Warioba anajua sheria si ufisadi


Kondo Tutindaga's picture

Na Kondo Tutindaga - Imechapwa 09 November 2011

Printer-friendly version
Kisima cha Mjadala

WAZIRI Mkuu mstaafu, Joseph Sinde Warioba sasa ameibua mjadala mpya. Akiongea kwenye hafla ya uzinduzi wa mpango wa miaka mitano wa chama cha majaji wastaafu, Jaji Warioba alisema mambo mawili.

Kwanza, alidai ni sharti serikali ilipe wezi wa fedha za umma – Makampuni ya Dowans Holding Ltd, Dowans Tanzania Ltd na dada yao, Richmond Development Company (RDC) – ili kulinda utawala wa sheria na kwamba waliohusika na mikataba hiyo wawajibishwe.

Pili, Jaji Warioba ameendelea kulalamika kuwa serikali iliyopo madarakani, imeshindwa kufikisha watuhumiwa wakuu wa ufisadi mahakamani.

Kwa miaka kadhaa sasa, Jaji Warioba amekuwa akilalamika hadharani juu ya kushamiri kwa rushwa nchini. Msimamo wake huo, umemuingiza katika mahusiano tete na watawala na hata wakati fulani kutuhumiwa ufisadi.

Mpaka sasa, si watawala wala Warioba waliojitokeza hadharani kueleza kinachoendelea kuhusu tuhuma zinazomkabili mwanasiasa huyo. Kimya hiki kinaweza kuwafanya baadhi ya watu, nikiwamo mimi, kuamini mabadiliko ya ghafla ya misimamo ya Warioba kuhusu ufisadi, yanatokana na kinachoendelea kati yake na watawala. Hilo likitokea litakuwa moja ya majanga ya kitaifa na ninamwomba Mwenyezi Mungu aliepushe.

Jaji Warioba ni mwanasheria. Anajua ni jinsi gani utawala wa sheria unavyokiukwa katika taifa hili kwa watu wachache wenye fedha chafu, kupata haki dhidi ya wengine. Anajua kwamba fedha zinaweza kununua chochote katika nchi hii. Anajua na kwa hakika, bado anakumbuka jinsi mpinzani wake kwenye kinyang’anyiro cha ubunge mwaka 1995 jimboni Bunda, Steven Wasira alivyotumia fedha kushinda.

Anakumbuka jinsi ilivyomchukua muda na fedha nyingi kupata haki yake mbele ya utawala wa sheria anaoutetea. Anajua kilichotokea siku ile ya uchaguzi wakati alipoamua kwenda kulala nyumbani kwake Nyamuswa.

Anajua ni kwa nini tangu wakati huo, alimua kutogombea tena ubunge. Je, utawala huo wa sheria ambao Warioba anautetea ili uheshimiwe katika kesi ya Dowans?

Kiasi cha fedha kinachodaiwa si ajabu ni kikubwa kuliko bajeti nzima inayoendesha idara ya mahakama na kwa hiyo wanaodai wanaweza kuwa wameishawanunua watoa haki wetu bila hata watoa haki kutaka.

Warioba si mgeni katika mambo haya, anajua kuwa katika mataifa yanayokua kama hili, utawala wa sheria siyo makini na dhabiti kuweza kuhimili vishindo vya watawala wasio na maadili mema.

Matahalani tuchukulie mfano, kwamba baadhi ya watawala wetu wana maslahi binafsi katika suala la Dowans; yaani mkuu wa nchi mwenyewe angekuwa na maslahi katika mkataba ununuzi wa Richmond iliyoizaa Dowans. Na kwamba wasaidizi wa mkuu wa nchi wanalijua hilo, lakini wamepata kutunza siri na utii kwake. Wasimamizi wakuu wote wa vyombo vya dola na usimamizi wa utawala wa sheria wakajua hilo, lakini kwa sababu ya utii na viapo wakakaa kimya.

Je, ni nani anaweza kumfunga kengele mkuu wa nchi mwenye maslahi katika Dowans ikiwa chama tawala yeye ni mwenyekiti, baraza la usalama yeye ni mwenyekiti, mahakama kuu yeye ni mteuzi, majeshi yote yeye ni jemedari mkuu, wazee wastaafu wote wenye maneno maneno, yeye ndiye mlipaji wa pensheni zao!

Huo ni mfano mdogo sana lakini iko mingine ambayo Warioba anahitaji ama afike mahali akae kimya au awaache wanaharakati wafanye kazi yao kwa sababu, wengi wao ni vijana kuliko yeye na mzigo wa deni la Dowans ni juu yao zaidi kuliko ulivyo juu yake na wazee wa aina yake.

Jambo jingine ambalo napenda nimkumbushe Warioba, ni ukweli kuwa maadili ya uongozi katika taifa hayapo kwa sasa. Watu wanatumia nafasi za uongozi kujinufaisha na yeye amekuwa msitari wa mbele kulipigia kelele suala hili.

Kutokana na kukosekana kwa maadili na miiko ya uongozi, ndiyo maana Dowans tunayoizungumzia, si mali ya wafanyabiashara, bali ni mali ya viongozi wetu waliojifanya ni mawakala wa makampuni ya nje. Kwa hiyo deni hilo linalipwa kwa makampuni ya nje yanayomilikiwa na viongozi wetu wa ndani.

Kila kukicha tumeshuhudia baadhi ya viongozi wakigeuka wabia na makampuni ya nje na ndiyo maana hata Warioba mwenyewe amejikuta anahusishwa na baadhi ya kashfa ikiwamo ile ya kampuni ya Mwananchi Gold Mining.

Uongozi bila maadili na bila miiko unawachafua hata baadhi ya “watakatifu” tuliokuwa tunawaheshimu. Inapofika mahali kiongozi kama Warioba anatoa matamshi yanayoweza kutafsiriwa kuwa anawatetea mafisadi, siku hiyo inageuka kuwa siku ya kilio kwa Watanzania wengi walio maskini kutokana na kuporwa kwa raslimali zao. Haya yote yanafanyika mbele ya utawala wa sheria anaoutetea.

Kwa macho yetu na masikio tumesikia wiki iliyopita kuwa kamati mbalimbali za Bunge zikiibua kashfa za ufisadi kila ofisi ya umma. Orodha ni ndefu kuanzia Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA), Bodi ya Pamba, mamlaka ya korosho, halmashauri za wilaya, bodi ya utalii na kwingineko.

Kinachowakatisha tamaa waliowengi, ni pale baadhi ya wabunge wanapoibua ufisadi bila fisadi; yaani wanaona uporaji lakini mporaji haonekani. Huu ufisadi usio na fisadi ndio huo huo tunaolalamikia katika Dowans.

Mkuu wa nchi anadai hawajui Dowans, lakini ni Dowans hao hao walioweka mkataba wa mabilioni ya shilingi na serikali kupitia shirika la umeme la taifa (Tanesco). Mkuu wa nchi anadai hawajui Dowans, lakini ni Dowans inayouza umeme kupitia kampuni ya Symbioni. Je, utawala wa sheria anaodai Warioba uko wapi hapa? Au kule mwizi anapokuibia kisha akakuuzia kile alichokuibia, huo ndiyo utawala wa sheria?

Nimebaki najiuliza hivi fisadi yuko wapi sasa ikiwa Warioba anataka watumishi walioweka mikataba ndio wawajibishwe? Yaani aliyesahau kufunga mlango na mwizi akaingia na kuiba ndiye awajibike, lakini mwizi aachwe afaidi mali aliyoiba?

Naelewa umuhimu wa kuwajibisha watendaji wa serikali, lakini tusiishie hapo. Ikifanyika kama Warioba anavyoshauri ni sawa na kusema watu wana ruhusa ya kutuibia na sisi tusihangaike nao bali tuhangaike na tuliowaweka kulinda. Hili lina maana lakini si yote na si kamili. Mzee wetu anapaswa aishi kama asemavyo.

Kinachoonekana kuendelea katika taifa letu ni kuwa ufisadi ni dhana ya kufikirika ikiwa wazee kama Warioba wataugeuka mkondo wa mabadiliko na kuanza kutuimbisha wimbo wa utawala wa sheria.

Watanzania hawa wanajua kuwa yapo majengo ya mahakama, mapya na yaliyochoka; wapo mahakimu na majaji; wanajua kuwa yuko waziri wa sheria asiyejua sheria. Wanajua pia kuwa yuko mwanasheria mkuu wa serikali asiyeishauri serikali mambo ya sheria bali anaishia kuishauri serikali jinsi siasa inavyoweza kuongoza sheria.

Lakini zaidi ya hapo, Watanzania wanajua kuwapo kwa vitu na watu hao, haina maana kuwa kuna utawala wa sheria. Utawala wa sheria unaodaiwa kuwapo ni ule unaowalinda matajiri na watu mashuhuri kama yeye. Watu maskini na raslimali za taifa havina mtetezi katika utawala wa sheria nchini.

Nimalize kwa kumtaka radhi mzee Warioba ikiwa katika “jazba” yangu nimemkwaza. Utawala wa sheria uliobaki hapa nchini unanipa uhuru wa kutoa maoni yangu yasiyoleta mabadiliko yoyote.

Hii haina maana kuwa sina imani katika utawala wa sheria kama upo- la hasha. Utawala wa sheria unaoweza kumkamata Warioba kama amekosea na kumtia ndani nautaka. Hivi sasa hatunao. Tulio nao ni ule wa kumpa shikamo Warioba kwa kuwa ni maarufu na kisha kumwomba akubali kuhojiwa kama amefanya makosa.

Tuliobaki, hata kuambiwa kosa hatuambiwi na mpaka tufike polisi, tunakuwa tumeota nundu kwa mateke na virungu.

tutikondo@yahoo.com
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: