Warioba kuongoza tume ya katiba


Jacob Daffi's picture

Na Jacob Daffi - Imechapwa 29 February 2012

Printer-friendly version

JAJI Joseph Warioba ametajwa kuwa ndiye atakuwa mwenyekiti wa Tume ya kukusanya maoni ya katiba mpya nchini, MwanaHALISI limeelezwa.

Taarifa za ikulu jijini Dar es Salaam na mjini Dodoma zinasema Rais Jakaya Kikwete atamtangaza Jaji Warioba wakati wowote kuanzia sasa.

Vyanzo vya taarifa vinasema Rais Kikwete alitaja jina la Warioba kwa mara ya kwanza katika mkutano wake na kamati ya wabunge sita wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mjini Dodoma.

Mkutano kati ya Rais Kikwete na wabunge wa CCM, ulifanyika Jumatatu, ya tarehe 6 Februari 2012. Ilikuwa katika juhudi za kuzima kilichoonekana kuwa “maasi” ya wabunge.

Baadhi ya wabunge wa chama hicho walikuwa wamechachamaa wakidai hawatapitisha marekebisho ya Sheria Na. 8 ya Mabadiliko ya Katiba ya Mwaka 2011.

Aidha, mtoa taarifa amesema Rais Kikwete alizungumzia uteuzi wa Warioba alipokutana na kiongozi mmoja mwandamizi serikalini ambapo amenukuliwa akisema amefikiria sana mtu wa kuteua ili kuongoza tume ya katiba na kwamba anaona “Warioba ndio chaguo sahihi.”

“Hili la Warioba kuwa mwenyekiti wa Tume ya kukusanya maoni, rais alitueleza tukiwa Dodoma tulipokwenda kumuona kuhusiana na mapendekezo ya marekebisho ya sheria ya kuanzisha mchakato wa kupata katiba mpya.

“Kwa hiyo, kama na wewe umelisikia, basi habari ndiyo hiyo,” mtoa taarifa aliliambia gazeti hili. Huyu alikuwa mmoja wa wabunge wa CCM aliyekuwa miongoni mwa wabunge sita waliokutana na rais.

Kwa mujibu wa mtoa taarifa, jina la Warioba lilifuatia hatua ya wabunge kugoma kuondoa, kutoka kwenye muswada wa marekebisho ya sheria hiyo, kifungu kinachozuia wanasiasa kuwamo kwenye Tume ya kukusanya maoni.

Hatua ya kukataliwa kuondolewa ibara ya 2 iliyopendekeza kuondolewa kwa maneno, “au kiongozi wa chama cha siasa wa ngazi yoyote;” na badala yake kuweka kifungu kinachoruhusu wanasiasa kuingia kwenye tume ya kukusanya maoni, inatajwa kupalilia mazingira ya kuwezesha Jaji Warioba kuteuliwa.

Mbali na kuwa waziri mkuu mstaafu, Warioba ni balozi wa nyumba kumi wa CCM katika eneo la Msasani, jambo ambalo kwa kuzingatia sheria ya awali iliyopitishwa na bunge, lingemnyima nafasi ya kuteuliwa.

Mtoa taarifa anasema kutajwa kwa Jaji Warioba kushika nafasi hiyo muhimu kwa mustakabali wa taifa, kumelenga kumnyamazisha yeye na baadhi ya viongozi wastaafu wa kitaifa ambao wamekuwa wakishambulia serikali ya Rais Kikwete kwa madai kwamba imekuwa goigoi na inaendekeza vimelea vya ufisadi.

Katika hatua ya juu ya kujikinga, baadhi ya viongozi waliokuwa wanakubaliana na Rais Kikwete, waliwageukia wenzao na hata kutishia kuwafikisha mahakamani kwa tuhuma mbalimbali.

Miongoni mwa waliotajwa kuwa huenda wangefikishwa mahakamani, ni pamoja na Warioba mwenyewe ambaye amekuwa akituhumiwa kwa ufisadi wa mabilioni ya shilingi uliofanywa na kampuni ya Mwananchi Gold kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Hata hivyo, mwenyewe amekuwa akikana madai hayo kupitia vyombo vya habari na kutoa msimamo kuwa kampuni ya Mwananchi Gold ni mali ya CCM.

Gazeti hili limeshindwa kujua mtu anayetarajiwa kuwa makamu mwenyekiti wa tume hiyo. Sheria ya marekebisho ya katiba inaelekeza kuwa iwapo mwenyekiti wa tume hiyo atatoka upande mmoja wa Muungano, makamu wake atoke upande mwingine.

Haikufahamika pia iwapo tayari Rais Kikwete ameshauriana na kukubaliana na Rais Ali Mohammed Shein wa Zanzibar juu ya hatua hiyo kama sheria hiyo inavyoshurutisha.

Jaji Warioba, mwenye umri wa miaka 71, ni mwanasheria kitaaluma. Aliteuliwa tarehe 5 Novemba 1985, kuwa waziri mkuu katika serikali ya awamu ya pili chini ya Rais Ali Hassan Mwinyi. Alidumu kwenye nafasi hiyo hadi tarehe 9 Novemba 1990 alipoteuliwa Cleopa David Msuya.

Warioba ana shahada ya kwanza ya sheria kutoka Chuo Kikuu cha Afrika Mashariki jijini Dar es Salaam. Aliingia katika utumishi wa umma mwaka 1966 akianza na uwakili wa serikalini. Kutoka mwaka 1968 hadi 1970 alikuwa mwanasheria wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.

Miongoni mwa kazi nyingine alizofanya nchini baada ya kustaafu uwaziri mkuu, ni ile ya mwenyekiti wa Tume ya Rais ya kuchunguza ukubwa wa tatizo la rushwa.

Ripoti ya tume hiyo ilitoa picha halisi ya tatizo la rushwa nchini. Wakati huohuo, Jaji Warioba alifanya kazi nje ya nchi, hasa nchini Ujerumani alipoteuliwa kwenye Tume ya Kimataifa ya masuala ya Bahari.

0
Your rating: None Average: 2 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: