Watanzania tunaibiwa: Magufuli


Iddy Mkwama's picture

Na Iddy Mkwama - Imechapwa 29 April 2008

Printer-friendly version
Aahidi kupambana na watendaji wabovu
Waziri wa maendeleo ya  mifugo na Uvuvi, John Pombe Magufuli

"Haiwezekani bahari yetu igeuke kuwa kama shamba la bibi kila mtu anaingia na kuvuna chochote anachotaka bila kuka tazwa na mtu yoyote, nasema wizi huu sasa unafikia kikomo."

"Hatuwezi kuvumilia kuona tunaendelea kuibiwa na watu ambao si wazalendo, wakati wavuvi wetu wakiendelea kupiga yowe la umaskini."

Haya ni maneno ya Waziri wa maendeleo ya mifugo na Uvuvi, John Pombe Magufuli wakati alipokuwa akizungumzia mikakati ya kuhakikisha sekta ya uvuvi inachangia asilimia kubwa ya pato la taifa tofauti na ilivyo sasa.

Magufuli anasema kwa muda mfupi alioingia kwenye wizara hiyo amegundua kuna mambo ya ajabu ambayo kwa kiasi kikubwa ndio yanaikwamisha sekta ya uvuvi na kama itaendelezwa inaweza kuwa zaidi hata ya madini.

"Tunaojua umuhimu wa sekta hii ndio tuna moyo wa kuiendeleza, kama kukiwekwa mikakati itakayotekelezwa inaweza kuwa muhimu zaidi hata ya madini katika kuchangia pato la taifa. Inakwama kwa kuwa kuna mambo ya ajabu yanayoendelea haswa kwa watendaji waliopewa jukumu la kuiendeleza." anasema Magufuli.

Anasema watu ambao wanaikwamisha sekta hiyo ni maafisa uvuvi na watumishi wengine wa Wizara hiyo ambao wamekuwa wakishirikiana na watu wanaofanya vitendo viovu dhidi ya viumbe vilivyopo baharini.

"Nimegundua maafisa uvuvi wanahusika kwa kiasi kikubwa katika kuwafuga watu wanaofanya hujuma kwenye bahari zetu wanajulikana ila wanafumbiwa macho waendelee kuvua kwa mabomu na kutumia makokoro sasa mwisho wao umefika" anasema.

Anasema kama watendaji hao wangekuwa wanawajibika ipasavyo kusingeshamiri kwa vitendo hivyo kwani amegundua kilomita 1400 za bahari kutoka Moa, Tanga hadi Msimbati, Mtwara wanavua kwa samaki kutumia uvuvi haramu.

Na idadi kubwa ya watu hao ni wavuvi kutoka nje ya nchi na pamoja na hayo wanafanya ufisadi wa hali ya juu kwa kuvua idadi kubwa ya samaki wakati taarifa zao za uvuvi zinaonyesha wamepata idadi ndogo.

Anasema kwenye bahari ya Tanzania kuna zaidi ya meli 200 zinazofanya shughuli za uvuvi lakini ambazo zimesajiliwa ma zinazotambulika ni 69 tu na nyingi kati ya hizo zinatumia vibali walivyouziwa na wavuvi wazalendo.

"Tumeanza kuzungumza na mabalozi ili kuangalia ni jinsi gani tutawadhibiti watu hawa wanaokuja kufanya uvuvi haramu usio na faida kwetu, wanavua tani nyingi za samaki lakini zinazotambulika ni ndogo" anasema.

Alitolea mfano utafiti uliofanywa mwaka 2004 ambapo kulikuwa kunavuliwa tani 1.5 milioni za kamba kwa mwaka kwa kutumia vyombo 25 kati ya 10 ambavyo vilikuwa vimesajiliwa hadi kufikia tani 220 baada ya watu hawa kutishwa na wavuvi wenzao kuacha kutaja kiwango halisi wanachopata.

Mwaka 2004 kwenye bahari ya Dar es Salaam kuna meli ambayo ilikuwa inatoa taarifa ya kuvua tani 470 kwa siku lakini nao walitishwa na wavuvi ambao wanavua kwa lengo la kujinufaisha huku wakidai hakuna samaki kwenye bahari.

Kutokana vitendo hivi amegundua kwamba mchango mkubwa wa samaki wanaouzwa nje ya nchi wanatoka Ziwa Viktoria kwenye mikoa ya Mwanza lakini kwa upande wa bahari kuna hujuma zinafanya na kusababisha kupatikana kwa idadi ndogo ya samaki.

Hivyo kuanzia sasa ili kupambana na tatizo hili wataanza kuzihakiki upya leseni za wavuvi hawa ili kupata waaminifu na wenye uchungu na rasilimili za taifa na ikiwezekana kuzitoa upya pamoja na kuwabana maafisa uvuvi kuanzia ngazi zote hadi vijiji.

"Kwenye kila kijiji, akikamatwa mvuvi anayetumia mabomu, sumu au makokoro afisa uvuvi ataunganishwa kwenye kesi ili kuwafanya wawajibike na hatutakuwa na mzaha kwenye hili, wakifungwa mchezo huu utakoma" anasema.

Pia wanafanya juhudi za kuwasiliana na Zanzibar ili kupanga jinsi ya kuwabana watakaonyimwa leseni bara kwani haitokuwa na maana kama wavuvi hawa haramu watakaponyimwa leseni kwa upande wa mmoja huku upande mwingine wakipewa.

"Kwenye upande wa bahari hatuna muungano hivyo tunawasiliana na wenzetu wa Zanzibar ili kupanga mikakati ya pamoja ya kuwabana watu hawa, haitokuwa na maana tukiwanyima leseni huku kwetu wakati kule wenzetu wanawapa au kule wamenyimwa huku tunawapa, tunataka tuwe na msimamo mmoja"

Aidha kuanzia sasa Wizara kwa kushirikiana na vyombo vya dola wataanza kutembelea masoko ya samaki ili kukagua samaki waliovuliwa na mabomu ili waweze kuwaonyesha wahusika wakuu na kisha wote watakamatwa na kukabidhiwa kwenye mikono ya sheria.

Suala lingine alilolizungumzia ni juu ya kufunga kanda za uvuvi ili kutoa nafasi kwa mazalia mapya ya samaki hususani kamba ambao ndio wamepungua kwa kasi kutokana na uvuvi haramu.

Alichukulia mfano zoezi lililofanya na nchi za Angola, Kenya, Zambia na Msumbiji ambao walizuia uvuvi kwa kipindi cha miaka mitatu na ilipofunguliwa idadi iliongezeka, hivyo wanataka kujaribu njia hiyo kwa hapa nchini kwa walau mwaka mmoja kama ilivyoshauriwa na watafiti.

Jambo lingine Magufuli ameshauri kuanzishwa kwa ufugaji wa samaki pasipo kutegemea wanaotoka baharini pekee na kuagiza sehemu zote kulipo na mabwawa na ranchi za mifugo zifugwe samaki ukizingatia ng'ombe hawali samaki hivyo wanaweza kufugwa bila tatizo.

Hata hivyo alisema ili kuweza kukabiliana na matatizo yote haya na kuhakikisha kwamba sekta ya uvuvi inachangia zaidi ya asilimia 3 ya pato la uchumi wa taifa ni sharti kuanzishwe kwa 'Beach Management Zone' ambazo ndio pekee zitakazoweza kusaidia ulinzi wa rasilimali za baharini.

Anasema kwa kupitia mpango huu ambao ni kwa mujibu wa sheria ya 22, ya mwaka 2003 kifungu cha 18, itaweza kusaidia kupambana na wezi wa rasimali za taifa sambamba na kuanzishwa kwa vikundi vya wavuvi.

"Kuna bilioni 51 zimetengwa kwa ajili ya kusaidia shughuli za uvuvi kwa kupitia mradi wa MACEMP ambao wakati wa uchaguzi kuna watu walisambaza habari potofu kwamba ni mradi wa CCM kwa ajili ya uchaguzi hivyo wengi wakaacha kuunda vikundi, lakini sasa itabidi watu wajitokeze ili tutumie fedha zile" anasema Magufuli.

Waziri Magufuli anasema serikali inatambua umuhimu wa sekta hiyo ndio maana ikaamua kutoa kipaumbele cha pekee kwa kuwekwa kwenye Wizara ambayo hatokuwa na shughuli nyingi.

Hivyo alitoa wito kwa wadau wenyewe wa sekta ya uvuvi kuanzia Chama Cha Wafanyakazi wa Meli (WAMEUTA) na taasisi nyingine zinazohusika na sekta hiyo kutoa ushirikiano kwa serikali ili iweze kujua nini haswa cha kufanya ili kuongeza tija katika sekta hiyo.

Hata hivyo alitoa ahadi katika bajeti ijayo ya wizara hiyo atahakikisha kwamba kunatengwa walau fungu kidogo ambalo litachangia kwenye vyama vya wavuvi wadogowadogo, wafanyakazi wa meli na vyama vingine ili ziweze kuchangia kuboresha shughuli zao ikiwemo kununulia zana bora za uvuvi.

0
No votes yet