Wasemaji wa serikali wamekuwa bubu


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 10 February 2010

Printer-friendly version
Waraka wa Wiki
Yahofiwa hawajui lolote, wamejaa woga
Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Ikulu, Salva  Rweyemamu

SERIKALI ya Tanzania ina tabia ya kukaa kimya bila kujibu hoja wala tuhuma inazoelekezewa kupitia vyombo vya habari. Inawezekana inatumia ukimya ili kujijengea kinga. Lakini sivyo ilivyo katika mataifa mengine.

Mwaka 2007 nilikuwa naishi na kufanya kazi nchini Uganda. Wakati huo nilishuhudia mijadala na majibizano makali katika magazeti makuu ya nchi hiyo.

Hayo yalikuwa kati ya watu wawili: Andrew Mwenda na Teddy Ssezi Cheeye. Wakati Mwenda alikuwa mwandishi wa habari wa gazeti la The Daily Monitor, Cheeye alikuwa Mkuu wa Kitengo cha Ujasusi wa Kiuchumi wa Shirika la Ujasusi wa Ndani wa Uganda (ISO).

Mwenda alikuwa anaponda utawala wa Rais Yoweri Museveni kwa kushindwa kufuata kanuni za kawaida kabisa za kiuchumi kama zilivyoelezwa na mchumi maarufu wa Marekani, John Maynard Keynes.

Cheeye alikuwa akimjibu Mwenda na kueleza jinsi serikali ya Uganda ilivyokuwa inafuata kanuni ya uchumi ya Keynes iitwayo The Law of Money, Interests and Employment.

Nilijifunza mengi katika mijadala hiyo. Nilijifunza pia kutoka makala za mshauri wa mambo ya sheria wa Museveni, Fox Odoi, aliyekuwa mstari wa mbele kuelemisha jamii kuhusu masuala kadhaa ya kisheria yaliyohusu serikali.

Mshauri wa Museveni wa masuala ya kisiasa, Moses Byaruhanga, alikuwa na safu yake ya kudumu kwenye gazeti la The Daily Monitor ambalo nchini Uganda linachukuliwa kama la upinzani.

Mshauri wa Museveni wa masuala ya habari, John Nagenda, alikuwa na safu katika gazeti la serikali la New Vision (bado anaendelea nayo).

Waandishi wawili wa ikulu, Mary Karooro Okurut na Ofwono Opondo walikuwa wakiandika mara kwa mara kwenye magazeti na kushiriki kwenye midahalo ya televisheni na redio kutetea hoja za serikali.

Niliwahi pia kusoma, zaidi ya mara tatu katika mwaka huo mmoja, makala zilizoandikwa na Rais Museveni akijibu hoja zilizomgusa binafsi.

Ukija Tanzania, hali ni tofauti. Hoja zinajengwa kuhusu serikali ya Rais Jakaya Kikwete lakini hazijibiwi au zinajibiwa kijuujuu mno.

Chukua mfano huu. Kuna siku nilialikwa kama mchangiaji mada katika kipindi kimoja cha televisheni hapa nchini. Mada ilihusu masuala ya madini.

Wengine walioalikwa ni mwanasheria Tundu Lissu na mwakilishi mmoja wa serikali. Mwakilishi wa serikali alikataa kuhudhuria kwa madai kuwa Lissu “anasema sana.” Serikali ikakosa msemaji.

Mimi ni miongoni mwa wale wanaomini kwamba serikali ina taarifa nyingi (na sahihi zaidi) kuhusu nchi hii kuliko sisi tulio nje ya serikali.

Hii ndiyo maana wakati MwanaHALISI lilipofichua habari za ufisadi na mafisadi mwaka 2007, taarifa hizo zilihusu mambo ambayo yalifanyika nyuma ya mwaka huo. Kwa hiyo kuna watu serikalini walijua yote hayo kabla hata gazeti hili kufichua.

Wakati JK alipoingia madarakani, miongoni mwa mapinduzi makubwa yaliyofanyika ilikuwa kuhakikisha wizara na taasisi za serikali zinakuwa na wasemaji. Kazi yao ni kuzungumzia mambo ya serikali.

Kwa tathmini yangu, hadi sasa, naona wasemaji wameiangusha serikali. Nimebaini mambo kadhaa yaliyochangia hili.

Hebu nianzie juu kabisa. Nakiri mapema kwamba Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Ikulu, Salva Rweyemamu, ni miongoni mwa waandishi wa habari wazuri nchini.

Salva wa sasa, kama angekuwa Salva yule wa miaka kumi iliyopita (alipokuwa Mhariri Mtendaji wa iliyokuwa Habari Corporation), angemsaidia mno Kikwete na serikali yake. Ninaamini angeendesha mijadala ya hoja na wale ambao inadaiwa “hawaiongelei vizuri” serikali.

Mwandishi wa ikulu angekuwa akijibu hoja na tuhuma, na watu wakaelewa na kuamini. Hii ni kwa sababu ya nafasi yake katika jamii wakati huu.

Lakini tatizo kubwa la Salva ni kuwa heshima yake katika jamii hivi sasa si sawa na ile aliyokuwa nayo miaka kumi iliyopita. Amehusishwa na tuhuma mbalimbali na kuna baadhi ya mambo ambayo serikali imekuwa ikiandamwa sana na yeye ametajwa kuhusika nayo.

Kimsingi, amekosa moral authority ya kuwa msemaji wa serikali katika hoja inazorushiwa kuhusu ufisadi. Kwa maana hiyo, hawezi kuisaidia serikali kwenye hilo. Inawezekana kuna wengi serikalini wenye tatizo kama lake.

Wasaidizi wake, kwa mfano, Premi Kibanga (namheshimu pia kama mwanataaluma), hajazoea kuandika magazetini. Inawezekana amewahi kuandika kitu magazetini, lakini sijawahi kuona makala yake ya uchambuzi hata siku moja. Katika hili afadhali Salva.

Waandishi wa habari wa ikulu na Ofisi ya Waziri Mkuu wamebaki kuwa watu wa kutoa taarifa za maandishi tu – Press Release. Taarifa hizi hazifafanui mambo bali kueleza rais au waziri mkuu atakwenda wapi, alikuwa wapi na alifanya nini.

Nakumbuka miaka michache iliyopita, mwandishi mkuu wa habari wa waziri mkuu, Said Nguba, alikuwa akijitahidi kuandika; enzi zile Edward Lowassa akiwa waziri mkuu. Mara nyingi nilikuwa nikifaidika sana na ufafanuzi wake. Yeye alikuwa akieleza ukweli ulivyo.

Kwa kipindi kirefu sasa, Nguba amekuwa kimya. Nilisikia alipata matatizo ya kiafya na huenda ndiyo sababu. Hata hivyo, yeye si mwandishi pekee wa habari katika ofisi hiyo. Wako wapi wengine?

Kuna Idara ya Habari ya serikali, maarufu kwa jina la MAELEZO. Kwa kadri ninavyofahamu, waandishi waliopo pale wamekuwa wakiandika tu kuhusu ziara za viongozi na miradi ya serikali.

Ni kweli kwamba taarifa za ziara za viongozi na miradi au mipango ya serikali zinafaa kuelezwa kwa wananchi, lakini kazi yao haiwezi kuishia hapo. Wana wajibu pia wa kushiriki katika mijadala ya kitaifa.

Na hapa ndipo linapokuja tatizo la pili baada ya lile la usafi wa wateule binafsi wa serikali; suala la uwezo binafsi wa wasemaji hao wa kuchanganua mambo.

Kuna wana habari wazuri tu pale MAELEZO; wenye vyeti vya kutosheleza kitaaluma lakini wasiokuwa na uwezo wa kujieleza mbele ya kamera au redioni na magazetini. Tatizo jingine linatokana na kutojiamini miongoni mwa wasemaji hao wa serikali.

Niliwahi kuzungumza na ofisa habari mmoja wa wizara moja nyeti ya serikali ambaye alinieleza kwamba kuna siku aliandika kitu kwenye gazeti na mkubwa wake hakufurahi. Bosi akaona kijana anataka “kumfunika.”

Hivi ni kweli kwamba hakuna hata msemaji mmoja wa serikali ambaye anaweza kuomba kuwa na safu kwenye magazeti kama hili au Tanzania Daima, kwa mfano, ili kuwa akijibu hoja zinazojengwa?

Hivi ni kweli serikali haina walau mtu mmoja mwenye uwezo wa kufafanua na hata kujenga hoja kukabiliana na zile zinazojengwa na wananchi wasomaji na baadhi ya waandishi kama Ndimara Tegambwage, Ansbert Ngurumo, Mwanakijiji, Mwalimu Mkuu wa Watu na wengine?

Huwa ninajiuliza, ni nani washauri wa Rais Kikwete katika masuala, kwa mfano, ya uchumi, siasa na ulinzi na usalama? Tutajuaje wanajua wanachojua iwapo hawaandiki kujibu, kukubaliana, kufafanua na hata kupinga kilichoandikwa. Au nao hawajui kitu?

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: