taasisi nyigi za ndani na nje ya nchi, zikiungwa mkono na Benki ya Dunia (WB), walipinga mradi huo kwa hoja kwamba unaliangamiza taifa; bado TAKUKURU ilikuwa imelala usingizi mnono.

Pamoja na kwamba kulikuwa na kila dalili za wakubwa kutafuna mlungula katika sakata zima la mkataba, bado TAKUKURU haikuwa na meno ya kusaka wahusika.

Si hivyo tu, TAKUKURU hawakuweza kusikiliza vilio wala manung'uniko ya wananchi.

Kukurupuka kwa taasisi hii, kumekuja pale shirika la Uchunguzi wa Makosa ya Jinai nchini Uingereza (Serious Fraud Office -SFO), lilipoanza kulichunguza suala hilo.

Katika uchunguzi huo, SFO walilazimika wahusika kuja hapa ambako rada ndiko ilikouzwa; mamlaka ya nchi hii haikuweza kuwakatalia kuingia nchini kwa hofu ya kukatiwa misaada kutoka Uingereza.

Lakini haiyumkiniki iwapo TAKUKURU walitoa ushirikiano wa kutosha. Hii ni kwa sababu kama inavyodhirika sasa, wapo baadhi ya wakubwa katika serikali wametajwa kupokea milungula kwa lengo la kufanikisha dili hiyo.

Bila shaka maafisa wa SFO walishangaa sana kuwakuta wenzao wa Tanzania (TAKUKURU) hawana hata jalada la kuonyesha kile nao walichokuwa wanatarajiwa wakifanye upelelezi wa dili hiyo. Hakika, ni aibu tupu.

Hii inaeleweka, kwani serikali nzima ilikuwa haina ari ya kuchunguza sakata hili. Hata Rais Jakaya Kikwete, alipokuwa ziarani Uingereza mwaka 2006 aliwahi kutamka kwa Watanzania waishio huko kwamba sakata la rada ni lao Waingereza, si la Tanzania.

Alisema kama wakosaji ni kampuni ya BAE, ambayo iliiuzia rada hiyo Tanzania. Tayari imedhirika kwamba rais Kikwete hakuwa sahihi, kwani walioingizwa mjini ni sisi watanzania.

Wapo wanaosema, Kikwete alilazimika kutoa kauli hiyo, ili kulinda marafiki zake ndani ya serikali ambao muda si mrefu wataanza kumbuliwa.

Kuanzia wakati huo ndipo TAKUKURU ikaanza kuonekana nayo ni mshiriki mkuu? wa SFO katika uchunguzi huo. Lakini hakuna ubishi kwamba sifa za matokeo ya upelelezi huo zinatokana na jitihada kubwa za Waingereza.

Hii ni aibu kubwa. Maana Waingereza ndiyo wanaonekana wanauchungu sana na mustakabli wa nchi hii kuliko hata viongozi wetu. Matokeo ya hali hiyo, tayari tumeanza kuyaona. TAKUKURU na serikali zimeanza kuvuliwa nguo.

Tayari Waziri wa Miundombinu, Andrew Chenge, amehojiwa na kupekuliwa. Kuna taarifa kwamba amekutwa na dola zaidi ya milioni tano (Sh. 6.5 bilioni) kwenye akaunti zake mbalimbali nje ya nchi.

Kufuatana na taarifa za SFO, fedha hizo zinashukiwa kuwa ni mlungula wa dili ya rada.

Wanang'ang'ania hivyo kutokana na jinsi mlolongo wa uhamishaji wake ulivyokuwa baina ya Uingereza, Uswisi na kisiwa cha Jersey. Chenge mwenyewe amekanusha kuwa fedha hizo zinahusiana na dili ya rada.

Taarifa za SFO zinasema bado anatafutwa mtuhumiwa mkuu katika dili hiyo, Saileshi Vithlani. Huyu ni Mtanzania anayedaiwa ana uraia pia wa Uingereza.

