Watumishi wa umma acheni dhuluma


editor's picture

Na editor - Imechapwa 23 June 2009

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

KATIKA kuhimiza uwajibikaji kazini na utumishi adilifu, serikali imekuwa ikiadhimisha wiki ya utumishi wa umma kila mwaka.

Mwaka huu, wiki hii iliadhimishwa sambamba na mkutano wa wataalamu wa utumishi wa umma kutoka nchi mbalimbali Afrika.

Hivi utumishi bora ndio nini? Ni utumishi unaozingatia haki, nidhamu, uadilifu, usawa, utu, uwajibikaji na uzalendo wa kweli kwa kila mtumishi.

Wakati haya yanachukuliwa kama vigezo vya utumishi bora, uzoefu unaonyesha kuwa ni watumishi wachache mno wanaoyazingatia.

Kila tunapoangalia kiwango cha ushughulikiaji malalamiko katika ofisi za umma, tunapata hofu kubwa.

Unakuta mwananchi anapeleka barua katika ofisi ya umma, lakini hapati jibu; hata lile la kutaarifu kuwa suala lake linashughulikiwa au limetupwa.

MwanaHALISI lina lundo la malalamiko na vielelezo vingi vinavyoonyesha mifano ya watu wengi wanaosubiri kwa zaidi ya mwaka sasa, ufumbuzi wa matatizo waliyowasilisha serikalini – wizara na taasisi zake.

Katika hali kama hii, ni nani kinara wa kuongoza harakati za kukomaza utumishi uliotukuka mawazoni mwa watumishi wa serikali?

Ajabu ni kwamba mtumishi akishikishwa pesa, ambazo kwa hakika ni rushwa, anachukua hatua haraka kufuatilia shida anayopaswa kuishughulikia bila ya kudai chochote.

Sasa mwenendo wa mtumishi kutaka “Kitu Kidogo (KK)” ndipo amhudumie mtu, imekuwa ada hata kwenye wodi hospitalini. Balaa isiyo kifani!

Iwapi haki ya mtumishi kudai mapato nje ya utaratibu, kanuni na sheria? Nani ametoa ruksa ya kukaba koo watu wanaohitaji huduma na kuwalazimisha kutoa chochote ndipo wahudumiwe?

Kama wanavyoumia wananchi wenye shida zinazosubiri ufumbuzi serikalini, ndivyo MwanaHALISI tunavyoumia kuendelea kusikia simulizi hizi.

Watanzania na wageni wana haki ya kuhudumiwa na serikali. Wanayo pia haki ya kuchagua wa kumlalamikia wanaponyimwa au kucheleweshewa huduma na ofisi husika ya umma.

Wanajiuliza kama tunavyojiuliza; waendelee hadi lini kubena shingo na roho wakiichukia serikali isiyowajibika kwao, lakini isiyokubali kutoka madarakani?

Lazima mtumishi wa umma ajali kazi aliyoajiriwa kuifanya na ambayo kutokana nayo anapata mshahara. Na watumishi wakumbuke mshahara wanaolipwa unatokana na kodi wanayotoa wananchi hawa wanaowadharau.

Tunapohoji yote haya, tunajenga imani ya mabadiliko. Kwani utumishi uliotukuka ndio maratajio ya wananchi.

0
No votes yet