Waziri Kamala acha udanganyifu


Mwandishi Maalum's picture

Na Mwandishi Maalum - Imechapwa 27 October 2010

Printer-friendly version

UMEJITOKEZA utamaduni wa baadhi ya watu nchini kujifanya wamesoma na wana haki ya kusema chochote na jamii ya Kitanzania wajibu wake ni kutii na kusikiliza nini wanaojiita wasomi hasa wanasiasa wanachokisema, hata kama suala linalojadiliwa halihitaji elimu ya chuo kikuu.

Sote tumemsikia Diodurus Kamala, Waziri wa Afrika Mashariki ambaye amepoteza nafasi ya ubunge katika jimbo lake la Nkenge akimwambia Dk. Willibrod Slaa asiongee kitu chochote kuhusu uchumi eti si mchumi.

Alikuwa akimjibu Dk. Slaa aliyesema katika mahojiano na ITV na kwenye mikutano yake ya hadhara kuwa akipewa ridhaa ya kuiongoza nchi, atahakikisha kuwa sementi na saruji zitashuka hadi kufikia Sh. 5,000.

Kamala, katika kujibu hoja nzito, alitoa majibu rahisi na ya kitoto kwa kusema kuwa sementi haiwezi kushushwa kutoka bei ya sasa hadi kufikia Sh. 5,000 kwa madai eti ni makubaliano ya Afrika Mashariki.

Kitu ambacho Kamala ameshindwa kuelewa ni kwamba Watanzania hawataki kuingia kwenye Jumuia ya Afrika Mashariki inayowaumiza. Katika hili, Kamala anawezaje kusema Dk. Slaa asiongee mambo yanayohusu uchumi eti kwa kuwa siyo mchumi?

Kama Kamala alikuwa anamaanisha Dk Slaa si mchumi kwa kuwa hana shahada ya uchumi ni sahihi, lakini ajue Dk. Slaa ni msomi wa shahada ya udaktari wa falsafa katika fani ya sheria tofauti na yeye aliyeanza kujiita ni daktari wakati hakuwa na sifa hiyo.

Kila mtu anajua kuwa hata chuo alichosomea udaktari Kamala hakitambuliki. Pia ni vyema Kamala akaelewa kuwa hoja ya Dk. Slaa kupunguza bei ya sementi au kutoa elimu bure hadi kidato cha sita haihitaji kwenda chuo kikuu kuelewa kwani tatizo la Tanzania sio fedha bali ni matumizi mabaya ya fedha.

Kwa hiyo, ayasemayo Dk. Slaa yanawezekana ikiwepo serikali safi inayosimamia vyema matumizi ya fedha na kukusanya kodi na kuziba mianya ya ufisadi.

Lakini mbona Kamala mwenyewe hana shahada ya uchumi toka chuo kikuu ila ana diploma ya juu kuhusu mipango ya uchumi (advanced diploma in economic planning) kutoka iliyokuwa Taasisi ya Maendeleo (IDM) na shahada mbili za uzamili (masters) zote kwa pamoja hazihusiani na uchumi.

Kamala si miongoni mwa magwiji wa uchumi kama Prof. Ibrahim Lipumba au Prof. Samwel Wangwe, na alipokuwa IDM alikuwa mhadhiri tu wa kawaida wala hakuwa mhadhiri mwandamizi.

Sasa nguvu ya kujiona yeye ni mchumi na msomi anaitoa wapi? Kwa kuwa na Advanced Diploma In Economic Planning ana tofauti gani na vijana wengine waliomaliza Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE)?

Inabidi Kamala ajue kuwa, kwa kujisifu kwake kuwa yeye ni msomi na kuwaona watu wote mbumbumbu ndicho kilichomfanya watu wa jimbo lake wakamkataa kwenye kura za maoni.

Pia kitendo cha yeye kujifanya kuwa mjanja na wengine wote wajinga kimemfanya ashindwe kura za maoni na mgombea wa kike ambaye hakusoma kama yeye lakini anaheshimu mawazo ya watu.

Kina marehemu Rashid Kawawa hawakuwa na elimu ya chuo kikuu chochote, lakini waliheshimika sana kwa kuwa walikuwa na mawazo ya kizalendo hadi akafikia kuwa Waziri Mkuu. Frederick Sumaye hakuwa na shahada lakini alikuwa waziri mkuu mzuri tu na mpaka leo anaheshimika.

Mwalimu Julius Nyerere alikuwa msomi sana lakini hakuna sehemu katika hotuba yake utamsikia akiwaambia watu wasiosoma kuwa hawana nafasi ya kutoa mawazo kwa kuwa hawajasoma au kusomea fani fulani.

Pia aliwachagua hata wasiosoma kuwa mawaziri. Sasa Kamala ana usomi gani wa kujivunia? Au anatapatapa baada ya kushindwa kura za maoni ili Kikwete amuone na kumteua?

Kamala ajiulize Prof. Jumanne Maghembe imekuwaje amefikia kusema serikali itatoa elimu hadi kidato cha nne kwa watoto wote bila kujali wamefaulu darasa la saba au la?

Haoni kuwa ni kutokana na mawazo mbadala ya Dk. Slaa ndiyo yameifanya serikali kukumbuka shuka asubuhi? Kumbe haya yote ayasemayo Dk Slaa yanawezekana. Kamala aache kudanganya wananchi!

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: