Waunguja, Wapemba tusigombanishwe


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 20 June 2012

Printer-friendly version

KATIKA toleo lililopita, ukurasa huu wa Waraka wa Wiki, ilikuwepo makala iliyoandikwa na Nyaronyo Kicheere, ikibeba kichwa “Muungano wetu unamnufaisha nani?”

Inasikitisha kuwa Mwandishi alipotosha historia ya Zanzibar, ya kabla na baada Mapinduzi ya 12 Januari, 1964.

Kwanza, waliofanya mapinduzi hawakuwa Waunguja, bali Chama cha Afro-Shirazi Party (ASP) kwa kushirikiana na kile cha Umma Party.

Pili, katika mapinduzi yale hakupinduliwa mtawala wa Kiarabu, bali serikali ya Jamhuri ya Watu wa Zanzibar iliyoundwa baada ya Zanzibar kupata uhuru wake rasmi 10 Desemba 1963, kutoka kwa Mwingereza, ndiyo iliyopinduliwa.

Serikali hii ilikuwa inaongozwa na Waziri Mkuu Mohamed Shamte na ilipinduliwa siku 33 tangu uhuru.

Shamte alitoka Pemba lakini hakuwa Mwarabu, ilhali Ali Muhsin Barwani kutoka Unguja na Badawi Kulateni ambaye alikuwa Naibu Waziri wa Habari wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, wote walikuwa Waunguja wenye asili ya Kiarabu.

Ninalenga kufuta upotoshaji wa historia yetu Zanzibar unaofanywa kwa makusudi ili kugawa Wazanzibari kwa misingi ya Uunguja na Upemba. Jitihada mbaya hizo hazijafanikiwa.

Msomi mmoja, wakati huo akiwa mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kitivo cha Sheria, ambaye hivi sasa ni waziri katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano, alikuja Zanzibar kuendesha semina ya REDET katika ukumbi wa Bwawani.

Akamtaja Mohamed Shamte kuwa mwanasiasa aliyekuwa Mwarabu na eti alikimbilia Uarabuni na familia yake yote. Maelezo yake yalishtua wanaojua kuwa alidanganya. Mmoja wa watoto wa Mohamed Shamte ambaye alikuwepo, alikana taarifa hiyo na kusema baba yao hakuwa Mwarabu na hakukimbia na familia.

Ukweli wasioujua wengi, ni kwamba miongoni mwa watu waliofanikisha mapinduzi ni Waarabu tena weupe – Ali Sultan Issa, aliyekuwa Waziri wa Elimu baada ya mapinduzi na Hashil Seif aliyefanikisha operesheni ya kuvunja jela akishirikiana na Komredi Amour Dughesh baada ya kina Okello kushindwa, ni miongoni mwao.

Hashil ndiye alimpigia simu mzee Aboud Jumbe Mwinyi (Rais wa Awamu ya Pili Zanzibar) na kumfahamisha kuwa Cable and Wireles iko chini ya udhibiti wake, hivyo akataka aifahamishe dunia kuwa Zanzibar imefanya mapinduzi na “tunataka tutambuliwe” (Soma kitabu cha Biographia ya John Okello, Britania, US Documents, Hashil Seif, Al Zenjibari).

Hawa wote ni Waarabu wa Unguja na wenzao wa kuongoza mapambano kama Kanali Ali Mahfoudh, mwanajeshi aliyekuwa Mwarabu mwenye asili ya Yemen, ambaye baadaye alishiriki mapambano ya kuikomboa Msumbiji.

Hata hao wanaojiita Washirazi kama (marehemu) Thabit Kombo, asili yao ni Uajemi au Shirazi na ipo huko Uarabuni.

Ni kweli, vyeo vyote vilishikwa na Waunguja kwa vile Shamte alikuwa mzaliwa wa kisiwa cha Pemba, lakini Waziri wake, Ali Muhsin Barwani, alikuwa Mwarabu wa Unguja.

Wakati huo, bado karafuu ilikuwa na soko zuri duniani lakini wananchi wengi walinyang’anywa mashamba yao tena Waunguja na Wapemba na kupewa watu tofauti kwa utaratibu wa Eka Tatu Tatu. Mashamba hayo mengi yaliishia kutelekezwa na uzalishaji ukapungua.

Kutokana na dhulma kubwa iliyopita, mauaji ya raia wema, na unyang’anyi wa mali za watu, baadhi ya watu walikimbia nchi. Kwa hivyo, si Wapemba tu, hata Waunguja kama Ali Muhsin Barwani, Aman Thani na wengineo walikimbia kwa kuhofia maisha yao.

Hofu ya kuuliwa na wanamapinduzi ilisababisha Wazanzibari wengi kuhamia miji ya Dar es Salaam na Tanga, wakiwemo Wangazija waliozaliwa Unguja baada ya kufukuzwa na Rais Abeid Amani Karume na unyanyasaji wa mtawala wa Pemba, Rashid Abdalla maarufu kama Mamba.

Mathalani, mimi binafsi ni Muunguja na sina hata damu ya Kipemba, lakini sithubutu kumdharau Mpemba hata siku moja; namchukulia kama ndugu yangu wa kuzaliwa na siyo wa kuungana kama Watanganyika.

Hakuna historia inayoonesha kama visiwa hivi viwili viliungana au vilikuwa mbalimbali. Hata enzi hizo za Waarabu vilikuwa pamoja.

Na hapa pia, naomba niweke wazi kuhusu madai kuwa Maalim Seif Sharif Hamad, kwa makusudi au kwa bahati tu, katika kupindi hicho kilishuhudia Wapemba wengi wakijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Ule ni wakati wa utawala wa Rais Jumbe mwaka 1972 aliporuhusu Wazanzibari wote kwenda kusoma Chuo Kikuu. Walionufaika ni vijana wa wakati ule, Maalim Seif akiwa mmojawao. Wengine ni Omar Ramadhani Mapuri, aliyekuja kuwa Waziri wa Elimu Zanzibar na baadaye Waziri wa Mambo ya Ndani Tanzania.

Pia walikuwepo Iddi Pandu Hassan ambaye alikuja kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar; Mohamed Mwinyi Mzale ambaye sasa ni Balozi wa Tanzania nchini Sweden; Juma Duni Haji, sasa Waziri wa Afya. Wote hao, isipokuwa Maalim Seif, mzaliwa wa kisiwani Pemba, wanatoka Unguja.

Ni dhahiri baada ya Wapemba kutengwa na SMZ, kwa kutopewa vyeo, wengi wao walikuwa walimu na waliwekeza katika kusomesha watoto wao kwa vile wale Waunguja walikuwa wakiwania vyeo tu hata kama hawakuwa na sifa.

Changamoto hii iliamsha Wapemba wengi kupata nafasi za kusoma kwa kuwa walikuwa na sifa kinyume na wenzao wa Unguja waliokimbilia madaraka na kuajiriwa Tanzania Bara kutokana na elimu yao.

Ali Hassan Mwinyi alipokuja kuwa Rais wa Tanzania mwaka 1985, na kwa kuwa aliamua kufungua milango ya biashara Bara, baada ya kutanguliwa na Zanzibar iliyofungua mwanzo mwaka 1984, kulifanya wimbi kubwa la wafanyabiashara wa Kipemba na Wahindi kutoka Unguja kuhamia Dar es Salaam na miji mingine kama Mwanza, kwa ajili ya kuendesha biashara na kuweka makazi ya kudumu.

Na kwa kuwa Watanganyika wengi walikuwa hawajapata ujuzi wa kuendesha biashara, Wapemba wengi walizama hasa katika biashara kama za kilimo, dhahabu na nyenginezo.

Sasa iweje Wapemba waongoze kupinga Muungano ambao unawanufaisha?

Mfanyabiashara mkubwa wa Dar es Salaam, Said Salim Bakhressa anatokea Unguja na ni Mwarabu. Hata wasomi wakubwa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kama marehemu Prof. Haroub Othman na Prof. Abdul Sharrif, pia wanatoka Unguja.

Sasa ukiangalia Muungano huu, unanufaisha watu wa pande zote yaani Tanganyika na Zanzibar na siyo Wapemba tu kama alivyoandika Kicheere. Angekuwa anajua, Waunguja ndio wanaoongoza hasa katika kudai kubadilishwa mfumo wa Muungano.

Mwakilishi wa Jimbo la Kwamtipura (Unguja), Hamza Hassan Juma na Mansour Yusuf Himid, waliokuwa mawaziri katika Serikali ya Amani Abeid Karume (2000-2010) ni makada wakubwa wa Chama cha Mapinduzi (CCM).

Hamza amebaki mwakilishi wakati Mansour, ambaye pia ni mwakilishi (Kiembesamaki), amepumzishwa juzi tu uwaziri katika serikali ya Dk. Ali Mohamed Shein.

Mzee Jumbe pia alimpinga Mwalimu Julius Nyerere kuhusu mfumo wa Muungano, hatua iliyosababisha alazimishwe kujiuzulu mjini Dodoma mwaka 1984.

Na kama mwandishi Kicheere anawaita Wapemba tu ndio wapinga Muungano, anasemaje kuhusu wale wabunge wa 1990-95, waliotaka kurejeshewa Tanganyika yao?

Nawakumbuka Philip Marmo (Mbulu), Njelu Kasaka (Lupa) na Jenerali Ulimwengu (mbunge wa Taifa). Hata Mchungaji Christopher Mtikila akiwa na DP, aliunga mkono kundi hilo la G-55.

Mwandishi Kicheere anaposema wapinga Muungano ni Wapemba tu ndipo ulipo upotoshaji mwingine hapo.

0
No votes yet