Watuhumiwa wa ufisadi hawasafishiki


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 24 June 2008

Printer-friendly version

WALE wanaoitwa watuhumiwa wa ufisadi hawajasafishwa. Vikao vya Chama Cha Mapinduzi (CCM) vilivyofanyika mkoani Dodoma wiki mbili zilizopita, kamwe haviwezi kuwasafisha.

Hakika, havijafanya kazi hiyo na hata kama vingefanya, bado kazi waliotaka kuibariki, isingekidhi matakwa ya umma na hata ya kisheria.

Kikao cha Kamati ya wabunge na kile cha wabunge na wajumbe wa Halmashauri Kuu (NEC), havina mamlaka ya kutengua maamuzi ya Bunge.

Wiki mbili zilizopita, wabunge wa CCM na wajumbe wa NEC walikutana mjini Dodoma, katika kile kinachoitwa "kikao cha kusafisha mafisadi."

Mkutano wa wabunge na wajumbe wa NEC ulihudhuriwa pia na mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete. Karibu wajumbe wengi waliozungumza, walitetea watuhumiwa. Baadhi yao walifikia hatua hata ya kunyooshea vidole wenzao.

Lakini aliyelengwa alikuwa Edward Lowassa. Inawezekana huo ndiyo uliokuwa mkakati wa kwanza. Kwamba kwanza asafishwe Lowassa halafu watasafishwa wengine.

Wengine waliotajwa kutaka kusafishwa ni mbunge wa Igunga, Rostam Aziz, Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi na aliyekuwa Waziri wa Miundombinu Andrew Chenge.

Rostam ametajwa na wapinzani kwamba ndiye mmiliki wa kampuni ya Kagoda Agriculture Limited (KAL). Ni Kagoda pamoja na kwamba anwani zake zote zina utata, ilichotewa dola za Marekani 30,732,658.82 (sawa na zaidi ya shilingi bilioni 40 za Tanzania) kwa kazi ambayo serikali imekataa kutolea maelezo.

Aliyekuwa waziri wa Fedha, Zakia Meghji, alisema fedha hizo "zilitolewa na serikali kwa kazi maalum ya serikali." Kwa maneno mengine, Meghji alitaka kuaminisha umma kwamba Kagoda ilipewa fedha kwa ajili ya kununua vifaa vya Idara ya Usalaa wa Taifa.

Lakini alipoona uwongo wake hauwezi kukubalika, mara moja akaamua kufuta barua yake aliyoiandika kutetea kampuni hiyo. Mwisho akaishia kutupa tuhuma na lawama kwa aliyekuwa Gavana wa BoT, Dk. Daud Balalli, kwamba alimpotosha.

Fedha hizo ni miongoni mwa mabilioni ya shilingi ambayo serikali, kupitia Wizara ya Fedha na BoT, ilichotea washirika wake mbalimbali katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2005.

Inaelezwa kuwa hata rais mstaafu Benjamin Mkapa hakuachwa nyuma. Alitetewa na Rostam. Kilichomfanya Rostam kumtetea Mkapa, hakijajulika. Lakini lililodhahiri ni kwamba alikuwa anatafuta kinga kupitia mgongo wake.

Rostam anajua kuwa Kikwete asingependa kumshitaki Mkapa. Anajua jinsi ugumu huo ulipo. Lakini anajua kwamba iwapo Kikwete atazidi kung'ng'aniwa hasa na wafadhiri, uwezekano way eye kusalimika ni mdogo.

Na sasa anaona hatari hiyo kuwa iko wazi zaidi. Ni kutokana na hatua ya Kikwete ya kukubaliana na wafadhiri, kwamba angalau serikali ipeleke vigogo watano mahakamani ambao ni watutuhimuwa wa ufisadu kila mwaka. Je, hao ni kina nani?

Bila shaka Rostam amenusa na ndiyo maana ameamua kumtetea Mkapa. Kwamba ama aachwe pamoja naye, ama kama itafikia hatua ya kutumbukia, watumbukie kwa pamoja.

Ni fedha hizo ambazo baadhi ya wabunge wamesimama kidete kuhakikisha kwamba wahusika wanaachia uongozi. Ni fedha hizo na nyingine ambazo wabunge mahiri wa CCM na wale wa upinzani, wanataka wahusika wachukuliwe hatua za kisheria. Ni shinikizo hilo lililosababisha kufanyika kwa vikao hivyo.

Ni wazi kwamba wapo baadhi ya wajumbe waliotaka kutumia vikao hivyo kujisafisha, ama kusafisha wengine. Lakini ukweli ni kwamba mikusanyiko hiyo, haina uwezo wa kufuta maamuzi yaliokwisha fikiwa.

Hii ni mikusanyiko inayoweza kufananishwa na vijiwe, ama kumbi za soga. Ndiyo maana haikusangaza rais Jakaya Kikwete ambaye ni mwenyekiti wa chama hicho kukubali moja ya vikao hivyo, hata pale ilipobainika kwamba kikao kilikuwa hakina ajenda.

Kwamba mahafidhina, wakiongozwa na Katibu wa Kamati ya Wabunge wa CCM, Ali Amir Mohammed na Katibu Mkuu wa chama hicho, Yusuf Makamba waliamua kuficha ajenda za kikao.

Awali ilikubaliwa kuwa kila mbunge aandae ajenda yake. Sektalieti ya chama itazichuja na kupata ajenda moja ambayo ingewasilishwa Kamati Kuu (CC). Hayo ndiyo yalikuwa makubaliano.

Na hivyo ndivyo wabunge wa CCM walivyofanya. Lakini baada ya baadhi ya wabunge kuwasilisha ajenda iliyotaka Makamba ang'oke katika wazifa wake, wahusika wakaamua kuficha ajenda.

Lakini hiyo haikuzuia wabunge wa CCM kupeleka kilio chao kwa Kikwete na wenzake. Pamoja na kwamba walikutana katika kikao ambacho hakikuwa na ajenda wala mamlaka ya kutengua maamuzi yaliokwishafikiwa.

Rafiki yangu mmoja anafika mbali zaidi. Anasema kutaka kusafisha mafisadi katika kama kile, ni sawa na mtu anayehukumiwa na Mahakama ya Rufaa, lakini akapeleka rufaa yake Mahakama ya wilaya.

Hii ni kwa sababu, kwa mujibu wa katiba ya CCM, chama hicho kina vikao vitatu vyenye maamuzi. Kikao cha Kamati Kuu, Halmashauri Kuu na Mkutano Mkuu. Hata hivyo, vikao vyote hivyo haviwezi kufuta maamuzi ya Bunge.

Mkutano mkuu ndiyo kikao cha mwisho katika chama. Ndiyo chenye maamuzi ya kubadilisha chochote kiliachoamuliwa na vikao vya chini.

Hata hivyo, mkutano mkuu wa chama chochote hauna ubavu wa kubatilisha maamuzi ya Bunge. Maamuzi haya yanaweza kubatilishwa na mahakama pekee.

Kutokana na hali hiyo, mkutano kati ya wabunge na wajumbe wa NEC, haiwezi kuwa mikutano ya kusafisha mafisadi. Huu unaweza kuwa mkusanyiko wa watu kujifurahisha.

Katika Ripoti yake, Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza mkataba wa kinyonyaji kati ya serikali na kampuni ya Richmond Development Company (LLC), Kamati ilidhirika kwamba, ama Lowassa alizembea, ama alinyamazia mkataba huo.

Mpaka sasa hakuna ambaye anaweza kubishia ukweli huo. Hata Lowassa mwenyewe hawezi kubisha. Ndiyo maana alipopewa nafasi ya kujitetea ndani ya Bunge, alishia kulalama "Nimeonewa sana. Nimefedheheshwa sana na nimedhalilishwa sana."

Lowassa wala hakujihangaisha kusema kwamba hakuhusika. Hakukana amri zake zilizotajwa kwamba alikuwa anazitoa kwa mawaziri na makatibu wa wizara (Nishati na Madini, Fedha na ofisi ya mwanasheria mkuu wa serikali).

Hakufanya hivyo kwa sababu anajua kuwa hayo aliyafanya. Anajua kwamba hata wenzake wanajua. Wengine wanasema aliogopa kwani baadhi ya wahusika walikuwa wamejiweka tayari kutoa vimemo alivyowatumia.

Hata Karamagi, pamoja na maelezo marefu aliyoyatoa aliishia kusema kwamba alitoa maagizo ya kuhamisha mkataba kutoka Richmond kwenda Dowans akiwa nje ya nchi; alifanya hivyo kwa maslahi ya taifa.

Hakukana kwamba aliongeza mkataba kutoka mwaka mmoja wa awali, hadi miaka miwili. Hilo hakulisema. Lakini kikubwa ambacho hakiwezi kukanwa na wote, ni kwamba kwa muda wote wahusika walikuwa wanafanya kila liwezekanalo kuficha ukweli.

Hii maana yake ni kwamba walijua walichokifanya na hivyo walitaka umma usifahamu "dili yao."

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: