Wazanzibari hawadai upendeleo, wanataka haki


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 20 April 2011

Printer-friendly version
Kalamu ya Jabir

WAZANZIBARI wanaweza kutafsiriwa vyovyote kuhusu hisia zao juu ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar, unaotimiza miaka 47 Jumanne ijayo.

Wanaonekana hawajatulia akili, walalamishi, wana jazba wanapozungumza, na wanafiki. Kwa hivyo, “watu wa kupuuzwa tu.”

Mwandishi mmoja, akijadili hivi karibuni matukio katika mjadala wa muswada wa sheria ya marejeo/mapitio ya katiba ya jamhuri, ameandika katika makala yake:

“...ingawa watu hawa (amelenga Wazanzibari wawili) wanataka kuwa na uhuru wa kusema kama katiba inavyotoa haki hiyo, bado hawako tayari wala huru kusikia kile ambacho hawakitaki, kwa maana hiyo katika dhana nzima ya demokrasia hawa si wanafunzi tu, ila wamefeli vibaya katika uwanja wa demokrasia.

Yeye alikerwa na mtu aliyechana muswada pale shule ya sekondari ya Haileselassie na aliyeuchoma moto kwenye mkutano wa hadhara wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), mjini Zanzibar.

Ukiwauliza Wazanzibari wenyewe, wanasema watafsiriwe vyovyote, ukweli unabaki palepale: “Zanzibar ni nchi yetu, na ni moja ya nchi mbili zilizounganishwa mwaka 1964 ndipo ikazaliwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kila ninaposoma au kusikiliza maelezo ya Watanzania wa Bara, napata picha kuwa Zanzibar inaonekana kero katika muungano kama vile iliomba kuungana. Kwamba inanufaika sana na muungano kiasi kwamba usipokuwepo, itapotea.

Kuwa kwao wachache na nchi yao ndogo mno kuliko Bara, hakutoshi kuwa sababu ya kubezwa. Kuwa watu wa kuchukuliwa kiwepesi; kuonekana hawana haki sawa na washirika wenzao wa muungano.

Imani hizi zinathibitishwa na matamshi na vitendo vinavyofanywa waziwazi. Mara kadhaa wakuu wa serikali ya muungano hutoa matamshi ya dharau kwa mamlaka ya Zanzibar na watu wake.

Kwa mfano, kuiita Zanzibar si nchi wakati inatambuliwa kama nchi hata kabla ya mabadiliko ya 10 ya katiba yaliyofanywa Agosti mwaka jana, ni dharau tupu.

Ni dharau kama ukweli una nguvu kuliko uongo. Kulingana na makubaliano yaliyozaa muungano, kila nchi itakuwa na sheria zake na mamlaka yake ya kuzisimamia. Ni kwa mambo yasiyokuwa ya muungano.

Ni imani hizi zinazokera Wazanzibari. Hawataki kudharauliwa hata kwa uchache wao au udogo wa nchi yao. Wakidharauliwa, ndipo huhoji maana ya muungano unaosababisha wadharaulike.

Kipo kitu ambacho wasiokuwa Wazanzibari, na hasa Watanzania wa Bara, hawajakielewa. Kwa hulka yao, Wazanzibari wanapenda kuelezea wanachokiamini kuhusu jambo linalowagusa wakiona linapelekwa sivyo.

Hufanya hivyo kwa moyo mweupe, ujasiri na bila ya kuogopa mtu.

Tatizo, wale wanaowachukulia kiwepesi wanapobaini kinyume. Wanajiuliza, “Kumbe Wazanzibari ni wakakamavu, wanajua haki zao na wakiamua wanazidai.”

Muungano wowote unatarajiwa kulenga kuendeleza walioungana. Wazanzibari wanaamini, na matukio yanathibitisha, ni muungano uliochangia wanyimwe haki zao na wakandamizwe.

Kwa kuwa wanajitambua na wanataka watambuliwe, wanatafuta kujinasua na minyororo inayowakaba. Kwa hilo, hawatalala na kusahau hatima yao.

Waafrika weusi wa Afrika Kusini walipokuwa wanakandamizwa na makaburu hawakulala. Warhodesia, sasa Zimbabwe, hawakulala. Hata Watanganyika, hawakulala.

Wazanzibari wanajua ndani ya visiwa vyao vya Unguja na Pemba, kuna raslimali nyingi – bahari, ardhi nzuri, misitu, wanyama wadogo, mafuta, na utajiri wa raslimali-watu. Hizi zingetumika vizuri na kwa uhuru, wangekuwa mbali kimaendeleo.

Leo, wanajua hawawezi kujenga kiwanda mpaka Dar es Salaam (Dar) waridhie, hawajengi ushirikiano/uhusiano na nchi nyingine mpaka Dar waidhinishe, vijana wao hawasomi nje mpaka Dar watake, hawachagui na wakichagua, ikiwa tu ametoka CCM, aweza kuondoshwa Dodoma.

Watu wanaoishi katika utajiri wasioweza kuutumia kujijenga kiuchumi mpaka fulani aridhie, si huru. Kuwataka watulie ni ujinga.

Wazanzibari hawajadai hata siku moja kupendelewa. Wanachotaka ni haki yao kama washirika wakuu. Wakae na Watanganyika, siyo Muungano; Tanganyika, wasikilizwe.

Wanataka heshima, uwazi na uadilifu katika kuendesha muungano huuhuu wa mfumo wa serikali mbili. Kwa kuamini hawajatendewa haki, ndio maana wengi wanadai serikali tatu.

Ukiwa na Zanzibar na ikifichuliwa Tanganyika, iiitwe vyovyote watakavyoamua wenyewe, unakutanisha washirika. Tangu 1964, kinachotokea ni kukutanisha mzazi (Zanzibar) na mzaliwa (Serikali ya Muungano). Yuko wapi mzazi mwenzake (Tanganyika)?

Somo kuu: Muungano umekuwa ukiendeshwa kimabavu tangu ulipoasisiwa.

Ili unayesoma hapa, hasa ndugu yangu wa Bara, upate picha kamili ya ninachokieleza, hebu tuingie darasani kidogo. Chukua karatasi na kalamu. Niandikie idadi ya mambo ya muungano. Nataka idadi tu wala usitaje mambo yenyewe.

Swali hili nalitupa pia kwa wabunge wa bunge la Jamhuri ya Muungano. Waziri Mkuu, mawaziri na mwanasheria mkuu wa serikali, wafanye hivyo. Ili kupata ulinganisho, mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, makamu wawili wa rais na mwanasheria wa SMZ, nao wajibu.

Kila mmoja ampe jibu lake mtu aliye karibu naye. Kwa wale mtakaotofautiana jibu, amueni cha kufanya. Bali wale mtakaolingana, nitumieni jibu lenu. Hiyo itakuwa elimu kubwa kwangu. Nitaitoa kwa wasomaji wengine.

Najua hata marais na mawaziri watatofautiana. Wanasheria walio wachambuzi na wachokonozi, wanatofautiana kwa hili.

Niliwahi kuhudhuria mkutano mmoja mwaka 2004 uliojadili Muungano. Mtoa mada ambaye ni mwanasheria, alitoka na mambo 42. Mjadala ulikuwa mkali, wengine wakisema ni 32, au 23, au 21 au 18.

Mchangiaji mmoja akahitimisha, “Sasa kama mambo ya muungano hatuyajui idadi yake, turudi tulikotoka. Mkataba wa muungano una mambo 11 tu.

Huu ni ushahidi wa namna muungano unavyoendeshwa kihuni kama ulivyoasisiwa. Turekebishe sasa.

Kama kuna makosa yalifanywa, kizazi kilichopo hakipaswi kuyaacha. Kwani tukianza upya tutapoteza nini kama nia ni muungano unaonufaisha pande zote? Tutakuwa na muungano wa maridhiano badala ya unaotutenganisha na kutugombanisha.

Uonapo mwanasheria mkuu wa serikali na waziri wa katiba na sheria wanalalamika Zanzibar haikushirikishwa katika kuandaa muswada wa sheria wa katiba, huelewi?

Yule anayedhani ni kitu kidogo kuishirikisha Zanzibar katika kupata utaratibu wa kuifikia katiba mpya, akubali waseme. Hapa Wazanzibari wanataka haki yao siyo upendeleo.

Katiba ya muungano itaandaliwa na watu walioungana. Anayeona hila zimeanza asubuhi katika suala hili, anakosea wapi kuchana/kuchoma muswada wa sheria anayojua imemtenga?

Mabadiliko ni muhimu. Lakini hayaji hivihivi. Yanahitaji viongozi wanaosikiliza na kuzingatia vilio vya raia. Viongozi wanaoheshimu haki na kuishuhudia inatendeka.

Mabadiliko ya Tunisia yalitokeaje? Labda watu wamesahau. Wala si kwa kuchana muswada. Hilo ni dogo tu kama mtu alisigina katiba ya nchi pale Jangwani, Dar es Salaam.

Kijana mlalahoi mjini Tunis alijiteketeza kwa moto kupinga udhalimu. Alikuwa anapinga kudharauliwa na viongozi wa jiji waliomvunjia biashara yake. Alichagua kufa. Aliamini hiyo ndiyo afadhali yake. Leo, Tunisia wanapanda mbegu za demokrasia pana.

Pale ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam, baba mmoja akitoa maoni, alisema: “Zanzibar wana katiba yao ya mambo yao. Tumeungana sawa. Lakini sisi hapa tunataka hii iwe katiba ya muungano. Iwe ya mambo yanayotuhusu sisi tu watu wa Tanganyika. Haya muyaweke vizuri tuelewane.”

Je, Sheikh Farid Hadi Ahmed wa JUMAZA? “SMZ iukatae; iitishe kura ya maoni kutuuliza kama tunataka au hatutaki muungano. Serikali ya Muungano irejeshe Katiba ya Tanganyika, kabla ya mjadala wa muswada wa katiba kufanyika. Zama za udikteta wa milele zimekwisha.”

Wote wawili wanautaka muungano lakini wanataka muungano wa haki na endelevu. Muungano huo utakuja kwa kujali haki siyo ubinafsi.

0
Your rating: None Average: 5 (1 vote)