Wazazi walea ngono shuleni Masasi


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 09 September 2008

Printer-friendly version

HUYU hapa ni injinia wa ujenzi wa barabara. Siku tatu zilizopita alirejea nyumba ya wageni usiku, mjini Masasi, ambako alikuwa amepanga, akiwa na msichana wa umri mdogo. Binti huyo alilala pale na kuondoka kesho yake.

Sasa sikiliza anavyosema injinia huyo anayefanya kazi kwenye ujenzi wilayani Masasi. “Hebu niwachekeshe. Yule binti niliyelala naye juzi, nimekutana wanafunzi wakimkokota; wanampeleka shule,” anasimulia.

Kila mmoja wetu alikaa kimya akisikiliza. Ndipo aliongeza, “Kumbe ni mwanafunzi. Naambiwa alikuwa hataki hata kwenda shule. Ilibidi wanafunzi wenzake wamfuate nyumbani, kumvalisha nguo kwa nguvu na kumkokota hadi shuleni.”

Hiyo ndiyo hali inayojidhihirisha mjini Masasi na vijiji vya Mbonde na Malika ambavyo mwandishi wa habari hizi alitembelea na kuongea na wakazi wake.

Wanafunzi wa kike katika maeneo haya ya mkoa wa Mtwara wanafanya ngono kama “mchezo wa bembea.” Baadhi wanadai hakuna wa kuwatisha wala kuwazuia.

Ni kweli. Katika shule ambazo mwandishi amefanya uchunguzi, kuna maelezo mengi juu ya sababu za wanafunzi kujihusisha sana katika ngono na kupata mimba; hatua ambazo wanachukua kudhibiti hali hiyo.

Kwanza, walimu wanasema wazazi wanatoa “uhuru” mwingi kwa watoto wao wa kike; kwenda wanakotaka na wakati wowote; na kurudi nyumbani usiku sana au kurudi asubuhi bila kuwauliza au kuwachukulia hatua.

Pili, baadhi ya walimu na viongozi wa kata na wilaya wanasema umasikini ndio chanzo cha wazazi kutotilia maanani ulinzi wa watoto wao – wa kike na hata wa kiume.

“Chanzo kukibwa cha mimba za wanafunzi ni umasikini wa familia; kwani watoto wanapofanya ngono hupewa fedha na baadhi ya fedha hizo hupelekwa kwa wazazi wao. Hili likiendelea, linageuka kuwa utamaduni,” anaeleza Husein Salum Mrekoni, Afisa Mtendaji wa Kitongoji cha Mkomaindo.

Mrekoni anasema wilayani Masasi hakuna mwamko mkubwa wa elimu. “Watu hawana wivu wa elimu,” anasema na kuongeza kuwa hata watoto wao wakipata mimba inakuwa vigumu kwao kuelewa kwamba wamepoteza kitu muhimu maishani.

Kwa upande wa walimu, maelezo ni kwamba wamekuwa wakiwafafanulia wanafunzi umuhimu wa elimu na wakati mwingine kutumia adhabu ya viboko kupambana na utoro na uchelewaji shuleni. Wanasema hilo lingewasaidia zaidi wasichana.

Hata hivyo, baadhi ya wanafunzi waliohojiwa wamesema hata viboko vinaweza kusababisha wanafunzi kuogopa kwenda shule; hivyo wakatoka nyumbani na kuishia njiani ambako wanajiingiza katika vitendo vya ngono.

Aidha, hivi sasa kuna asasi ya kijamii mjini Masasi inayotwa PASHA ambayo inapasha elimu wilayani humo juu ya kuzuia miemuko ya mwili na madhara yatokanayo na ngono isiyosalama.

Kwa mujibu wa Mwalimu B.R. Shauri, anayefundisha Shule ya Sekondari ya Kutwa ya Masasi na ambaye ni katibu wa PASHA, asasi hiyo inadhaminiwa na asasi ya GTZ kutoka Ujerumani.

Baadhi ya wanafunzi waliohojiwa kuhusu elimu inayotolewa na PASHA wamesema kuna walimu wanaowambia kuwa “kila mmoja ana haki ya kufanya ngono,” hivyo kufanya baadhi yao kuingia mitaani kwa madai kuwa wameruhusiwa na wataalam.

Hii ina maana somo la “haki ya ngono” halijaeleweka vema hasa kuhusu umri, mahali, wakati (mwanafunzi) na madhara yatokanayo; kama vile maabukizi ya magonjwa mbalimbali kama HIV/UKIMWI na mengine yanayoharibu uzazi na kulemaza viungo.

Tatizo jingine katika kukabiliana na ngono za utotoni na hasa shuleni limekuwa kile ambacho wengi wameita “imani za ushirikina.”

Mwalimu wa Shule ya Msingi ya Mkarango, akielezea kisa kilichotokea katika Shule ya Msingi Njisa, ana haya ya kusimulia: “Mimi na familia yangu tulikwenda kulala. Sote tukiwa na nywele kichwani. Asubuhi tulipoamka, sote tulikuwa vipara,” anasimulia mwalimu huyo.

Kitendo hicho kinahusishwa na ukali wa mwalimu katika kukazania wanafunzi wa kike kuhudhuria shuleni na kuwapa adhabu wale ambao hawafuati taratibu na kanuni.

Mwaka 1984 mwalimu mwingine wa shule hiyohiyo  alikumbana na masaibu baada ya kukataa shinikizo la wazazi kutaka asiadhibu watoto wao watoro.

“Mwalimu na mkewe walikwenda kulala. Asubuhi yake wakajikuta wamelala katikati ya uwanja wa shule – yeye na mkewe – wakiwa wamenyolewa nywelenywele za sehemu zao nyeti,” ameeleza mwalimu mmoja huyo.

Matukio kama hayo yamekuwa yakitumika kama rejea kwa walimu mbalimbali. Inasimuliwa kuwa baadhi ya walimu walijikuta wamelala kwenye matawi ya miti; wao na familia zao. Kisa? Wamekuwa wakali kwa watoto wa kike na kwamba hizo ni adhabu wanazopewa na wazazi wa watoto hao.

Matukio hayo yamefanya walimu kushindwa kutekeleza kanuni za shule. Wameogopa kutoa adhabu. Wapo waliohama na wengine wameamua kutulia wakijisemea, “Nimekuja mzima na nataka kuondoka kama nilivyokuja.”

Walimu wanapokata tamaa, wanafunzi watoro hupata fursa ya kutoroka au kutokwenda shule. Hapo wazazi wasiojali wala kuthamini elimu, hupata mwanya wa kuwatumia watoto wao wa kike kukusanya “mafao” dhalili kutokana na ngono isiyosalama.

Vitisho ni vingi. Vinafanyika wakati wazazi wanapokutana na walimu kujadili tabia za watoto wao. Baadhi ya wazazi hutishia walimu kuwa “watakiona” iwapo wataendelea kuwaadhibu watoto wao.

Hayo yanafanyika wilayani Masasi ambako wakazi wake ni Wamakuwa, Wamakonde, Wamwera na Wayao. Wengi wa wanaume wanaowapa wasichana ujauzito, ama huhama mjini au kijijini.

Shule zenye matukio ya kutatanisha ni zile za vijijini kama vijiji vya Malika na Mbonde na zile zilizoko kwenye viunga vya mji wa Masasi zikiwemo za kitongoji cha Mkomaindo na Nyasa West.

Angalau mwanafunzi mmoja wa kike amekiri kuanza kufanya ngono akiwa na umri wa miaka 11. Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na mwandishi huyu, katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Masasi, asilimia 91 ya wanafunzi wamesema tayari ni wazoefu wa ngono na wengine wakisema wameanza toka wakiwa darasa la nne.

0
No votes yet