Wasomi wachokonoa CCM


Mwandishi Maalum's picture

Na Mwandishi Maalum - Imechapwa 21 April 2010

Printer-friendly version
Ilishinda kwa fedha za wizi
Rais Jakaya Kikwete

WASOMI wawili wa Marekani wamedai kuwa angalau sehemu kubwa ya dola 20 milioni (Sh. 25 bilioni) kutoka mabilioni yaliyoibwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) zilitumika kuleta ushindi katika majimbo mawili ya uchaguzi mwaka 2005.

Wakinukuu taarifa za gazeti moja nchini Uganda, wasomi hao, pamoja na kutaja majimbo husika wanakodai Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilikuwa kimeelemewa, wanasema pia wizi BoT ulishinikizwa na baadhi ya viongozi wa kisiasa.

Kuelekea uchaguzi mkuu 2005, Sh. 133 bilioni zilikwapuliwa kutoka akaunti ya madeni ya nje (EPA) iliyoko BoT na makampuni mbalimbali, yakiwemo feki ambayo baadhi tayari yamefikishwa mahakamani.

Hata hivyo, baadhi ya makampuni na wahusika wake hawajafikishwa mahakamani kutokana na kinachoitwa “msamaha wa rais” kwa waliokiri kuiba na kukubali kurejesha sehemu ya walichokwapua.

Barak Hoffman na Lindsay Robinson kutoka Chuo Kikuu cha Georgetown nchini Marekani, katika ripoti yao iitwayo “Tanzania’s Missing Opposition” – Ukosefu wa upinzani Tanzania – wanasema dola milioni 20 zilitumika katika majimbo mawili.

Majimbo hayo wanayataja kuwa ni Kigoma mjini na Songea mjini. Majimbo haya yalikuwa na upinzani mkali mwaka 2005 ingawa ripoti haielezi fedha hizo zilitumika kufanya kazi gani ili kuimarisha nguvu za chama tawala.

Ushindani kwa upande wa Kigoma mjini ulikuwa kati ya Peter Serukamba (CCM) na Dk. Aman Walid Kabourou (Chadema).

Kwa upande wa Songea mjini, ushindani ulikuwa kati ya Emmanuel Nchimbi (CCM) na wakili wa mahakama kuu, Edison Mbogoro (Chadema). Upinzani ulishindwa katika majimbo yote mawili.

Kushindwa kwa Dk. Kabourou, hata hivyo, kumekuwa kukitiliwa mashaka kufuatia mlegezo uliojitokeza katika kura za kumpata mbunge wa baraza la kutunga sheria la Afrika Mashariki. Bunge lilimpitisha kwa kura nyingi.

Kinachotumiwa kuvumisha hilo zaidi ni hatua ya Kabourou kukana chama chake na kuhamia CCM mara baada ya kushindwa jimboni. Lakini Kabourou amekuwa akitaka chambo cha ubunge wa Afrika Mashariki.

Bila kutaja wapi fedha nyingine zilizoibwa zilitumika, wasomi hao wanadai kuwa ukwapuaji wa mabilioni ya shilingi kutoka BoT “ulifanywa kwa makusudi” ili kunufaisha CCM na mgombea wake wa urais, Jakaya Kikwete.

“Viongozi wa juu wa CCM ndio walioagiza uchotaji wa mabilioni ya shilingi katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ili kunufaisha chama chao katika uchaguzi wa mwaka 2005,” inasema sehemu ya ripoti hiyo.

Ripoti ya uchunguzi ya wasomi hao ambayo inaonekana kutolewa Desemba mwaka jana,
inahusisha ukwapuaji huo na viongozi waandamizi wa CCM.

Katika baadhi ya maeneo, ripoti inadai kuwa gavana wa BoT na watumishi wa ngazi ya juu wa benki hiyo, walitishwa na viongozi waandamizi katika serikali na CCM ili wakubali utekelezaji wa mpango huo.

“Gavana na watendaji wengine wa ngazi ya juu ndani ya BoT wanateuliwa na rais wa Jamhuri ya Muungano ambaye ni mwenyekiti wa CCM. Bali kuna ushahidi kuwa watumishi wa serikali wamekuwa wakitishiwa kuwa watapoteza ajira zao iwapo hawataisaidia CCM,” imeeleza taarifa bila kutaja ushahidi huo.

Aidha, ripoti inang’ang’aniza kuwa baadhi ya watuhumiwa katika ukwapuaji huo “wamedai kwamba waliagizwa na kigogo wa ngazi ya juu katika chama tawala kuharakisha wizi huo.”

Kwa zaidi ya miaka minne sasa, CCM imekuwa ikituhumiwa hadharani kuhusika katika ukwapuaji wa mabilioni ya shilingi kutoka BoT na kuingiza fedha hizo kwenye uchaguzi.

Mara zote, si CCM wala serikali imeweza kujivua tuhuma hizo. Hii ni pamoja na kuwepo madai kwamba rais mstaafu Benjamin Mkapa, aliagiza “kuchukuliwa kwa fedha nyingi kutoka BoT.”

Wakili wa mahakama kuu, Byidinka Sanze, chini ya kiapo, anadaiwa kutamka kuwa alialikwa ofisini kwa Rostam Aziz – mfanyabiashara na mbunge wa Igunga – kushuhudia moja ya mikataba iliyotumika kuchotea mabilioni ya shilingi kutoka BoT.

Mkataba huo ni ule unaofahamika kuwa wa Kagoda Agriculture Limited, kampuni iliyochota kiasi cha Sh. 40 bilioni kwa kile Sanze anachodai Rostam alimwambia ni “kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa 2005.”

Kwa nyakati tofauti, serikali imekiri kushindwa kujua Kagoda ni kampuni ya nani wakati watu wote wanaotajwa kuhusika nayo bado wako hai.

Wakati fulani, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alisema serikali inaendelea kuchunguza nani wamiliki wa kampuni hiyo na kwamba “haiogopi kumchukulia hatua yeyote” atakayebainika kuhusika na Kagoda.

Lakini katika siku za karibuni, Pinda amekaririwa akisema ni vigumnu kujua Kagoda ni nani.

Naye Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Eliezer Feleshi amewahi kukaririwa akisema ofisi yake haijawahi kupata uthibitisho wa wamiliki wa Kagoda au ushiriki wa wanaotuhumiwa.

Katika hatua nyingine, ripoti ya wasomi hao wa Marekani inasema kufungiwa kwa gazeti la MwanaHALISI Oktoba 2008, kwa kuandika juu ya mgogoro ndani ya CCM, ni miongoni mwa mbinu za vitisho zinazotumiwa na chama hicho kubaki madarakani.

“Zaidi ya kufungiwa kwa gazeti hilo, wafanyakazi wawili wa ofisi hiyo walishambuliwa na kumwagiwa tindikali na wavamizi…lakini lengo kuu lilikuwa ni kuwatisha,” imeeleza ripoti ya utafiti wa wanazuoni hao.

Kuvamiwa kwa MwanaHALISI, wahariri wake kumwagiwa tindikali na kukatwa mapanga, ni vitendo vilivyofuatia gazeti kuripoti mfululizo kashfa ya Richmond, inasema ripoti hiyo.

Kashfa ya Richmond inahusu hatua ya serikali kutoa mkataba wa kuzalisha umeme wa dharura kwa kampuni isiyo na anwani, fedha wala wataalam “kwa njia ya upendeleo.”

Ni kashfa hii iliyomng’oa Edward Lowassa kutoka wadhifa wa waziri mkuu, Februari 2008.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: