Watumishi wanaugua posho, uvivu


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 06 July 2011

Printer-friendly version
Tafakuri

TUJIULIZE maswali magumu leo. Hivi kama akina Edward Lowassa, Andrew Chenge na Rostam Aziz wakijivua nyadhifa zao zote ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wakaachia ubunge wanaoshikilia kule Monduli, Bariadi Magharibi na Igunga, tutakuwa tumetatua matatizo ya kuzorota kwa utumishi wa umma?

Nauliza swali hili la kizushi kwa sababu nyingi. Mwaka jana Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) alibainisha kwamba serikali ilikuwa imetoa msahama wa kodi wenye thamani ya zaidi ya Sh. 640 bilioni.

Mwaka huu kabla ya kusomwa kwa bajeti ya serikali, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alishuhudia Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo akisaini makubaliano ya msaada wa wafadhili wanaosaidia bajeti ya serikali wa Sh. 820 bilioni kwa ajili ya mwaka 2011/12.

Sherehe hizo zilifanywa kwa mbwembwe kana kwamba wafadhili walikuwa wanatoa msaada wa asilimia 100 katika bajeti yetu.

Walisifiwa. Nami nasema wamefanya vizuri kutusaidia. Lakini walichosaidia ukitoa misamaha ya kodi inayotolewa na serikali kila mwaka ni sawa na kusema tungeweza kupata fedha hizo kwa asilimia mia kama tungekaza buti kwa sababu bakaa linaloonekana hapa ni kiasi cha Sh. bilioni 200 hivi.

Lakini tukiachana na habari ya misamaha ya ovyo ya kodi, ukichungulia kwenye halmashauri zetu, huwezi kuamini kwamba watumishi wa umma wanaweza kutafuna fedha za walipa kodi na wakabaki kama walivyo bila kuchukuliwa hatua. Hili linahitaji mjadala wa kipekee kwamba wanalindwa na nani miaka yote hii?

Tuachane na misamaha ya kodi na wizi wa fedha za halmashauri. Tujiulize, hivi adha ya mgawo huu wa umeme imeletwa na nani?  Nini chanzo cha kushindwa kutimia kwa miradi mikubwa ya umeme?

Serikali iliahidi miradi ya megawati 645 ingekuwa imekamilika ilipofika mwaka 2010, lakini ni megawati 145 tu zilizopatikana. Najiuliza kinachokwamisha miradi hii ni nini?

Natambua Chenge alikuwamo wakati IPTL inasainiwa miaka ya 1990 akiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali; kadhalika najua kwamba Lowassa alihusika kwa asilimia nyingi katika suala la Richmond na Dowans kwani ndilo lilimfanya ajiuzulu wadhifa wake wa Waziri Mkuu Februari 2008; vivyo hivyo kwa Rostam ambaye naye alihusika na Richmond na Dowans kwa kiwango kikubwa kwa kuwa mwakilishi  aliyetambuliwa kisheria.

Je, baada ya kutoswa mbona umeme bado hakuna? Kelele zinazopigwa mitaani ni kwamba serikali imeshindwa kutimiza wajibu wake; imeshindwa kukabiliana na watuhumiwa wa hujuma kubwa za uchumi; imeshindwa kutekekeza kwa wakati ahadi rundo zilizotolewa wakati wa kampeni; na kwa hakika kila siku mpya tunayojaliwa na Muumba inakuwa afadhali ya jana.

Ukitazama kwa kina utagundua kwamba inawezekana kwamba wakati Bunge likiendelea kujadili makadirio ya matumizi ya wizara mbalimbali na wakati huo huo mwaka wa fedha wa 2011/12 ukiwa umekwisha kuanza, ni dhahiri shahiri kuwa haitufikishi kokote.

Kwa mfano, ukitazama kwa kina Juni 8, mwaka huu wakati Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo anawasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya serikali kwa mwaka 2011/12 thamani ya dola moja ya Marekani ilikuwa sawa na Sh. 1,550.90, lakini ilipofika Julai mosi siku bajeti mpya inaaza kufanya kazi, thamani ya dola moja ilifikia Sh. 1,587.90. Hivi ni viwango vya Benki Kuu ya Tanzania (BoT). Viwango hivi kwenye maduka ya kubadili fedha za kigeni vimefikia zaidi ya Sh. 1,600 kwa dola moja ya Marekani. Viwango hivi leo vinatisha mno!

Tathmini ya kuporomoka kwa sarafu ya Tanzania kwa kiwango hicho maana yake ni kwamba thamani ya bajeti ya Tanzania ya Sh. trilioni 13.5 iliyosomwa Juni 2011, ilipotimia Julai mosi, 2011 ilikuwa imeporomoka thamani yake kwa Sh. bilioni 323. Hizi ni fedha nyingi.

Tujiulize, hivi nini kinafanya serikali kushindwa kuibuka na mikakati ya kulinda sarafu yetu? Hivi hizi ni njama za ‘mafisadi’ pia? Hivi matatizo haya ni ya kujivua gamba pia? Hivi kupiga marufuku kuingiza bidhaa za ovyo ovyo, ambazo hazina maana katika kuongeza thamani katika uchumi, kuna ugumu gani, mbona hatua hazichukuliwe?

Tanzania inawezakana ikawa ni nchi pekee duniani ambako viongozi wake wanaamini kufanya vitu kihuria mno. Ukisikia viongozi wa serikali wikilalamika kuhusu matumizi ya ovyo ya watumishi wa umma, utadhani kwamba hawana nguvu na mamlaka ya kudhibiti watu hao.

Mara kadhaa Waziri Mkuu Pinda amekuwa akilalamika juu ya tabia ya watumishi wa umma kutamani sana anasa, hasa katika manunuzi ya magari ya kifahari. Lakini kinachonisikitisha ni pale Pinda naye anashindwa kuwawajibisha wahusika na kuonekana akilalamika kana kwamba hana nguvu za maamuzi. Nani sasa achukue maamuzi?

Ukitafakari matatizo mengi ya nchi hii yanaangukia kwenye kitu kimoja tu, maamuzi ya ovyo na kulindana. Katika mkutano wa Bunge la bajeti unaoendelea Dodoma hoja kubwa iliyorindima ni posho.

Katika bajeti ya mwaka 2011/12 serikali imetenga takribani Sh. 1 trilioni kwa ajili ya posho, tena ikipendekeza watumishi wake wasilipe kodi kutokana na posho hizo. Kulikuwa na mvutano mkubwa kati ya kambi ya upinzani na ile ya serikali ikisaidiwa na wabunge wa chama tawala.

Utetezi wa posho ulifanywa kwa nguvu na serikali wakati kimsingi imezindua Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa miaka mitano hadi 2015, ambamo inaelezwa wazi kwamba itapunguza matumizi yasiyokuwa na tija zikiwamo posho.

Posho ni ugonjwa wa serikali. Ni ugonjwa ambao umeua ufanisi na tija. Ni dudu linalotafuna kodi za wananchi bila sababu yoyote ya maana. Hapa hakuna ubishi ndicho kiini cha kushindwa kuwajibika kwa watumishi wa serikali.

Nina mifano hai ya rafiki yangu mmoja anayefanya kazi katika wizara moja ambaye alinieleza wazi, bila posho serikalini hakuna kazi inayofanyika. Aliongeza kuwa hakuna mtumishi wa serikali utamtumwa kufanya kazi fulani kama haina posho. Akitumwa kuhudhuria kikao chochote cha kazi ambayo ndiyo ameajiriwa kwayo kama hakuna posho, haendi na hafanywi lolote.

Ninachosema hapa ni kwamba, ingawa ni kweli mafisadi ni kikwazo kikubwa cha maendeleo ya nchi hii, na kwa hali yoyote wasionewe huruma na waswagwe na kuwajibishwa hasa kufungwa jela, lakini ni vema na haki pia kuutazama utumishi wa umma kwa mapana yake.

Haikubaliki kuendelea na uroho wa posho, uvivu wa kuchukua maamuzi na kukosa ubunifu katika ofisi za umma huku watu wakiendelea kukalia ofisi hizo kana kwamba ni urithi wao. Tunataka mabadiliko na ni lazima yaanze sasa.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: