Wassira: Tutamkomboa mkulima hatua kwa hatua


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 16 June 2010

Printer-friendly version
Tafakuri

STEVEN Wassira, ni miongoni mwa mawaziri waliopita katika wizara tofauti kwa kipindi cha miaka minne ya utawala wa Rais Jakaya Kikwete.

Kwanza alikuwa Wizara ya Maji, akaenda Kilimo na Ushirika na baadaye wizara ya tawala za mikoa na serikali za mitaa (TAMISEMI) kabla ya kurejea Kilimo, Chakula na Ushirika ambako yuko hadi sasa.

Kuna taarifa kwamba chini ya uongozi wake katika wizara ya kilimo na ushirika, tatizo la kukopa wakulima katika zao la korosho lilikuwa limeanza kukabiliwa kwa juhudi binafsi za waziri.

Vilevile kuna taarifa kuwa Wassira alikuwa anajiandaa kumaliza tatizo la wakulima wa pamba la kukopwa na wafanyabiashara.

Wapo wanaosema kwamba kurejeshwa kwake katika wizara hiyo, kumetokana na uwezo wake wa kukabiliana na matatizo ya wakulima.

Wassira, aliwahi kutumikia wizara hiyo akiwa naibu (ikiiitwa Wizara ya Kilimo na Maendeleo ya Mifugo) katika utawala wa awamu ya kwanza.

Leo hii ndiye chachu ya utekelezaji wa kile kinachoitwa, “Mpango wa Kilimo Kwanza” uliozinduliwa mwaka jana mjini Dodoma.

Katika mahojiano na MwanaHALISI wiki iliyopita mjini Dodoma, Wassira anasema, “Watu watofautishe kaulimbiu ya Kilimo Kwanza na tamko la Kilimo cha Kufa na Kupona lililotolewa na Mwalimu Nyerere mwaka 1973 kule Musoma.”

Anasema kaulimbiu ya Kilimo Kwanza, pamoja na kufanana kiasi na tamko la Siasa ni Kilimo lililotolewa Iringa mwaka 1972, inakiri pia kwamba, ili nchi iweze kuwa na chakula cha kutosha na kupata ziada ya kuuza, sharti kilimo kiwe cha kisasa badala ya kile cha kujikimu.

Sekta ya kilimo inatoa ajira kwa zaidi ya asilimia 70 ya wananchi; inaingiza zaidi ya asilimia 30 ya fedha za kigeni; ndicho kinatoa zaidi ya asilimia 65 ya malighafi inayotumika viwandani.

Vilevile kauli mbiu inakiri kwamba ikiwa kilimo kitaachwa kiendelee kuwa cha kujikimu uwiano unakataa kwa watu zaidi ya asilimia 70 kuendelea kutegemea kilimo cha kujikimu.

Aidha, takwimu zote zilizofanywa na asasi mbalimbali na hasa zilizoko serikalini, zinaonyesha kuwa umaskini uko zaidi vijijini.

“Kwa hiyo kama tunataka uchumi wa kisasa kama Dira ya Taifa ya 2025 inavyoainisha, ili kupunguza umaskini kwa wananchi waliowengi, ni kuongeza uwekezaji katika kilimo,”anasema Wassira.

Uwekezaji unawekwa katika aina tatu: Kwanza, ni kupitia Bajeti ya Serikali ambayo inamsaidia mkulima kupata pembejeo na mbegu pamoja na vifaa vya kilimo.

Wakati wa uzinduzi wa mpango wa Kilimo Kwanza, mwaka jana, Rais Kikwete alitangaza kuwa zimetengwa Sh. 118 bilioni kwa ajili ya kununulia mbolea kwa mwaka wa fedha 2009/2010.

Hapa ndipo Wassira anasema mafanikio ya mpango huo yameanza kuonekana kwani kuna taarifa ya ongezeko la kuridhisha la mazao msimu huu.

Serikali inagharimia pia tafiti za kilimo cha kisasa, huduma muhimu za ughani na inaweka miundombinu ya umwagiliaji ili wakulima wasitegemee kilimo cha mvua peke yake.

Aina ya pili ya uwekezaji ni kwa njia ya mikopo. Kwa kuwa serikali inatambua kwamba bajeti pekee haiwezi kubadilisha kilimo kutoka cha kujikimu hadi kuwa cha kisasa, imeingiza suala la mikopo ya kilimo.

Wakulima wa Tanzania bado hawana fursa za kukopa kwenye mabenki na sababu kubwa ni kwamba mikopo ya namna hii kwa wakulima haipo.

Wakulima wanahitaji mikopo ya muda mrefu lakini ulipaji mikopo kwenye mabenki ya kibiashara ni wa muda mfupi.

Huu ndio msingi wa azma ya kuanzisha Benki ya Kilimo, na kwa umuhimu wa haraka, serikali imeanzisha dirisha dogo la kukopa kwenye Benki ya Raslimali ya Taifa (TIB).

Mchakato wa kuanzishwa kwa Benki ya Wakulima ulianza mwaka jana na Rais Kikwete amesema serikali inashirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo serikali ya China.

Aina ya tatu ya uwekezaji ni kufanya kazi ya kuwatafuta wakulima wa kati na wakubwa ambao hupatikana kwa kufanya ushawishi na kuwapa vivutio vya uwekezaji.

Wassira anasema Mkutano wa Kiuchumi Duniani (World Economic Forum) uliofanyika hivi karibuni Dar es Salaam ni sehemu ya mikakati ya kushawishi ujio wa wakulima wakubwa na wadogo.

Hata hivyo, Wassira amesema mpango wa Kilimo Kwanza hauishii kwenye wizara yake tu bali linahusisha pia wizara kadhaa.

“Ili kuhakikisha kilimo kinaboreshwa, lazima ifanyike mipango ya kuimarisha pia miundombinu ya barabara ili kurahisisha usafirishaji, kuanzisha viwanda, kusogeza huduma ya nishati, maji na kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na serikali za Mitaa,” anafafanua.

Mchango wa wizara nyingine ni kwamba Wizara ya Miundombinu inajenga barabara kuu na ndogo, Wizara ya Viwanda na Biashara inatafuta masoko ya nje na kushawishi ujenzi wa viwanda kama vile vya kusokota nyuzi badala ya kuuza pamba; wakati Wizara ya Madini na Nishati inapeleka umeme kwenye viwanda hivyo na Tawala za Mikoa wanafanya kazi ya usimamizi.

Kuhusu ushirika, Waziri Wassira anasema akilinganisha hali ya sasa na walivyovikuta vyama vya ushirika mwaka 2004/05, kuna nafuu kubwa sasa, japokuwa bado kazi inahitajika kufanywa ili vifanye kazi kwa ufanisi.

“Nilipopewa kazi hii, korosho zilikuwa zinanunuliwa kwa mfumo usiohusisha vyama vya ushirika. Kilo moja ilikuwa inauzwa Sh. 300, lakini baada ya kuanzisha vyama vya ushirika na mfumo wa ununuzi kwa stakabadhi ghalani, kilo moja inauzwa kwa Sh. 700 hadi 900.” anasema.

Kazi nyingine inayofanywa na serikali ni kuhakikisha korosho zinabanguliwa ili kuongeza thamani badala ya kuuza zenye maganda.

Kuhusu tumbaku, waziri anasema wakulima walikuwa wanalaliwa kwa mikopo lakini ulipoingia ushirika, sasa mikopo ya ununuzi wa mbolea inadhaminiwa na vyama vya ushirika na wakulima wamepata nafuu.

Akizungumzia pamba, Wassira amesema baadhi ya vyama vya ushirika wa pamba vinafanya vizuri na vingine vinasuasua.

Amesema Chama cha Ushirika Mkoa wa Shinyanga (Shirecu) kinafanya vizuri kiasi, lakini Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Mwanza (Nyanza Cooperative) kinasuasua.

Amesema wakati Nyanza inasuasua na serikali inaendelea na tiba, kule Mara kimeanzishwa chama kipya na vyama vingine vidogovidogo kama Igembesabo vinaendelea vizuri.

Kuhusu vyama vya ushirika wa kahawa, Wasssira anasema vinafanya kazi vizuri japokuwa havijafikia kiwango kinachotakiwa na serikali.

Waziri anasema tatizo ambalo bado halijapatiwa ufumbuzi kwa mujibu wa ni ushirika wa mazao mchanganyiko na kilichofanyika hadi sasa ni kuunda Bodi ya Mazao Mchanganyiko yanayohusisha mpunga na mahindi.

Hata hivyo, Wassira amesema kuna matarajio kwa nchi kupiga hatua kubwa ya maendeleo kutokana na raslimali zilizopo kama vile gesi, misitu, madini na hifadhi za taifa.

0
No votes yet