Wasio na sifa wawafunda mawaziri


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 18 May 2011

Printer-friendly version
Tuseme Ukweli
Semina elekezi kwa viongozi wa Serikali

ILI kupata wanafunzi bora katika ngazi zote za elimu ni lazima wawepo walimu bora na waadilifu. Hata katika semina, mwezeshaji lazima awe mjuzi na mwadilifu ili kuwajengea imani wanasemina au hadhira.

Ndiyo maana serikali huingia gharama kubwa kuandaa walimu ili wawe weledi na mahiri katika nyanja zote, na waadilifu.

Katika baadhi ya shule, walimu na hata wakuu wa shule hukataliwa na wanafunzi kwa kukosa sifa. Pengine ni walevi, wachafu, wazinzi, walarushwa kiasi cha kuwa chukizo kwa wanafunzi na jamii.

Maelezo hayo ni ya msingi ili kujua ubora wa walimu waliotumiwa katika semina elekezi iliyoandaliwa na Rais Jakaya Kikwete kwa ajili ya mawaziri, manaibu waziri, makatibu wakuu, manaibu katibu wakuu na wakuu wa taasisi mbalimbali za serikali.

Rais Kikwete, kama mkuu wa semina, aliorodhesha sifa wanazopaswa kuwa nazo wanafunzi wake hao. Aliwaambia hataki kuona wakinyooshewa kidole kwa uvivu, uzembe, wizi, ubadhirifu wa mali ya umma.

Alitaka wasikutwe na vitendo vya ulevi wa kupindukia, uzinzi, majigambo, ubabe, uonevu na dhulma.

Je, walimu au wawezeshaji wa semina walikuwa na sifa? Walichoelekeza kilitoka moyoni? Je, walikuwa mfano wa kuigwa? Kama hawakuwa na sifa, basi kazi yao haikuthaminiwa.

JK lawamani

Kikwete aliyefungua na kufunga semina hiyo elekezi, hakusema ataanza lini kusikiliza au kutazama kidole kikinyooshwa dhidi ya wateule wake. Hakusema kama ataanza na orodha ya mafisadi walionyooshewa kidole na umma.

Maana katika orodha ile, yumo mkuu mwenyewe wa semina na pia mtangulizi wake, Benjamin Mkapa, na aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu (BoT), Daudi Balali.

Katika orodha ile walinyooshewa kidole waziri mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa; aliyekuwa waziri wa miundombinu Andrew Chenge, na mbunge wa Igunga, Rostam Aziz. Hao watatu hadi sasa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinahangaika kuwavua gamba baada ya kuwatuhumu kwenye vikao vyao vya hivi karibuni mjini Dodoma.

Wengine ni aliyekuwa waziri wa fedha, Basil Mramba, na aliyestaafu kuwa katibu mkuu wizara ya fedha, Gray Mgonja ambao serikali imewafungulia kesi ya ufisadi. Kwenye orodha ile pia yumo aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi.

Kama Rais Kikwete atatumia orodha ile basi mkuu wa semina naye hana sifa. Lakini kama atasema “yaliyopita si ndwele tugange yajayo,” atakuwa ameruka majivu akakanyaga moto.

Kwanini? Akiwa katikati ya semina inayofanana na twisheni kwa mawaziri ambao asilimia 53 ni wakongwe, rais amenyooshewa kidole kwa ubabe, uonevu na dhulma.

Anadaiwa kudhulumu nyumba iliyoko kiwanja Na. 64 katika makutano ya barabara za Ursino na Migombani, Mikocheni jijini Dar es Salaam. Hati zinaonyesha, pamoja na nyumba hiyo kukaliwa na watumishi wa serikali akiwemo Kikwete hadi alipochaguliwa kuwa rais mwaka 2005, wamiliki halali ni Amirali Abdulrasul Alarakhia Dewji na Yusufali Kassamali Remtula Parpia.

Sechi za nyumba hiyo ya mwaka 1982 na mwaka 2002 zinaonyesha hivyo. Bali katika mazingira tata, sechi ya mwaka 2010 imepokonya umiliki. Warithi wa nyumba hiyo wanataka Rais awarejeshee nyumba yao.

Malalamiko ya raia dhidi ya mkuu wao wa nchi yanazidi kumshushia heshima, hadhi na umaarufu. Atamwajibishaje mteule wake aliyekosa sifa?

Mzimu wa EPA

Kama mkuu wa semina amekosa sifa kuna uwezekano mkubwa itakuwa ameteua wawezeshaji wasio sifa. Hii ni kwa sababu ndege wa jamii moja huruka pamoja.

Baadhi ya mada zilizowasilishwa katika semina elekezi ni mapambano dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya na vita dhidi ya rushwa. Wawasilishaji wa mada hizo walikuwa maofisa kutoka Jeshi la Polisi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

Ofisi mbili hizo hazina sifa ya kutoa wawezeshaji katika semina iliyosheheni wanasiasa na watendaji weledi na wakongwe.

Kwanini? Alipounda kikosi kazi cha kuchunguza wezi wa fedha katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) iliyoko Benki Kuu (BoT), Rais Kikwete aliwateua mwanasheria mkuu, Johnson Mwanyika; Inspekta Jenerali wa Polisi, Said Mwema na Mkurugenzi mkuu wa TAKUKURU, Dk. Edward Hoseah.

Walichagua mafaili ya kuchunguza. Mengine wakayaacha. Maana yake walichagua fulani na fulani washitakiwe na wengine wasishitakiwe.

Hao ndio waliamua baadhi ya waliokwapua fedha za EPA, pamoja na kuwajua majina, kampuni zao na walikopeleka, kuwatangazia msamaha ‘duniani na mbinguni’ wakirejesha.

Hii ndiyo sababu, pamoja na kuwepo nyaraka muhimu za waliochukua fedha na walikopeleka, wateule hao kwa maelekezo ya rais, waliacha kuwashitaki waliokwapua mabilioni ya shilingi za EPA kupitia kampuni za Kagoda Agriclture na Deep Green Finance.

Kama Polisi wameficha wezi, hawana sifa ya uadilifu kuwa wawezeshaji wa semina.

Angalizo: Mwanyika amestaafu, nafasi yake inakaliwa na Frederick Werema ambaye weledi wake unatia shaka katika suala la Dowans, mrithi wa mkataba feki wa Richmond.

Hata kwa kutazama taasisi moja moja, TAKUKURU imebaki kuwa muhimu kwa kutoa ajira siyo tija kiutendaji.

Mbali na kushirikishwa kuficha wezi wa fedha za EPA, ni taasisi iliyoshindwa kunusa rushwa katika namna Richmond walivyopewa mkataba wa kufua umeme wa dharura mwaka 2006.

TAKUKURU ndiyo iliyojitosa kumsafisha Chenge katika kashfa ya kuweka vijisenti nchi za nje vilivyotokana na ‘dili’ la ununuzi wa rada kwa bei mbaya. Taasisi ya Uchunguzi wa Makosa Makubwa ya Jinai ya Uingereza (SFO) ilibaini rushwa, lakini TAKUKURU ikadai hakuna. Ilidanganya.

Hii ndiyo taasisi iliyoshindwa kunusa rushwa katika mchakato wa kupata wagombea wa nafasi za ubunge katika CCM na iliowanasa ‘ililengeshewa’ kuwazibia nafasi.

Hii ndiyo taasisi ambayo bosi wake alikaririwa na mtandao wa kiuchunguzi wa WikiLeaks akilalamika kuzuiwa na Rais Kikwete kushitaki watuhumiwa ufisadi wenye majina makubwa. Dk. Hoseah angesema nini tofauti katika semina ambayo msimamizi ni JK mwenyewe?

Polisi wana sifa ya kukamata wavutaji na wakulima wa bangi na labda watumiaji cocaine. Kama Jeshi lilishiriki kuficha mafisadi wa EPA haliwezi kutaja matajiri wa biashara hiyo.

0
Your rating: None Average: 4.3 (3 votes)
Soma zaidi kuhusu: