Wapinzani kupingana ni kwa faida ya nani?


editor's picture

Na editor - Imechapwa 17 November 2010

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

KWA kipindi kirefu tangu uanzishwe mfumo wa vyama vingi nchini, vyama vya siasa vya upinzani vimekuwa vikikutana, kujadiliana na kutangaza kushirikiana.

Vyama hivyo vilitoa tamko la ushirikiano mwaka 1995, lakini ulipokaribia uchaguzi vilifarakana na kutoleana shutuma.

Katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2000, viongozi wa vyama hivyo walitokea wameshikana mikono wakisisitiza kuwa na umoja, lakini ulipowadia uchaguzi walihitilafiana kila chama kikaondoka na msimamo wake.

Wakati vyama vya upinzani vikikorofishana kutokana na hisia za kusalitiana, chama tawala- CCM-kimekuwa kikinufaika na kujiimarisha. CCM imekuwa ikitumia kumeguka kwa kambi ya upinzani kama kigezo kikuu cha kushawishi wananchi wasichague upinzani.

Wapinzani walihitilafiana katika chaguzi zote ndogo za mwaka 2008 na 2009 na kuiacha CCM ikizoa ushindi wa kishindo katika majimbo ya Busanda, Biharamulo na Mbeya Vijijini.

Mwaka huu, wakati wananchi wakionekana kuchoshwa na uongozi wa CCM, wapinzani ndio wakawa wa kwanza kujibomoa wakakataa kushirikiana na kuachiana majimbo na kata.

Kwanza kila chama kilijifanya kinapendwa na wananchi na pili kilijiona kina uwezo wa kutoa gharama zote za usimamizi wa uchaguzi. Matokeo yake, vyama takriaban vyote vya upinzani vimepigwa kumbo.

CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi wanaweza kujiona wana nafuu kwani vimepata viti vya udiwani na ubunge, lakini vimeingia gharama kubwa za fedha kwa ajili ya mawakala.

Kitu kinachosikitisha ni kwamba, baada ya uchaguzi kumalizika, vyama vya upinzani ndivyo vimekuwa vya kwanza kutoa taarifa za kuwafikisha mahakamani washindi wengine wa upinzani kwa madai ya kuporwa ushindi.

Tunajua kwamba kila chama kina haki za msingi katika uchaguzi na kingependa kushinda, lakini ni kwa faida ya nani wapinzani kwa wapinzani kufikishana kortini? Ni kweli kwamba maeneo yenye hitilafu ni yale ambayo wapinzani wameshinda?

Pamoja na vyama kuwa na haki kuhoji matokeo katika uchaguzi mkuu na ikiwezekana kuomba yatenguliwe, wajue kwamba wanayemnufaisha ni CCM.

Chama tawala ndicho, wakati wote, kimenufaika na msuguano au mvutano wa wapinzani, maana kama kunguru, CCM inafurahia vita vya panzi—wapinzani kwa wapinzani.

Tunajua kwamba kila chama kina sera zake, msimamo wake na taratibu tofauti na vingine, lakini ni vyema vikajitazama upya, vikajiuliza tena wapinzani kupingana ndani ya bunge na kushitakiana ni kwa masilahi ya nani? Wajue anayenufaika ni mpinzani wao mkuu CCM.

0
No votes yet