Taarifa zinasema, Vithlani ndiye aliyepewa dola za Kimarekani zaidi ya 12 milioni kutoka kwa kampuni ya BAE. Fedha hizo ziliingizwa katika akaunti yake ya Uswisi kama "kamisheni"? kwa kufanikisha dili.

Kiasi hicho cha fedha kwa mujibu wa sheria za Uingereza hakiwezi kuwa kamisheni. Ni wazi kwamba hizo ni fedha za mlungula.

Kwa sheria za Uingereza, kamisheni halali ya dili kama hiyo, ni asilimia tatu. Kwa hali hiyo, Vithlani alitakiwa kulipwa karibu dola 400,000 milioni (zaidi ya Sh. 600,000) ambazo tayari alikuwa amekabidhiwa.

Kwa hivyo, SFO (inasemekana pamoja na Tanzania) inamtafuta Vithlani, na Taasisi ya Polisi Duniani (Interpol) imearifiwa kumkamata ili aeleze ni akina nani hasa aliwagawia dola hizo 12 milioni.

Tanzania, kwa maana ya TAKUKURU, haiwezi kuwa inamtafuta Vithlani kwa dhati, hilo nalikataa kabisa. Ni kwa sababu Vithlani ni mtu anayeweza kuja kuiumbua serikali. Hapa ndipo anapoweza kutaja vigogo aliokula nao pamoja mabilioni hayo ya fedha.

Isitoshe Vithlani aliwahi kutiwa mbaroni na TAKUKURU mwaka jana ambapo walimfikisha mahakamani kwa "kusema uongo"? kwa wapelelezi na baadaye akatoweka nchini katika mazingira ya kutatanisha.

Yumkini wapelelezi wa SFO waliwashangaa sana wenzao wa TAKUKURU kwa kumwachia shahidi mkubwa kabisa katika kesi hiyo.

Haifahamiki ni kiasi gani viongozi wa TAKUKURU walilipwa na Vithlani ili "kufakisha dili la kumwachia huru." Lakini bila shaka walilipwa.

Kutoroka kwake bila shaka kulipangwa, kwa sababu serikali haitaki kuwapo kwake nchini. Ni kama vile aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu (BoT), Daudi Ballali, asivyotakiwa na wakubwa nchini.

Balali huku serikali ikujua kwamba ni mtuhumiwa muhimu katika sakata la wizi wa mabilioni ya shilingi katika akaunti ya EPA, serikali haijihangaishi kumtafuta.

Bila shaka baadhi ya wakubwa ndani ya serikali wanaogopa kutajwa juu ya jinsi walivyohusika na kadhia hiyo.

Ni wazi kwamba serikali haitaki kabisa kuwapo kwa Balali nchini. Na hata kauli ya TAKUKURU kwamba inapeleleza suala hilo, bado ukweli utabaki palepale kwamba hahitaji nchini kwa hofu ya kuumbua wakubwa.

Ndiyo maana Kamati maalum inayoongozwa na Mwanasheria Mkuu wa serikali, Johnson Mwanyika haisemi chochote iwapo inafanya jitihada zozote za kumtafuta, na kama wanafanya, jitihada hizo zimefikia wapi.

Kwa hivyo basi, iwapo Ballali atapatikana, basi hata huyu Vithlani atapatikana. Lakini kamwe haiingii maanani iwapo hayo yatatokea.

Lakini hili halishangazi sana kwa taasisi kama TAKUKURU ambayo kama nilivyotaja hapo awali, haina utamaduni wa kufanikisha uchunguzi wowote wa ufisadi unaohusu wakubwa. Siku zote, TAKUKURU inataka ionekane tu inafanya kazi, ijapokuwa moyoni hakuna kitu.

Tumeona uchunguzi wa Richmond na namna walivyojaribu kumsafisha aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa. Tumeona hili la EPA na sasa tunashuhudia uchunguzi huu wa rada.

Hakika, ukiacha hili la rada, mengine yote yaliobakia, TAKUKURU haiwezi kufanya kazi, zaidi ya watanzania kushuhudia danadana na porojo.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: