Watawala hawatatuburuza tena


M. M. Mwanakijiji's picture

Na M. M. Mwanakijiji - Imechapwa 20 April 2011

Printer-friendly version
Kisima cha Mjadala

WANANCHI wakijua vizuri nguvu waliyonayo juu ya watawala wao na wakaitumia vizuri nguvu hiyo, watawala watalazimika kufikiri mara mbili kabla ya kuwabambikizia wananchi sheria mbovu.

Nguvu iliyotumika kujenga hoja katika muswada wa sheria ambayo ilitakiwa isimamie mchakato wa mapitio kuelekea Katiba Mpya, imeonyesha kuwa wananchi wanaweza kuzuia serikali yao kuwaburuza.

Muswada wa sheria ambayo ingesimamia mchakato wa kufikia Katiba mpya ulionekana umejaza ndani yake vipengele ambavyo vingefanya wazo zima la Katiba Mpya kuwa halina maana kwani ingemfanya Rais kuwa mdau mkuu wa mchakato huo na siyo wananchi ambao ndio “wenye nchi”.

Hivyo juhudi za kupinga muswada huo zinahitaji kupongezwa na zitakuwa zimefanikiwa sana endapo muswada mpya utakaoletwa Bungeni baada ya kujadiliwa na wananchi utakuwa umeakisi matarajio ya Watanzania na kuweka mfumo ambao utahakikisha wananchi wanatumia haki yao ya kutawala kutengeneza Katiba waitakayo wao.

Kwa bahati mbaya, kwa muda mrefu Watanzania wamekuwa wakikaa pembeni kama watazamaji wakati wabunge wa CCM walipopitisha sheria mbalimbali ambazo utekelezaji wake umetuletea matatizo mengi.

Ni kutokana na kukaa pembeni kwa muda mrefu matokeo yake tumeshuhudia sheria mbalimbali zikiwa tayari kutumika huku zikiwa zimejaa mapungufu mengi na ambayo yana madhara mengi.

Tuna sheria nyingi lakini hapa nitazungumzia zile zilizoingizwa kuanzia 1995 ambazo leo zinatugharimu sana kama taifa kwenye upande wa fedha na hata kwenye maisha ya kawaida. Hapa sitagusa sheria nyingine ambazo tumezirithi kutoka kwa wakoloni au ambazo tuliziandika wakati wa dunia ya vita baridi.

Baadhi ya sheria hizo nimewahi kuzigusia huko nyuma, na watu wengine wamewahi kuziangalia. Ninaamini wananchi tukitumia haki yetu ya kutawala tunaweza kabisa kuendelea kuwalazimisha watawala kubadili mawazo kama tulivyofanikiwa katika sheria mbalimbali kama za Haki ya Maoni, Gharama za Uchaguzi, na hii ya Kuelekea katiba mpya.

 Sheria ya Usalama wa Taifa ya 1996

Mojawapo ya sheria mbaya ambazo zimeandikwa na watu wenye akili na bado ziko vitabuni ni iliyoingizwa na utawala wa Rais Benjamin Mkapa ambayo imedhoofisha sana idara ya Usalama wa Taifa na kuliweka Taifa katika uzio wa kunyanyaswa na mafisadi wa kimataifa na wa ndani.

Sheria hiyo ambayo iliunda rasmi “idara” kama tunavyoijua sasa haikupata kuchanganuliwa kiuwazi na vipengele vyake kuangaliwa kwa karibu. Huu ulikuwa mpango wa makusudi wa kudhoofisha idara ili kikundi cha watu wachache waweza kufanya lolote wanalofanya.

Mojawapo ya vipengele vya ajabu kabisa vilivyoko katika sheria (vipo vingine) ni kile cha Ibara ya 5:2(1). Kipengele hicho kinasema haitakuwa kazi ya Idara kuhakikisha kuwa hatua za kiusalama zinatekelezwa bila kufafanua “hatua za kiusalama” ni zipi na ni kwanini Usalama wa Taifa uzuiwe kusimamia usalama.

Kama watu wangepata nafasi ya kuipitia wangejua ni mojawapo ya nyenzo ambazo zimetumiwa katika kutengeneza mazingira ya kufanya Idara kutumika kisiasa na kuondoa usimamizi unaotakiwa.

Sheria ya Madini ya 1998

Mojawapo ya sheria  mbovu ambazo CCM walizipitisha kusimamia raslimali zetu za madini ni hii ya mwaka 1998.

Hata hivyo imekuja kujulikana ubovu wake baadaye na imekuwa vigumu sana kuifanyia mabadiliko makubwa kwa sababu inagusa maslahi ya “wakubwa” wengi nchini. Madhara yake mengine tuliyaona wakati wa sakata la Buzwagi na masuala mbalimbali yanayohusiana na usimamizi wa sekta ya madini na mapato yanayotokana na sekta hiyo.

Sheria hii inahitaji kuandikwa upya siyo kufanyiwa marekebisho tu.

Sheria ya Fedha ya 2004

Hiii nayo ni mojawapo ya sheria ambazo zimechangia katika matatizo ya kusimamia uchumi. Ikitanguliwa na sheria ya Fedha ya 2001 Sheria hii na hata mabadiliko yake ya baadaye imetufikisha mara kwa mara kwenye mifumo inayokinzana sana ya masuala ya fedha, kodi (pamoja na sheria ya kodi ya 2004).

Wengi wetu tunakumbuka mojawapo ya matatizo yake kwenye suala la Buzwagi na hata leo hii tunaona bado matatizo yake.  Mojawapo ya matokeo ya sheria hii na nyingine zinazohusiana ni kuwa katika mwaka wa fedha 2009/2010 Tanzania ilisamehe kodi mbalimbali zenye themani ya Sh 680.7 bilioni sawa na asilimia 14 ya mapato ya mwaka huo!

Ili kuweza kuweka katika mwanga wa kujua kiasi hicho ni kikubwa kiasi gani ni kuwa Serikali hii iliyosamehe kodi zenye thamani hiyo imetangaza juzi (kupitia Dk. John Magufuli) kuwa imetenga kiasi cha Sh 289 bilioni kwa ajili ya Mfuko wa Barabara ambao unatumika kujenga barabara za manispaa Tanzania nzima. Yaani, taifa ambalo limesamehe bilioni 680 limetenga zaidi ya nusu ya kiasi hicho kwa ajili ya barabara.  Taifa limekubali kujinyima mapato na baadaye linajikuta halina fedha ya kutosha kufanya mambo ya maana.

Sheria ya Kuzuia Ugaidi ya 2002

Sheria hii tuliipitisha kwa haraka kufuatia matukio ya Septemba 11, 2001 kule Marekani baada ya kikundi cha magaidi kulipua jengo la Kituo cha Biashara Kimataifa pale New York na majengo ya miji mingine. Tukiwa marafiki wa karibu wa Marekani tulijikuta tunaletewa muswada wa sheria ambayo kwa kweli hatukuwa na ujanja wa kuukataa.

Siyo kwamba hatukuhitaji muswada wa namna hiyo bali ni kwa kiasi gani tulishirikishwa katika kuandika na sheria hiyo ili kujilinda sisi wenyewe na matukio ya ughaidi?

Sheria ya Gharama za Uchaguzi

Sheria nyingine ambazo nazo zinatuletea matatizo katika siasa zetu ni hizi zinazohusiana na mambo ya uchaguzi. Sheria ya TAKUKURU ya 2007 na hata sheria ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa serikali zote zimetengenezwa kama kuchongwa kwa haraka haraka. Ni sheria mbazo zina majina mazuri lakini hazina vipengele au vitu muhimu kuzifanya ziweze kusaidia katika utawala bora.

Mifano hiyo michache (na zipo sheria nyingine nyingi) inatuonesha kuwa wananchi wanatakiwa kuwa macho wanaposikia “muswada”. Na ili wananchi wengi waweze kujua wakati umefika kwa wasomi wetu na taasisi huru kuwa wachangamfu kuweka hadharani na kuitisha mijadala kuhusiana na miswada hiyo. Wananchi ni lazima watambue kile ambacho wanasiasa wao wanakipanga. Mojawapo ya hatua za kuchukua kuanzia sasa:

a) Tusikubali tena miswada ya sheria zinazowahusu Watanzania kuandikwa tena kwa lugha ya Kiingereza. Tung'ang'anie kuwa sheria zote zinapoandikwa kwa Kiingereza wakati huo huo zipatikane katika Kiswahili.

b) Tusikubali kuharakishwa bali muda uwepo wa kupitia mswada wowote kabla haujafanyika sheria. Tujihadhari sana na haya mambo ya kukimbizwa mchakamchaka kuwa “tupitishe tupitishe”.

Ni lazima tutumie nguvu ya umma yaani uwezo wa wananchi kuishinikiza serikali na viongozi wao kufanya yale ambayo wananchi wanataka kuweza kuhakikisha kuwa maslahi yetu yanakuwa ni ya kipaumbele cha juu zaidi. Na kama ushahidi uliopo unavyoonesha tukiitumia vizuri nguvu hii ya umma watawala wetu hawawezi kutuburuza tena.

mwanakijiji@jamiiforums.com
0
No votes yet