Watakaotii amri haramu watashtakiwa!


M. M. Mwanakijiji's picture

Na M. M. Mwanakijiji - Imechapwa 06 October 2010

Printer-friendly version
Kisima cha Mjadala

KUNA imani potofu imejengeka kwamba mwanajeshi akiamriwa jambo na wakubwa zake, ni lazima alitekeleze. Imani hii imewafanya baadhi ya wananchi kuhofia wanajeshi kuwa wakiamriwa amri yao ni halali.

Kwa upande mwingine wapo wanajeshi wanaoamini wakiamriwa chochote, hawawezi kuhoji.

Vilevile, wapo wakuu wa vyombo vya usalama ambao wanaodhani wanaweza kuamuru lolote kwa yeyote na likatekelezwa. Imani zote hizi hazina msingi katika sheria, mikataba ya kimataifa wala katika ukweli.

Fikra hizi zilitawala kwa kipindi kirefu kiasi kwamba mtu anapozungumzia “ulinzi” alikuwa hazungumzii ulinzi wanchi/falme au wa watu wa falme hizo, bali alikuwa akizungumzia ulinzi wa waliokuwa madarakani. Hili lilikuwa na ukweli zaidi wakati wakoloni walipokuja Afrika.

Mojawapo ya mambo ya kwanza kabisa ambayo watawala wa kikoloni waliyafanya ni kuvunja mifumo yote ya ulinzi ya watawala wa Afrika. Kuanzia tawala za watu wanaozungumza lugha ya Kingoni Kusini mwa Afrika hadi Mtemi wa Mirambo. Mifumo yote hiyo ilibomolewa.

Badala yake wakaanza kuunda vyombo vya ulinzi vya watawala wa kigeni na huo ndio ukawa mwanzo wa kuundwa kwa majeshi ya usalama ya kikoloni.

Kwa Tanzania jeshi la Polisi liliundwa 25Augusti mwaka 1919 kama chombo cha usalama cha kikoloni huku kikipata nguvu kutoka kwa maafisa kutoka Uingereza.

Kikosi cha Kutuliza Ghasia cha FFU kiliundwa mwaka 1949 kuwa chombo cha kutuliza vurugu. Yote haya yalifanywa kwa maslahi ya wakoloni. Ni baada ya uhuru, Polisi ikawa chombo chenye mlengo wa kulinda wananchi.

Tovuti ya jeshi la Polisi inaeleza, “Baada ya uhuru, Jeshi la Polisi lilianza kubadili mwelekeo toka katika kutumikia wakoloni, walengwa wakawa wananchi kwa mujibu wa sera za serikali ya wananchi.”

Kwa upande wa jeshi la wananchi historia yake haina tofauti sana na ile ya polisi. Baada ya kongamano la Berlin la mwaka 1884/1885 ambalo lilifanya Tanzania kuwa chini ya himaya ya Ujerumani, jeshi jipya la ulinzi likiwa na askari wengi wenye asili ya Nubi (Sudan Kusini) liliundwa. 

Baada ya Wajerumani kupoteza vita ya kwanza ya dunia, Tanganyika ikawekwa chini ya udhamini wa Uingereza na mara moja Uingereza ikaunda jeshi lake lililojulikana kama King’s African Rifle ambayo lilikuwa ni sehemu ya jeshi la Mwingereza katika Afrika ya Mashariki.

Katika jeshi hilo, Tanzania ilikuwa batalioni 1, 2 na 6; huku Kenya ikiwa batalioni 4 na 5, wakati Uganda ilikuwa batalioni ya 3. Mkuu wa jeshi hilo alikuwa ni Malkia wa Uingereza.

Baada ya uhuru jeshi likabadilishwa jina na kuwa Tanganyika African Rifles, lakini baada ya maasi ya 1964 lilivunjwa na baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, utaratibu mpya ukaundwa na kulifanya jeshi hilo kuwa jeshi la Wananchi. Ni baada ya kuungana na jeshi la Ukombo la Wananchi wa Zanzibar.

Matokeo yake ni kuundwa kwa jeshi la kisasa ambalo lilikuja kuonesha umahiri katika kulinda wananchi na mipaka ya taifa kwenye vita ya Kagera na wakati wote wa harakati za ukombozi wa Afrika.

Leo hatuna tena jeshi la Mfalme au jeshi la Watawala. Ndiyo maana jeshi hili haliitwi Jeshi la Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania au “Jeshi la rais wa Tanzania.” 

Kutokana na msingi huo, ni muhimu amri na agizo lolote ambalo mwanajeshi anapewa, lazima lizingatie ukweli huu kuwa yeye ni mtumishi wa wananchi na si mtumwa wa serikali iliyoko madarakani.

Ni muhimu kuelewa kuwa vyama vya siasa hubadilika, viongozi hubadilika na sera zao hubadilika . Yeye habadiliki. Anatakiwa kubaki asiye na upande.

Je, mwanajeshi akiamriwa kufanya jambo ambalo ni kinyume na sheria au maadili, anapaswa kulitekeleza?

Katika mashtaka ya Nuremberg mara baada ya vita ya pili ya dunia, maofisa wa jeshi la Kinazi la Ujerumani waliosimama kizimbani kwa makosa ya vita dhidi ya ubinadamu.

Walipojaribu kujitetea kuwa walikuwa wanafuata amri za Hitler na maafisa wake wa ngazi za juu, utetezi wao haukukubaliwa.

Nchini Marekani afisa wa jeshi alitiwa hatiani baada ya kumuua raia wa Vietnam kutokana na kuamriwa na mkubwa wake.

Hapa nchini zipo sheria na taratibu za kijeshi zenye kusimamia amri za kijeshi na zinazotakiwa kufuatwa na maafisa wetu wanapotekeleza wajibu wao.

Kama ilivyo sehemu nyingine duniani maafisa wa jeshi wanatakiwa kufuata amri halali ambazo wanaamaini kuwa zimetolewa kihalali.

Yaani, lazima maagizo yanayotolewa yakubalike kisheria na watekelezaji wafahamu kuwa wanayo kinga ya kufanya hivyo.

Nimeyasema haya kwa sababu kadiri joto la uchaguzi linavyozidi kupanda kuna kila dalili kuwa watawala wetu “walioshindwa” wanataka kutumia hoja ya “amani na utulivu” kutafuta kisingizio cha kutumia nguvu dhidi ya wananchi.

Kama wengi mjuavyo, chama pekee ambacho kina uwezo wa kusababisha umwagikaji damu ni CCM. Ni wao wenye uwezo wa kuzuia kwa kukubali sauti ya wengi.

Kauli ya Shimbo kwamba wananchi watii watawala walioko madarakani, ni lazima iangaliwe kwa umakini mkubwa kwani kutii amri isiyo halali, ni uhalifu.

Vyombo vya usalama vinaowajibu wa kuwahakikishia wananchi wanatekeleza majukumu yao ya kisiasa ikiwa ni pamoja na kupiga kura, kuhesabu kura na kuhakikisha hakuna kura chafu inayoingizwa katika sanduku la kura au katika hesabu za kura.

Ni lazima vyombo hivyo vitambue haki ya msingi ya wananchi kupinga kisiasa dhulma ambayo wanaweza kuona inatendewa dhidi yao. Hapa ni lazima ikumbukwe kuwa matokeo ya rais yakitangazwa hayawezi kuhojiwa.

Hata hivyo, katiba haikatazi wananchi kuyafurahia au kuyapinga au kuonesha kutofurahia utaratibu uliotumika kutangaza matokeo. Ni muhimu kujiandaa si kuzima maandamano ya furaha au ya kupinga, bali kuhakikisha kuwa yote yatakayofanyika yanapitia katika mkondo huru na wenye utulivu.

Kama serikali inataka uchaguzi uwe huru na haki, ni lazima ipambane na wachakachuaji wa matokeo.

Nje ya hapo, vyombo vya usalama viwe tayari kabisa kuwajibishwa na watendaji wake kuwa katika nusura ya kushtakiwa endapo watatoa amri na maagizo ambayo yatavunja haki za raia na haki za binadamu kwa sababu ambazo zinaweza kuepukika.

Hakuna mashaka kuwa hilo halitatokea. Wanajeshi watakumbuka viapo vyao vya kuiweka Tanzania kwanza na kuwa tayari kupiga saluti kwa Amiri Jeshi Mkuu mpya pasipo kuwa na huruma au uchungu wa kumuaga yule anayemaliza muda wake.

Hii ndiyo demokrasia, na kama wanaiona ngumu, basi wajaribu udikteta.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: