Wasaidizi wa rais timizeni wajibu wenu


editor's picture

Na editor - Imechapwa 14 April 2010

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

KATIKA toleo la gazeti hili tumechapisha habari inayozungumzia sheria ya gharama za uchaguzi, tukihoji hatua ya Rais Jakaya Kikwete kusaini sheria hiyo kwa mbwembwe bila kuisoma vizuri.

Ukweli juu ya kasoro katika sheria hiyo iliyotiwa saini, umesemwa mapema tu na wadau mbalimbali, hata kabla hatujaandika habari husika. Ni katika mazingira haya ya kutokusoma, wasaidizi wa rais walidiriki kupachika kipengere kimoja cha 7 (3), naye akasaini kwa mbwembwe – jambo ambalo kwa wiki kadhaa sasa limekuwa linalalamikiwa na makundi kadhaa ya wananchi.

Ingawa serikali ilijitahidi kutetea kosa hili kwa lugha ya “kufafanua” au “kutafsiri” kilichotokea, ni dhahiri kwamba rais mwenyewe na wasaidizi wake wameingizwa katika tabaka la watu wenye umakini unaotiliwa shaka.

Kwetu sisi, na kwa wananchi wote walio makini, kitendo hiki cha watawala wetu ni ishara kwamba hawaipi jamii uzito na heshima inayostahili.

Bahati pekee waliyonayo watawala hawa ni kwamba mfumo waliouasisi na kuusimika kwa miongo kadhaa, umewanyima wananchi fursa ya kujua vema haki zao na wajibu wao katika kuwawajibisha viongozi wao.

Vinginevyo, sasa hivi kungekuwa na maandamano kila kona ya Tanzania kushinikiza watawala wawajibike, wakiri kosa na watuombe radhi.

Hata hivyo, tunaamini kwamba, taratibu, Watanzania wameanza kung’amua mambo haya na kuhoji, hata kwa maandishi tu; jambo ambalo, wakubwa wasipobadilika na kujirekebisha, linaweza kuzua mgogoro mkubwa wa kijamii, na kuhatarisha amani na utulivu tunaojivunia majukwaani.

Tungependa kumshauri mheshimiwa rais ajue kuwa jukumu la kuongoza nchi hii limo mikononi mwake kama alivyosema haba ubia katika urais. Kwa hiyo, asikubali “kuingizwa mjini” na wasaidizi wake kirahisi; ajue hata kama wanaomsababisha afanye makosa ni wasaidizi wake, yeye ndiye anayepaswa kuwajibika; na wanapofanya hivyo akubali kuwawajibisha na kujisafisha mbele yao na mbele ya umma.

Tunaamini kuwa ingawa rais hafurahii vitendo vya wasaidizi wake kumdhalilisha kisiasa na kiutendaji kwa hatua kama hizi, rais wetu naye ajifunze kuchukia na kuchukua hatua.

Maana hali ikiendelea hivi, na ikajirudia mara nyingi, itafika mahali wananchi wataacha kutumia lugha ya mzunguko ya “rais anadanganywa” na wasaidizi wake; jambo ambalo litazaa kauli nzito zaidi ambazo wakubwa wanaweza kuzitafutia tafsiri na ufafanuzi usiopendeza.

Hata kama inawezekana ni kweli kuwa rais si mwepesi wa kusoma, wasaidizi wake wamsaidie kumsomea na kumwepusha na mazingira tata kama haya, maana moja ya majukumu waliyonayo ni kumfichia kiongozi wetu baadhi ya udhaifu alionao, ili kukuza haiba yake na heshima mbele ya umma. Mifano ipo mingi na hatutaitaja hapa, lakini katika mazingira haya, ni dhahiri wasaidizi hawa wa rais hawajatimiza wajibu wao huu.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: