Watetezi wa wafugaji waingia mjini


Mwandishi Maalum's picture

Na Mwandishi Maalum - Imechapwa 16 May 2012

Printer-friendly version
Uchambuzi

WATETEZI wa wafugaji ni watetezi wa mifugo. Basi ni watetezi wa walaji wa nyama ya mifugo hiyo. Kumbe wewe na mimi tunafikiwa na utetezi huu.

Hawa walionekana jijini Dar es Salaam, Jumatano iliyopita. Asasi yao inaitwa PINGOs, kwa ufupi.

Walitoka kuongea na wafugaji, wawindaji na warina asali; wakaingia moja kwa moja katika chumba cha habari cha MwanaHALISI. Wanataka nini?

Wao wanasema wametembelea gazeti kuonana na waandishi na wahariri wao; kuwaeleza wanachofanya, kubadilishana mawazo na kutafuta jinsi ya kufanya kazi pamoja katika kukuza utetezi wa jamii za wafugaji.

Wanatembezwa ofisi ya utawala. Wanapelekwa chumba cha habari. Kwa MwanaHALISI, hapo ndio mwisho. Hakuna ofisi za madoido.

Wageni wanaelezwa jinsi gazeti linavyotengezwa. Nao wanaeleza kilichowaleta na kugawa kabrasha juu ya kazi zao.

Yote hayo yanafanyika kwa muda mfupi ili kutoa nafasi kwa uchambuzi wa gazeti hili litokalo kila Jumatano. Nao wageni ni “washamba.”

Hawakai sana mijini. Hawajui mengi ya mijini. Hata kule ambako wanakaa kwa muda mfupi, sharti kuwe karibu na mahali pao pa kazi.

Sasa wako mjini. Mwandishi huyu alifurahi kumwona Mkurugenzi Mtendaji wa PINGOs, Edward Porokwa.

Mara ya mwisho mwandishi alikutana na Porokwa mjini Banjul, Gambia. Ilikuwa kwenye kikao cha Tume ya Haki za Binadamu cha Umoja wa Afrika (AU) miaka mitatu iliyopita.

Wakati mwandishi alikuwa anaongoza ujumbe wa Taasisi ya Habari Kusini mwa Afrika (MISA) kwenye kikao hicho na kile cha asasi za kijamii za Afrika, Porokwa alikuwa anaongoza ujumbe wa wafugaji kutoka Tanzania.

Upandeni mwa Porokwa, alikuwa Mzee Olkosikosi; mfugaji wa kiwango chake ambaye miaka minne iliyopita, nyumba yake na maboma ya ng’ombe, vilichomwa moto wilayani Loliondo.

Waliochoma mali hizo ni polisi wa Tanzania. Shabaha? Kumwondoa kwenye eneo ambalo linadaiwa kuwa sehemu ya hifadhi ya mbuga za wanyama ambayo imekabidhiwa kwa kampuni ya mtoto wa mfalme wa Falme za Kiarabu.

Mamia ya wakazi wa eno hili, siyo Olkosikosi pekee, walikumbwa na chomachoma; wengine wakapigwa virungu na wengine kufyatuliwa risasi. Vyakula na mali nyingine za wafugaji viliteketea.

Kwenye kikao cha AU, mjini Banjul, serikali ya Tanzania haikupeleka mwakilishi. Angepata shida sana kujibu madai ya wafugaji.

Wafugaji katika maeneo ya mbuga, ambamo wameishi kwa miaka nendarudi, hunywa maziwa ya mifugo yao. Hula nyama ya mifugo yao. Hawali nyama ya wanyamapori.

Kwa msingi huu, wafugaji katika maeneo kama Loliondo, wamekuwa walinzi wa misitu, mbuga  na wanyama.

Lakini zawadi wanayopewa kwa kazi hii ya kuhifadhi na kulinda raslimali za taifa, ni kupigwa, kufukuzwa makwao, kuchomewa makazi.

Hapo ni pale wanapofukuzwa sasa. Waliofukuzwa zamani kutoka makazi yao, leo wanaambiwa “rudi kwenu.”

Kule Ihefu, wilaya ya Mbarali, mkoa wa Mbeya, wafugaji wanaambiwa warudi kwao. Walifukuzwa kwa kiboko. Vivyo hivyo Kilosa, mkoani Morogoro na sehemu nyingine nchini.

Miongoni mwa wanaofukuzwa na wasio na makazi, ni wale waliohamishwa kutoka Hanang, mkoani Arusha ili kutoa nafasi kwa kilimo cha mpunga katika maeneo ya Katesh, Setchet, Basotu Basodesh.

Zaidi ya wananchi 10,000 walitupwa nje ya makazi yao, ili eneo “lichukuliwe na mpunga.” Hiyo ni zaidi ya miaka 30 sasa. Leo hii, hata mpunga haupo tena; na wafugaji bado wanahamahama.

Waling’olewa kama magugu. Wakatupwa kwenye mwamba. Wakaachwa iwe itakavyokuwa. Wana mengi ya kusimulia. Machozi hayatiririki tena. Macho ni makavu; bali ulimi ungali na neno. Wanasema, watasema hadi kaburini.

Hao ndio Porokwa na wenzake wanasemea. Ndio wanatetea. Angalau wapate makazi; na ambao hawajatoka makazini mwao wabaki walipo.

PINGOs hawana cha kuwapa wafugaji kufuta machozi, kuondoa mikasa, kufidia mali zao au hata kuwafariji. Hawa wanatafuta njia ya kufanya sauti za wafugaji zisikike.

Matumaini: Sauti zikisikika, watawala wanaweza kufumbuka macho; kufunguka masikio na hata kuchukua hatua. Hatua yaweza kuleta mabadiliko. Ndio maana PINGOs hawalali.

0
No votes yet