Watu, petroli, sukari ndani ya boti


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 30 May 2012

Printer-friendly version
Ripoti Maalum

HAPA ni mwaloni Kirumba; moja ya bandari bubu zilizomea kama uyoga kwenye mwambao wa Ziwa Victoria mjini Mwanza.

Mbele yangu kuna boti iliyojengwa kwa mbao na mabati; inaonekana kuchakaa. Inapakia abiria na mizigo, tayari kung’oa nanga kwenda moja ya visiwa vingi vidogo vya Ziwa Victoria.

Nachungulia ndani ya boti hii. Naona maboya machache yamechomekwa ndani ya gunia kuukuu. Sioni vifaa vya kuzimia moto. Sioni kisanduku cha Msaada wa Kwanza(First Aid).

Kama ada, wapagazi wanaendelea kupakia mizigo – viroba vya sukari, chumvi, maboksi ya sabuni; magudulia ya mafuta ya taa na petroli. Tayari ndani ya boti hiyo kuna abiria walioketi  kimya. Wengine wanaendelea kuingia. Wote wanaona aina ya mizigo inayopakiwa, lakini hakuna anayestuka.

Hakuna mwenye hisia wala muda wa kuhoji iwapo boti ina maboya ya kutosha; ina bima au vifaa vya kuzimia moto.

Hii ndiyo sura ya usafiri wa boti, kutoka na kuingia kwenye bandari bubu zilizoko mwambao wa Ziwa Victoria. Mwandishi amechukua siku sita kuzungukia bandari hizi na kuona jinsi boti zinavyofanya kazi.

Takwimu zinaonyesha kuna boti zaidi ya 10,000 katika ziwa upande wa Mwanza. Kuna meli 47 ziwani ambazo zimesajiliwa. Kwa lugha iliyozoeleka, kubna “utitiri” wa boti. Lakini hazitoshelezi mahitaji ya wasafiri.

Je, Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) inajua haya?

Alfred Wariana, Ofisa Mfawidhi wa Sumatra mkoani Mwanza, anakubaliana na idadi hiyo ya boti na kwamba vyombo hivi vinasafirisha abiria na mizigo kwenda Sengerema, Geita, Ukerewe na visiwa vingi vidogo.

“Huwezi kusema boti na meli zote, kwa asilimia miamoja, hufuata sheria na kuzingatia maelekezo,” anaeleza ofisa huyo kwa sauti la malalamiko.

Anasema Sumatra Mwanza wana wakaguzi watatu tu. “Tuna mtandao usiotosheleza udhibiti wa wasafirishaji wasiopenda kutii sheria pasipo shuruti,” anaeleza.

Katika ziwa hili, kuna visiwa vipatavyo 60. Ukerewe peke yake kuna visiwa 38.

“Siyo rahisi kuwafikia wamiliki wote wa vyombo vya majini, hususan vidogo na kuvikagua kila mara. Unajua, ziwani siyo kama barabarani, ambako utaweka vizuizi na kufanya ukaguzi ili kubaini wahalifu,” anafafanua Wariana.

Lakini anasema polisi na watendaji wa vijiji wapo katika maeneo ya vituo vya kibiashara ambako boti hizi hutia nanga na kubeba au kuishusha bidhaa.

“Hawa wanapaswa kuwatia mbaroni wasafirishaji wasiozingatia sheria za usafirishaji majini,” anaeleza.

Kila anayeangalia jinsi boti zinavyojaza abiria, haraka anapata kumbukumbu ya mv Bukoba iliyopinduka na kuzama ziwani humu tarehe 21 Mei 1996. Kwa mujibu wa takwimu za serikali, zaidi ya watu 800 waliangamia katika meli hiyo.

0
No votes yet