Wazima moto wa M4C kwa fiksi


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 13 June 2012

Printer-friendly version

MOTO mbaya. Usiombe mtu akaipiga kiberiti nyumba yako. Mayowe ya “woooo, uuuii, jamani nakufaaaa…” yatahanikiza na kuomba msaada.

Itakuwa hekaheka tupu. Kuna kuchanganyikiwa, na kwa kiwewe, unaweza kuokoa mdoli badala ya mtoto wako.

Balaa kubwa kama kuna upepo mkali; kazi ya kuzima inakuwa ngumu, cheche huruka na kutua vichwani na katika vitu vilivyookolewa, na nyumba nyingine.

Mkiita zinamoto wanaweza kuwapa maudhi. Si ajabu magari yao hayana maji au yana maji kidogo au wakifika mipira mifupi. Ndiyo maana, mara nyingi wanachelewa kwa kisingizio hawakupata habari mapema au umbali mrefu, na ‘migari’ yao inakimbia kilomita 10 kwa saa.

Kwa kujua udhaifu wa zimamoto jamaa wa M4C wiki mbili zilizopita waliwasha moto mkubwa pale Jangwani halafu wakatimua mbio kwenda kuchoma vibanda vya kusini.

M4C hawana gharama kubwa kuwasha moto. Kazi yao ni kuvaa magwanda, kuchukua kiberiti (hoja za msingi) na kuchoma kibanda cha muungano, kufafanua katiba mpya, kuorodhesha mafisadi, na kuwaumbua watawala na wajukuu wao wanavyokula nchi.

Wenye vibanda kusini wakatimua mbio kupoza mambo lakini wakakuta vijana wao wamevalishwa magwanda na wanaongoza njia kutoka kibanda (jimbo) kimoja hadi kingine.

Ndipo Jumamosi iliyopita zimamoto wakafika Jangwani na wataalamu wa fiksi na mabingwa wa kukariri mbu na samaki eti kukazima moto wa M4C.

Aibu, yule kijana wao anayezunguka nchi nzima kama tiara iliyokata kamba akawa anateua wa kuchota maji na kumwaga.

Yule kijana anajua kuzungumza; anazungumza lakini hakawii kulikoroga. Akasema niseme nisiseme? Wale wanaoamsha watu kuhusu muungano kule Zanzibar majambazi!

Kule Misenyi alijisahau, badala ya kuchota maji yeye alichukua mafuta ya taa na kuwarushia vijana wenzake.

Eti “…hata wote mkiondoka nikabaki peke yangu, Sisiem haitakufa…” Hee, kumbe hana imani hata na mwenyekiti wake, katibu mkuu na wakubwa wengine?

Turudi Jangwani. Watu wakasubiri kasi ya uzimaji moto wa M4C. Hawakuona ila walijikuta wakisomewa Bajeti ya kesho, basi.

Wakapangwa waliosomea kila kitu hadi hawajui kama hawajui kitu – maprofesa na madokta – waliopewa kazi ya zimamoto.

Alianza Profesa mmoja akasema yeye atachimba visima kila kitongoji. Akaja Profesa mama akasema atageuza Kigamboni kama Dubai au Singapore. Akaja Stopper Mwenye Hasira.

Jamaa ana hasira! Akasema sirikali itaanzisha kilimo cha ‘mchele’ kiasi cha hekta laki moja na itajenga viwanda vitano vya sukari, Rufiji, Kilombero, Wami, Kagera na Malagarasi kote viwanda ili sukari iwe kama mchanga.

Alipoona hashangiliwi akasema, “…natoa laana. Huyu mwenyekiti wa M4C atapata laana.” Eti laana hiyo ni kudai kwake kuwa sirikali inaibia wananchi hali ya maisha ngumu.

Ninavyojua, Stopper Hasira aliwahi kufungiwa miaka mitano kwa kutoa rushwa ya uchaguzi na alipoona aliopigania nao uhuru hawamjali akaamua kujiunga na ‘Sisiara Mageuzi’ akidhani angepata cheo. Akashiriki kuilaani Sisiem kinoma. Alipoona anakufa njaa alirudi akawalamba miguu wenzake wakampokea na kumpa kacheo asiiumbue.

Ila kwa staili ile naye amewasha moto wa dharau, kejeli badala ya kujibu hoja. Asije akakimbilia kortini kushtaki akizidiwa.

Daktari mmoja bingwa wa fiksi akasema atanunua feri mbili kwa ajili ya kusafirisha abiria kutoka katikati ya mji hadi Bagamoyo. Mwenzake akaandika meseji na kuwatumia makuli akisema ameota wanafanya makosa.

Hadi wanaondoka Jangwani hawakuonyesha uongo wa M4C kwani bei ya mchele kilo imebaki Sh. 2000; sukari Sh. 2000, unga Sh. 1000. Wanalo hilo!

0658 383 979
0
No votes yet