Watuhumiwa aina ya Chenge wametuloga


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 29 June 2011

Printer-friendly version
Tafakuri
Mtuhumiwa kashfa ya Rada, Andrew Chenge

WAAFRIKA wana kitu kimoja kinachowaunganisha, pale wanapokosa jibu katika mambo magumu yanayokabili na kuhitaji kusumbua bongo, jibu lao huwa rahisi mno – kulogwa.

Ni akili ya mtu aliyelogwa tu kama anaruhusu mijadala ya aina tunayoisikia na kuona katika Bunge letu. Ni kulogwa hukuhuku kunakoruhusu wabunge, na hasa serikali, kuhalalisha matumizi ya kodi za wananchi bila ya kujiuliza nini hasa faida ya matumizi hayo.

Wiki iliyopita, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, aliwasilisha tamko la serikali kuhusu tabia ya kudhalilisha ya shirika la kutengeneza zana za kujeshi la Uingereza, BAE System la kukataa kutoa chenji ya rada kwa serikali na badala yake inataka kuipeleka kwa mashirika ya kiraia ya Uingereza. Fedha hizo zinafikia dola 30 milioni.

Membe alizungumza kwa hisia kali. Akashangiliwa na wabunge, hasa wa chama tawala - CCM, kufikia hatua ya kusema kama BAE haitatoa fedha hizo kwa serikali, ijue hakuna NGO ya Uingereza itakayoruhusiwa kufanya kazi nchini kwa kupewa fedha hizo.

Membe alisema mengi, lakini yote yalionyesha jinsi BAE System, kampuni iliyoshiriki mchezo mchafu wa kuizuia Tanzania rada ya bei mbaya wasivyoiamini serikali ya Tanzania wakati serikali ya Uingereza mwaka baada ya mwaka wamekuwa wakiipatia Tanzania misaada mbalimbali inayopitishwa katika mikono ya serikali. Membe alisema ikiwezekana, Tanzania itasusia fedha hizo.

Wakati Membe akiendelea na tamko lake, timu ya wabunge kadhaa ikiongozwa na Naibu Spika, Job Ndugai, ilikuwa Uingereza ikifuatilia chenji hiyo.

Spika Anna Makinda ameridhia wabunge kwenda Uingereza kwa ajili hiyo, ameridhia matumizi ya fedha za serikali; lakini baada ya kuwasilishwa kauli ya serikali na mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, kuomba ijadiliwe, Spika hakuona sababu wala uharaka wa kufanya hivyo. Badala yake, alisema utaratibu utapangwa baadaye.

Ninasema haya yote si kwa sababu sikubaliani na serikali kudai chenji hiyo, na wala si kwamba naunga mkono BAE System kuweka masharti ya kurejesha chenji hiyo kwa kuwa kimsingi inachofanya ni mwendelezo wa usanii baada ya ule wa awali wa kukwepa kutiwa hatiani kwa rushwa na badala yake kukiri kosa la kutoweka vizuri kumbukumbu za kihasibu katika ‘rushwa’ ya dola 12 milioni waliyopewa watu waliofanikisha dili ya ununuzi wa rada hiyo.

Rada hii ilisababisha aliyekuwa Waziri wa Misaada ya Maendeleo wa Uingereza, Claire Short, maarufu kama ‘mama rada’ kugombana na Waziri Mkuu wake, Tony Blair lakini ni rada hii pia ilisababisha aliyekuwa Waziri wa Miundombinu wa Tanzania, Andrew Chenge, kujiuzulu Aprili 2008.

Chenge, ambaye ni mbunge wa Bariadi Magharibi, alijiuzulu uwaziri baada ya kugundulika kuwa na kitita cha Sh. 1.2 bilioni katika akaunti yake moja kwenye benki iliyoko Visiwa vya Jersey, Uingereza.

Chenge alitajwa katika uchunguzi wa makachero wa Taasisi ya Makosa Makubwa ya Jinai ya Uingereza (SFO) kama mtu muhimu katika ununuzi wa rada hiyo akituhumiwa kunufaika na kamisheni hiyo kubwa kuwahi kutolewa.

Ukipima namna suala hili linavyopelekwa unapata jibu moja tu, tumelogwa: Kwanza Membe alikuwa Uingereza pamoja na mambo mengine akifuatilia chenji hiyo; sasa timu ya wabunge imekwenda kufuatilia chenji hiyo; na tamko kali la serikali limewasilishwa bungeni.

Hisia ni kali, lakini watu hawataki mjadala wa jambo kuu la msingi ambalo ni si jingine ila ni nani hasa wezi wetu? Nani alishiriki mchezo huu mchafu wa kuingiza taifa katika balaa la gharama kubwa kama hili? Wako wapi? Mbona hawazungumzwi? Nani alipewa nini na kwa sababu gani?

Chenge ambaye ni mmoja wa watuhumiwa wakuu wa balaa hili kwa kuwa wakati linapangwa na kutekelezwa, alikuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ametajwa na SFO kuwa mhimili wa mpango, na pia akihusishwa na kunufaika na kamisheni ya dola 12 milioni. Yuko bungeni.

Hivi wakati Membe akitoa kauli ya serikali kwa hisia kali, mhusika muhimu katika mpango mzima, alikuwa ndani ya Bunge, ni mbunge, ni kiongozi wa CCM na hivi majuzi tu alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya CCM na Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hiki kabla ya kamati hiyo kuvunjwa na kuundwa upya Aprili mwaka huu.

Chenge bado ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya (NEC) ya CCM. Yumo. Amejaa tele, bungeni na CCM. Amesheheni kweli kweli!

Kinachosumbua Watanzania wengi ni kuona eti Bunge la Tanzania, Serikali ya Tanzania (Utawala) kwa pamoja wameshindwa hata kutoa tamko kuhusu wezi wa fedha ya rada badala yake wakafungulia mashitaka mtu asiyekuwepo nchini huku kukiwepo tuhuma kuwa alisaidiwa kuondoka.

Watuhumiwa wengine wako ndani bungeni wakitamba na kujitapa kwamba walisomeshwa na serikali ya nchi hii tena zama za Mwalimu Nyerere, lakini wao wamelipa taifa hili machungu; machungu ya rada, machungu ya kuuza kifisadi mashirika ya umma; machungu ya kuitumbukiza nchi katika mkataba mibovu kama wa TRL na RITES. Kila kitu na upande ni machungu.

Nashindwa kufikiri sawasawa, nini hasa kinampa Spika ujasiri wa kuruhusu matumizi ya kodi kwa wabunge kufuatilia chenji ya rada nchini Uingereza lakini hawezi kuunda kamati teule ya Bunge kuchunguza wezi wetu wa rada.

Nashindwa kujua nini kinamzuia Membe kuanzisha hatua za kuwaadhibu watuhumiwa wetu bungeni bali analalamikia chenji ya rada wakati watuhumiwa wakiwa wanamuangalia hivihivi tu.

Unapokuwa huna majibu ya maswali haya magumu, kwamba kwa vipi taifa linalinda na kuwaenzi watu wanaotembea na tuhuma nzito za kuhujumu uchumi kupitia ununuzi wa rada kwa bei ya kuruka.

Jibu rahisi ni moja tu. Tumelogwa. Hili ni jibu la Kiafrika la aina ya Tanzania ambao kwao kukaa na kuwalinda watuhumiwa wa wizi si kitu, isipokuwa kufukuzana na makombo yaliyosazwa na watuhumiwa hao, hakika kila gharama itatumika, huku ni kulogwa kubaya.

0
Your rating: None Average: 4 (2 votes)
Soma zaidi kuhusu: